February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

THRDC YASAINI MAKUBALIANO YA MASHIRIKIANO BAINA YAKE NA MAHAKAMA YA ZANZIBAR

Na Loveness Muhagazi

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania kupitia tawi lake la Zanzibar (THRDC-Zanzibar), hii leo umesaini hati ya makubaliano (MOU) kati yake na Mahakama ya Zanzibar kwa lengo la kukuza na kuboresha mfumo wa utoaji haki na kukuza Haki za Binadamu Visiwani Zanzibar.

Tukio hilo la utiwaji saini hati ya makubaliano baina ya THRDC na mahakama Visiwani Zanzibar, limeshuhudiwa na Kaimu Jaji Mkuu wa Zanzibar, mahakimu, Mratibu Kitaifa wa THRDC pamoja na Mratibu THRDC- Zanzibar, baadhi ya Wajumbe wa bodi ya Mtandao wa THRDC kutoka visiwani Zanzibar, watumishi wa mahakama,  watumishi wa THRDC bara na Visiwani, pamoja na waandishi wa Habari kutoka katika vyombo mbali mbali vya habari nchini.

Akizungumza baada ya utiaji saini hati hiyo wa mashirikiano Mratibu THRDC – Zanzibar, Abdallah Abeid ameushukuru uongozi wa mahakama kwa kuona umuhimu wa kurasimisha mashirikiano yake na THRDC, mashirikiano ambayo yamelenga kuisaidia jamii ya wazanzibari kwa kiasi kikubwa.

“Tukio hili limekuja baada ya kazi nzuri tuliyokwisha kuanza kwa kushirikiana na Mahakama na tumeona kwamba inazaa matunda na tukaona bora tuirasimishe. Nisisitize kwamba mahusiano haya yanakwenda kujenga mfumo imara zaidi wa utoaji haki na wanufaika wa moja kwa moja ni wananchi” Ameeleza Mratibu THRDC- Zanzibar

Pamoja na hayo Bw. Abeid ameongeza kuwa THRDC imejipanga kuhakikisha inashirikiana na Mahakama na serikali kwa ujumla kuhakikisha jamii ya wa Zanzibari inahudumiwa ipasavyo;

“THRDC tumejitoa moja kwa moja kushirikiana na Mahakama kuhakikisha mfumo wa utoaji haki unaimarika na kufanya kazi vizuri visiwani Zanzibar, ni imani yetu kwamba mashirikiano haya yatazaa matunda na tunajivunia makubaliano haya ya miaka mitatu. Tunaishukuru Mahakama kwa kujenga imani ya kushirikiana na sisi kufanya kazi na kuhakikisha tunaimarisha mifumo ya utoaji haki hapa Zanzibar” Abdallah Abeid, Mratibu THRDC- Zanzibar

Naye Mratibu wa Kitaifa wa THRDC, Onesmo Olengurumwa alimshukuru Mh. Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dr. Hussein Mwinyi kwa kuweka mazingira mazuri ya Serikali ya Zanzibar na tasisi zake kufanya kazi kwa karibu na Asasi za Kiraia.

Olengurumwa alisema kuwa kwa muda mfupi tangu kusajiliwa kwa tawi la THRDC visiwani Zanzibar,  Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu umefanya kazi za ushirika na tasisi nyingi za serikali na wanategemea kufanya mengi kwa malengo ya kuwaletea maendeleo wazanzibari ikiwamo kukuza  usawa na  haki za binadamu.

Akizungumza na vyombo vya habari, Kaimu Jaji Mkuu wa Zanzibar Khamis Ramadhani Abdallah ameeleza mikakati ya Mahakama katika kuboresha huduma zake kwa wananchi na hasa kwa kuzingatia haki za binadamu;

“Mahakama imedhamiria kufanya maboresho ya utendaji wake. Kama nilivyoeleza mahakama imekumbwa na matatizo mengi, kwa hiyo tumedhamiria kuyaondoa kabisa hayo matatizo ili wananchi wapate kufaidika na huduma zinazotolewa na mahakama na kupunguza malalamiko”Khamis Ramadhani Abdallah Kaimu Jaji Mkuu Zanzibar

Katika kutatua changamoto mbali mbali ambazo zimekuwa zikilalamikiwa na wananchi Mahakama imeeleza kuwa imeunda kamati mbali mbali. Kamati hizo ni pamoja na kamati ya Maboresho ya mahakama ambayo inasimamiwa na mwenyekiti Mh George Kazi, kamati ya ICT na Takwimu, kamati ya tafiti na usimamizi, kamati ya sheria na miongozo, na kamati ya mafunzo ambazo zote hizo zimepewa wasimamizi ili kuhakikisha Mahakama inatatua changamoto inazopitia.

“Mahakama haiwezi kutembea peke yake, tupo chini ya serikali lakini kuna wadau wengine ambao tunashirikiana nao kuhakikisha tunafikia lengo letu la kufanya maboresho, mojawapo ya wadau waliojitokeza ni Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) ambao kupitia tawi lake la Zanzibar wamekuja na kuanza kushirikiana nasi” Khamis Ramadhani Abdallah, Kaimu Jaji Mkuu wa Zanzibar

Ameongeza kwa kueleza namna makubaliano hayo yatasaidia kuboresha maeneo mbali mbali ikiwa ni pamoja na;

1)    “Kujenga uwezo wa kutoa haki katika jamiii, “tutashirikiana katika mambo mbali mbali, yakiwemo kwanza kufanya tafiti na kutengeneza ‘document’ itakayoainisha changamoto zinazoikabili mahakama na namna ya kuzitatua”.

2)    Ufanyaji tafiti katika maeneo mbali mbali ikiwemo maswala ya udhalilishaji wa kijinsia, “tunaweza kufanya tafiti za sababu za ukatili wa kijinsia tatizo ambalo lipo katika jamii yetu na namna ya kukabiliana nalo.”

3)    Usimamizi wa mashauri (case management), “tunajua kuna tatizo la usimamizi wa mashauri, yapo malalamiko kwamba mashauri hayaendi kwa haraka, hukumu hazitoki kwa haraka, ‘proceedings’ hazitoki kwa haraka, kwa hiyo katika mashirikiano yetu tutatafuta namna nzuri na ya kisasa ya kusimamia mashauri yetu.”

4) Kushirikiana katika kuendesha semina na ‘refresher Courses’ kwa lengo la kuboresha huduma za kimahakama.  Alisema Kaimu Jaji Mkuu

Baada ya kusaini mkataba huo, THRDC na Mahakama imeazimia kutafuta Mshauri Elekezi atakayefanya utafiti na kuandaa ripoti itakayosaidia kuandaa mpango mkakati wa maboresho ya Mahakama utakaotumika kwa muda mrefu kuhakikisha mahakama inaendelea kuboresha huduma zake kuzingatia haki za binadamu.

Hatua hii ni mwendelezo wa THRDC wa kushirikiana na mamlaka mbali mbali kuhakikisha kunakuwa na uzingatiwaji wa haki za binadamu pamoja na uboreshwaji wa utolewaji huduma zinazozingatia haki za binadamu katika maeneo mbali mbali nchini Tanzania lakini pia makubalianao haya yatatumiwa na wanachama wa THRDC zaidi ya 200 waliosambaa Nchi nzima kushirikiana na Mahakama katika kuhakikisha kunakuwa na huduma stahiki zenye kuisaidia jamii ya watanzania.

Januari 14, 2022