February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

THRDC YAMTAMBUA DKT HELLEN KIJO BISIMBA KUWA MTETEZI WA MAISHA WA HAKI ZA BINADAMU

Mtandao wa watetezi wa haki za binadamu Tanzania (THRDC) umeungana na Dunia kuadhimisha siku ya wanawake duniani huku ukimtambua mwanaharakati mahiri na Mtetezi wa haki za binadamu DKt. Hellen Kijo Bisimba kama Mtetezi aliyetoa maisha yake yote katika kulinda na kutetea haki za binadamu.

Katika kusherehekea siku hii THRDC, imempatia Dkt. Bisimba tuzo kama ishara ya kutambua utumishi wake uliotukuka kwa sekta hasa katika kutetea haki za binadamu kwa miaka zaidi ya 30 bila kuacha Wala kuyumba.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wadau wa utetezi wa Haki za Binadamu wamempongeza Dkt. Hellen kwa kuwa mfano bora kwa vizazi vya sasa ambavyo vinapata fursa ya kuiga mfano bora wa kusimama imara katika shughuli za utetezi wa haki za binadamu bila kuyumbishwa Wala kukatishwa tamaa.

Akizungumza kwa niaba ya Mtandao, Mratibu kitaifa wa mtandao wa watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania THRDC, Onesmo Olengurumwa amempongeza Dkt. Bisimba kwa Kuwa mfano wa kuigwa kwa vizazi vya sasa lakini pia ameeleza kuutambua umuhimu wa mchango wa wanawake katika maendeleo yoyote.

“Watetezi wa Haki za binadamu wanawake ni watu ambao hawayumbishwi, wapo ‘focused’ wakiamua kusimamia maswala ya utetezi wanasimama imara, hii imeonekana hata kwenye hama hama za vyama wanawake wameonyesha mfano kwa kusimama na vyama vyao waliohama wengi ni wanaume, hii inatudhihirishia Kuwa wanawake Wana msimamo, hawayumbishwi hasa tunapokuja katika swala la haki za binadamu. Hivyo sisi kama THRDC tumaamini Ili tuweze kufika mahali au hata kama Nchi tunatakiwa kiwazingatia wanawake zaidi, hivyo tunatakiwa kuendelea zaidi na zaidi kutambua michango iliyotolewa na dada zetu kwa zaidi ya miaka 20 au 30 iliyopita” Olengurumwa

Kwa upande wake Kamishna Nyanda Shuli kutoka tume ya haki za binadamu na utawala bora (THBUB) ameeleza mchango wa wanawake katika maendeleo yake kama mwanaume kuanzia alipoanza taaluma yake ya uandishinwa habari hadi sasa.

“Mpaka leo nipo hapa ni kwa sababu niliaminiwa na kufundishwa na kina mama mahiri. Tume inaamini Kuwa ni lazima tutetee wanawake kwa Kuwa tumaamini lazima ifanyike njia ya ziada, ya kufuatilia, kutambua na kulinda Haki zao.” Nyanda Shuli, Kamishna wa Tume.

Baada ya kupokea tuzo hiyo Dkt. Bisimba ameushukiru Mtandao kwa kutambua mchango wake katika sekta hii ya haki za binadamu na kukiri kuwa tuzo hiyo imeongeza mzigo wa Ari yake ya utetezi wa Haki za binadamu hata baada ya kustaafu. Dkt. Bisimba Ameongeza kwa kuwataka watetezi wa haki za binadamu na wananchi wote kutofumbia macho vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu ambavyo kwa kiasi kikubwa vimekuwa vikifanywa katika jamii yetu.

Akizungumza wakati wa uhairishwaji wa hafla hiyo Mwenyekiti wa Bodi ya Mtandao wa THRDC, Jaji Mstaafu Joacquine De Melo amewataka watetezi wa haki za binadamu nchini kuiga utaratibu wa kuwatambua waasisi mbali mbali pindi wapo hai na kuutambua mchango wao katika maendeleo ya Jamii na kutosubiri mpaka kifo kisifia. Vile vile Hata hivyo Jaji De Melo ameupongeza Mtandao kwa Kuanzisha utaratibu wa kuwatambua watetezi wa haki za binadamu wenye mchango kwa jamii, huku akiwataka watetezi hao kusimamia ukweli na kutokuogopa kwani ukweli utawaweka huru.

Kwa kipindi cha miaka 10 sasa mtandao wa Watetezi wa haki za binadamu Tanzania umekuwa na utaratibu wa kuwatambua watetezi hasa wanachama na wadau mbali mbali wa Haki za binadamu ndani na nje ya nchi kwa kuwapatia tuzo mbali mbali katika maadhimisho ya siku ya watetezi wa haki za binadamu ambayo huandaliwa na Mtandao kila mwaka kama njia mojawapo ya kukuza ari na kutambua mchango wa wadau hawa katika shughuli za utetezi wa haki za binadamu nchini.

Mwaka huu Mtandao umepata fursa ya kutumia siku hii ya wanawake kutambua nafasi ya wanawake hasa mtetezi huyu nguli na mchango wake katika maendeleo ya sekta ya haki za binadamu nchini.