December 4, 2022

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

THRDC YALAANI UAMUZI WA KULIFUNGIA GAZETI LA UHURU,YATOA USHAURI KWA SERIKALI

Na Hilder Ngatunga

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umeeleza kusikitishwa na uamuzi wa serikali kulifungia gazeti la Uhuru linalomilikiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM)  kwa siku 14 na kusema kuwa haikuelezwa wazi kama gazeti la Uhuru lilipata nafasi ya kusikilizwa kabla ya kupewa hukumu hiyo.

Hapo jana Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo ,Gerson Msigwa hapo jana alitangaza kulifungia gazeti hilo baada ya kuchapisha taarifa ya upotoshaji kuhusu kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan wakati alipohojiwa na shirika la habari la BBC yenye kichwa cha habari “Sina wazo kuwania Urais 2025-Samia,” Taarifa ambayo imeelezwa kukiuka vifungu 50(1)(a),(b) na (d) na kifungu cha (52)(d) na (e)  vya sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016.

Taarifa iliyotolewa na THRDC hapo jana kutiliwa saini na Mratibu wa Mtandao huo,Wakili Onesmo Olengurumwa imesema serikali ingechukua hatua za kisheria kwa mwandishi aliyeandika habari hiyo na sio kulifungia gazeti kutofanya kazi kwa siku 14.

“Gazeti la Uhuru ni gazeti la kwanza kufungiwa kwa mwaka 2021, lakini tumeshuhudia kuwa kuna magazeti mengine yalikwisha kufungiwa kutokana na sheria hiyo ilipopitishwa mwaka 2016 ikwemo Tanzania Daima,Mawio, Mseto,Mwanahalisi,Raia Mwema,Mwananchi na The Citizen ambayo yalisimamishwa kwa muda,”imeeleza taarifa hiyo.

Aidha imeongeza kuwa vifungu vilivyotumika kulifungia gazeti hilo THRDC,LHRC na MCT mwaka 2017 vilishavipinga katika Mahakama ya Haki  Afrika Mashariki kwani ni Kinyume na Mkataba wa Afrika Mashariki na kuongeza kuwa Mwaka 2019 mahakama hiyo iliitaka serikali ya Tanzania kuondoa vifungu hivyo .

“serikali iheshimu uamuzi wa Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki na kuchukua hatua zote muhimu kuhakikisha Sheria ya Huduma ya vyombo vya Habari inalandana na Mkataba wa Afrika Mashariki,”

THRDC imeendelea kusisitiza kuwa Sheria ya Huduma za Habari ni miongoni ,wa sheria kandamizi na kusema serikali kutotekeleza hukumu iliyotolewa na Mahakama hiyo inatoa picha mbaya kwa taifa kwani serikali iliridhia kutia saini Mkataba wa Afrika Mashariki kwa nia njema.