Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), umelaani vitendo vya kukamatwa kwa watetezi wa haki za binadamu wanaofuatilia mgogoro wa ardhi katika Hifadhi ya Ngorongoro, mkoani Arusha.
Tamko hilo limetolewa hapo jana , tarehe 23 Machi 2022 na Kaimu Mratibu wa THRDC, Leopold Mosha, baada ya kuibuka madai ya kwamba kuna baadhi ya watetezi wa haki za binadamu na madiwani wa Wilaya ya Ngorongoro, wanasakwa na Jeshi la Polisi kwa ajili ya kuhojiwa juu ya mgogoro huo.
“Mtandao umesikitishwa na matukio yanayoendelea Wilayani Ngorongoro yanayohusisha kukamatwa kwa watetezi wa haki za binadamu. Leo Madiwani wa Kata ya Malambo, Joel Clemence na Mathew Siloma wa Kata ya Arash, wamehojiwa na Kamati ya Maadili ya Wilaya ya Ngorongoro katika ofisi za Chama Cha Mapinduzi (CCM), wilayani humo zilizopo Loliondo,” limesema tamko hilo.
Aidha, tamko hilo limedai THRDC imepata taarifa kwamba watetezi wa haki za binadamu katika eneo la kilomita za mraba 1,500 la Tarafa ya Sale na Loliondo, pamoja na madiwani wa kata za eneo hilo, wanasakwa na Jeshi la Polisi ili wakamatwe.
Tamko la THRDC limedai kuwa, tuhuma za kuhojiwa madiwani hao ni kutokana na kutetea haki za wakazi wa Loliondo na tarafa ya Sale, kutokuhamishwa kwa lazima kutoka kwenye eneo la ukubwa wa kilometa za mraba 1,500.
“Mtandao unatoa wito kwa Jeshi la Polisi kufuata taratibu zilizopo kisheria, endapo kuna uhitaji wa watetezi wa haki za binadamu kukamatwa na sio utaratibu unaotumika sasa wa kuwasaka watetezi wa haki za binadamu wilayani Ngorongoro,” limesema tamko hilo.
Habari Zaidi
DCI KINGAI ASISITIZA WAZAZI KUZINGATIA MALEZI BORA KWA WATOTO WAO ILI KUPUNGUZA UKATILI
THRDC,C-SEMA YAENDESHA MAFUNZO KWA POLISI NA WAENDESHA MASHITAKA