February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

THRDC, LHRC, SAVE THE CHILDREN WAFUNGUKA, WAPENDEKEZA SERIKALI KUKUBALI MAPENDEKEZO MUHIMU YA UPR YALIOACHWA

Na: Anthony Rwekaza

Baada ya Serikali ya Tanzania ambayo ni Nchi mwanachama wa Umoja wa Mataifa ambayo imekuwa ikishiriki katika mchakato wa Mapitio ya Haki za Binadamu, ikiwa imefanyiwa mapitio Novemba 5, 2021 na Baraza la kimataifa la Haki za Binadamu, Jumatano Novemba 10, 202 Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Kituo cha Sheria na Haki Binadamu Tanzania (LHRC), Asasi la Save the Children kwa kuungana baadhi ya Asasi nyigine wamelezea mchakato huo ulivyoenda na kutoa mapendekezo kwa Serikali.

THRDC, LHRC na Save the Children katika Tamko

Akizungumza na vyombo vya habari, Mratibu wa THRDC, Wakili Onesmo Olengurumwa akiwa pamoja na wenzake kutoka LHRC na Shirika la Save the Children wakiwa kwenye Ofisi za THRDC kitaifa, amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilipokea mapendekezo 252 kati ya hayo Serikali imeyakubali 108 sawa na 43% huku mapendekezo 12 sawa na 4.8% yanazingatiwa lakini mapendekezo 132 sawa na 52% hayajakubaliwa.

“Tanzania ikiwakilishwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi, ilipokea jumla ya mapendekezo 252, mapendekezo 108 sawa na 43% yalikubaliwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mapendekezo 12 sawa na 4.8% yanazingatiwa na mapendekezo 132 sawa na 52% hayakukubaliwa. ” amesema Mratibu wa THRDC, Wakili Onesmo Olengurumwa

Pia amesema kiwango cha asilimia za kukubaliwa kwa mapendekezo kumepungua kutoka 70% tokea Nchi ya Tanzania ilipoaza kufanyiwa mapitio kwa mihula mitatu ambayo mingine ni 2016 na mapitio ambayo ya mwaka huu 2021 ambayo mchakato wake haujakamilika rasmi lakini ukiwa unatarajiwa kukamilika siku chache mbeleni.

“Asilimia ya mapendekezo kukubaliwa imepungua kutoka 70% mwaka 2011, 58% mwaka 2016 mpaka 43% mwaka huu 2021. Mchakato bado haujakamilika kwa kuwa taarifa hii ni awali na taarifa rasmi na mwisho inategemewa kutoka siku chache zijazo.”amesema Mratibu wa THRDC, Wakili Onesmo Olengurumwa

Akiendelea kutoa ufafanuzi kwa niaba ya wenzake mbele ya wanahabari amesema idadi kubwa ya mapendekezo yaliyokubaliwa ambayo ni 108 sawa na 43% yalihusu haki za wanawake na watoto, haki za kijamii, ikiwa ni katika kuboresha wa huduma za kijamii ikiwemo afya na elimu jumuishi, haki za watu wenye ulemavu hususani watu wenye ualbino na haki ya maendeleo katika utekelezaji mipango ya maendeleo ya kitaifa na kikanda.

Lakini Wakili Onesmo Olengurumwa ameueleza umma kupitia wanahabari kuwa hidadi kubwa ya mapendekezo ambayo hayajakubaliwa yanahusu masula ya haki, ikiwemo haki za kiraia na kisiasa, haki ya kupata dhamana, watuhumiwa kutowekwa rumande kinyume na sheria, kufuta adhabu ya kifo pamoja na Tanzania kuridhia mikataba ya kimataifa,

Ambayo Wakili Onesmo Olengurumwa kwa niaba ya wenzake amesema inalenga kusaidia kukomesha vitendo vya utesaji wa binadamu, ameongeza kuwa pia mapendekezo juu ya kufanya mabadiliko ya sheria zinazohusu uendeshaji wa asasi za kiraia na kazi ya Watetezi wa haki za Binadamu, haki za wakimbizi, haki za watoto kwa kufanya mabadiliko ya sheria ya ndoa inayotafsiriwa kuwa inaruhusu ndoa za utotoni.

“Idadi kubwa ya mapendekezo ambayo hayajakubaliwa (132 sawa na 52%) yalihusu haki mbalimbali ikiwemo haki za kiraia na kisiasa ikiwemo haki ya kupata dhamana, kutowekwa rumande kinyume na sheria, ufutwaji adhabu ya kifo, pamoja na nchi kuridhia mikataba ya kimataifa inayolenga kukomesha vitendo vya utesaji binadamu pamoja na ulinzi dhidi ya kupotezwa; mabadiliko ya sheria zinazohusu uendeshaji asasi za kiraia na kazi za Watetezi wa haki za binadamu, haki za wakimbizi, haki za watoto kuhusu mabadiliko ya sheria ya ndoa ya 1971 dhidi ya ndoa za utotoni.” Amesema Mratibu wa THRDC, Wakili Onesmo Olengurumwa

Kwa umoja wao Asasi hizo zimesema kuwa, Tanzania ikiwa ni moja ya nchi mwanachama wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika, inao wajibu wa kuhakikisha kuwa hali ya haki za binadamu zinaimarika na kuzingatiwa, lakini wamesema pamoja na maboresho yanayoendelea kufanyika katika Nchi ya Tanzania, bado kuna changamoto nyingi za kisheria, kisera na mifumo inayoathiri haki za binadamu.

Aidha kutokana na hali hiyo asasi hizo zipendekeza kwa Serikali kuwa upo umuhimu wa kuangalia mapendekezo yaliyotolewa upya hasa yale yanayogusa haki za msingi, ili iweze kuridhia na kuyakubali kwa kuangalia maslahi mapana ya watanzania wakidai kuwa haki za binadamu ndiyo msingi wa maendeleo ya Taifa lolote.

Katika mchakato wa kutathmini mapendekezo yaliyotolewa kiujumla, Asasi hizo za kiraia zimepedekeza baadhi ya mambo wakidai ni hatua ya kuboresha hali ya haki za binadamu nchini kwa manufaa mapana ya Nchi na maendeleo ya watu kwa ujumla, wameshauri Serikali kuyakubali mapendekezo ambayo hayajakubaliwa lakini mlengo wake ni kugusa haki za kiraia na kisiasa ikiwemo haki mbalimbali ambazo alizitaja muwasilishaji mkuu Mratibu wa THRDC, Wakili Onesmo Olengurumwa kwenye mkutano na waandishi wa habari.

“Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ifikirie zaidi na kuyakubali mapendekezo ambayo hayajakubaliwa hasa yale yanayogusa haki za kiraia na kisiasa ikiwemo haki ya kupata dhamana, kutowekwa rumande kinyume na sheria, ufutwaji adhabu ya kifo, pamoja haki za Watetezi wa Haki za Binadamu na Asasi za Kiraia, Tanzania kuridhia mikataba ya kimataifa inayolenga kukomesha vitendo vya utesaji binadamu pamoja na ulinzi dhidi ya kupotezwa; haki za wakimbizi; haki za watoto kuhusu mabadiliko ya sheria dhidi ya ndoa za utotoni.” amesema Mratibu wa THRDC, Wakili Onesmo Olengurumwa

Vilevile Asasi hizo zimeishauri Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwashirikisha wadau wengine wa haki za binadamu hususani Asasi za Kiraia na Nchi wanachama zilitoa mapendekezo ili kujadili uwezekano wa kuyaboresha kulingana na mazingira halisia ya nchi, huku pia wakishauri Nchi wanachama waliotoa mapendekezo waangalie uwezekano wa kuyaboresha mapendekezo ambayo hayakukubaliwa na ambayo yanafikiriwa ili yaweze kukubaliwa, ikiwa ni baada ya uchambuzi wao kubaini mapendekezo mengi kuunganishwa katika pendekezo moja.

Hata hivyo wamependekeza kuwa Watetezi wa haki za binadamu wapitie rasimu ya ripoti ya kikao cha tatu cha Mapitio ya Hali ya Haki za Binadamu (Universal Periodic Review- UPR), ili kuwafanya mawasilisho mapema ya hoja zao kwa kuishauri Serikali juu ya mapendekezo yaliyotolewa, katika hatua hiyo wameshauri Watetezi hao kuchukua maoni kutoka kwa wadau mbalimbali kabla ya mawasilisho ya mwisho.

“Watetezi wa haki za binadamu wapitie rasimu hii ya repoti ya kikao cha tatu cha Mapitio ya Hali ya Haki za Binadamu (UPR) ili kuwasilisha mapema hoja zao ili kuishauri serikali juu ya mapendekezo yaliyotolewa, Hivyo tunawaomba viongozi wa mamlaka mbalimbali za serikali kuchukua maoni ya wadau mbalimbali ili kufanya marekebisho katika mapendekezo yaliyokataliwa kabla ya kutoa maamuzi ya mwisho” amesema Mratibu wa THRDC, Onesmo Olengurumwa

Ikumbukwe kwenye Mkutano wa tatu wa UPR uliofanyika Novemba 5, 2021 Tanzania iliwakirishwa na mjumbe Mkuu ambaye ni Waziri wa Katiba na Sheria Prof Palamagamba Kabudi ambaye aliambatana na timu ya wajumbe wengine ambapo alipata fursa ya kujibu maswali mbalimbali yaliyoulizwa, ikiwemo uchaguzi Mkuu wa 2020, haki za watoto pia masuala ya haki kwenye nyanja ya elimu.

Wakati mkutano huo ukiwa unaedelea Geneva Uswiz, Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) ambao una zaidi ya wanchama 200, uliwaalika wanachama hao kufuatilia kinagaubaga mkutano huo ili kuifahamu matipitio hayo, ambavyo THRDC pamoja na Asasi zinazotetea Haki za Binadamu zimekuwa zikishiriki katika hatua mbalimbali za mchakato wa UPR ikiwemo kuwasilisha maoni na kuwasilisha ripoti zinahusu haki za binadamu