February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

THRDC KWA KUSHIRIKIANA NA ABA WAMEENDESHA KIKAO CHA ROBO MWAKA JUU YA UHURU WA KUJIELEZA

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) kwa kushirikiana na Shirika la ABA wameendesha kikao kazi cha robo mwaka juu ya uhuru wa kujieleza ambapo jumla ya wajumbe 25 walishiriki kikao hicho kilichofanyika jijini Dar es salaam hapo jana .

Akizungumza katika ufunguzi wa kikao hicho cha siku moja,Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania,Wakili Onesmo Olengurumwa ameipongeza serikali ya awamu ya sita kwa mabadiliko makubwa ambayo imeifanya katika eneo la uhuru wa kujieleza.

“Niwapongeze kwa kushiriki katika kikao hiki kwa ajili ya kujadili masuala kadhaa yanayohusu haki ya kujieleza,mifumo,sharia mbalimbali inayosimamia uhuru wa kujieleza nchini.Tumeona mabadiliko makubwa sana katika eneo la uhuru wa kujieleza au haki za kujieleza na vyombo vya habari tunaona vyombo vya habari vingi vimeachiwa huru toka Rais samia ameingia madarakani,”amesema Olengurumwa.

Olengurumwa amepongeza jitihada zinazofanywa na Wizara ya Habari ya kutaka kufanyia maboresho ya sheria mbalimbali zinazoonekana kuminya uhuru wa kujieleza na masuala ya vyombo vya habari nchini na kueleza kuwa kwa Tanzania kukubali baadhi ya mapendekezo ya katika mkutano wa 49 mapitio ya Hali ya haki za Binadamu (UPR) uliofanyika Geneva juma liliopita inatoa mwangaza kuwa Tanzania inaelekea pazuri katika masuala ya uhuru wa kujieleza.

“Kimsingi tunakuwa na sababu kubwa ya kuona kwamba tunaelekea kuzuri katika eneo hili la haki ya kujieleza,kupata habari,kutoa maoni na vyombo vya habari.Pamoja na hayo hatupaswi kutulia au kusema kwamba kila kitu kimekwenda sawa tunapaswa kuendelea kufanya jitihada tunazoweza kufanya,”amesema Olengurumwa .

“Tumeona kwamba kila jambo linalofanywa sasa hivi na uongozi wetu kuanzia Rais mpaka Waziri wa habari tunaelekea katika safari nzuri sana ya uhuru wa kujieleza na habari, mpaka sasa hivi hatujaona matukio ya watu kukamatwa au watu kupotezwa au watu kufunguliwa kesi au vyombo vya habari kufungiwa kwasababu ya uhuru wao wa kujieleza hatujaona matukio hayo kuwa makubwa kama miaka mitano iliyopita ,” ameongeza Olengurumwa.

Hata hivyo Olengurumwa amebainisha kuwa licha ya jitihada kubwa zinazofanywa na serikali katika kuurudisha uhuru wa habari nchini kumekuwepo na changamoto kadhaa ikiwemo vyombo vya habari kutokuwa na uhuru wa kuripoti kuhusu mgogoro unaoendelea Ngorongoro.

“Tunapozungumza sasa hivi vyombo vya habari vina hali ngumu sana ya kutoa taarifa ya kule Ngorongoro ni kama vile vimepigwa ganzi au vimepigwa mkwara visitoe taarifa za wananchi kule Ngorongoro na wakati mwingine hata fedha zinatumika,” amesema Olengurumwa.

Amesema kuwepo kwa chnagamoto hizo huenda ni kwasababu ya uwepo wa watu wachache wanaodhani kuwa bado wapo kwenye zama za kuendelea na uminyaji wa vyombo vya habari na sio mfumo wa kitaifa.

“Wapo baadhi ya watu ambao wanataka tuendelee kuwa kwenye dhana ile au awamu ile ya kubania vyombo vya habari,kuminya uhuru wa wanahabari,kuminya uhuru wa watu kujieleza kuna watu bado wanaamini hivyo na mimi niwashauri tu kwamba sasa hivi tuko na uongozi mwingine wa Rais wetu mama Samia pamoja na wizara yetu ya habari ambayo wote kwa pamoja wanaamini katika kuleta uhuru wa vyombo vya habari,uhuru wa kujieleza na kulinda haki za watu na kutokuruhsu mtu yoyote kuonewa au chombo chochote cha habari kubanwa au kuonewa ,”ameongeza Olengurumwa.

Olengurumwa amesema kuwepo kwa ahueni ya uhuru wa habari nchini isiwe sababu ya watetezi wa haki za binadamu kukaa kimya bali ni wakati wa kuendelea kuzipigia kelele ili kuwa nan chi yenye uhuru kamili wa kujieleza.

“Tumeona mabadiliko makubwa,lakini haimaanishi kwamba changamoto za hapa na pale hazipo hizo ambazo nimezitaja na zingine mtakazojadiliana ni muhimu sana kuzipigia kelele kwamba ili tuweze kuwa na nchi ambayo ina uhuru wa kujieleza uliokamilika ina uhuru wa vyombo vya habari uliokamilika basi tuendelee kufanya maboresho ya sharia zetu zote zinazosimamia sekta hii lakini mwisho wa siku tuwe na mfumo mzuri wa kuruhusu waandishi wa habari kufanya kazi zao kwa uhuru Zaidi,”ameongeza.