February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

WANACHAMA WA THRDC KUANDAA MPANGO WA UTEKELEZAJI WA MPANGO WA TATU WA MAENDELEO YA TAIFA WA MIAKA MITANO

Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umeratibu kikao cha wanachama wa mtandao huo mapema hii leo kilicholenga kufanya mapitio ya maeneo yanayohusu Asasi za Kiraia (AZAKI) katika uandaaji wa mpango wa utekelezaji wa mpango wa tatu wa maendeleo ya taifa wa miaka mitano (FYNDP III).

Akizungumza wakati wa kikao hiko kilichofanyika kwa njia ya mtandao, Mratibu wa Kitaifa THRDC,Wakili Onesmo Olengurumwa amesema kuwa katika maadhimisho ya saba ya siku ya watetezi wa haki za binadamu (Defenders Day) nchini mnamo Julai 2 mwaka huu watajikita katika kuonyesha mchango wa asasi za kiraia katika kutekeleza mpango wa tatu wa maendeleo wa taifa wa miaka mitano.

“Wakati mwingine tunatajwa kuwa hatufanyi yale ambayo yapo katika mpango na tunafanya vitu vya mabeberu ambayo hayana tija kwa taifa,kwahiyo tutumie siku hiyo kuonyesha umuhimu wetu kama AZAKI tuanonekana  hatuna faida lakini kuna mashirika mengi yanayofanya kazi kubwa kwa jamii lakini hazifahamiki,” amesema Wakili Olengurumwa.

Aidha ametoa wito kwa wanachama wa mtandao huo na wadau wa sekta ya AZAKI kutafuta njia mbadala  za kufanya michango yao katika mendeleo ya jamii kutambulika na kujulikana.

“Kama wanachama tutumie fursa hii kuonyesha kwamba sisi tuna mchango mkubwa lakini mchango wetu hautambuliki lakini pia na sisi hatufanyi vitu ambavyo vitafanya michango yetu ikaonekana.Tumeiona tutumie fursa hii kwa ajili ya kuhakikisha kwamba na sisi kama wadau na watetezi wa haki za binadamu tunaonyesha umuhimu wetu katika mikakati ambayo serikali inafanya,”ameongeza.

Olengurumwa ameongeza kuwa mpango huo wa tatu wa maendeleo ya taifa wa miaka mitano una maeneo ambayo yameainishwa yanayogusa sekta ya AZAKI moja kwa moja ikiwemo kupambana na ukatili wa kijinsia,Amani,utulivu,ufuatiliaji na utoaji wa msaada wa kisheria na kutoa wito kwa wanachama hao kuonyesha ushirikiano kwa kujaza dodoso watakalotumiwa na mtandao kuhusu mchango wao kwa jamii.

 Aidha kwa upande wake mtaalamu mwelekezi anaeshirikiana na wanachama wa THRDC kuandaa mpango huo,,Kipobota amewasihi wanachama wa mtandao pamoja na Asasi za kiraia kuona fursa ya kuanzisha mahusiano mazuri na sekta binafsi kama ilivyo kwa serikali kwani katika FYDP III sekta binafsi imepewa fursa kubwa.

“Kwenye ile plan sekta binafsi imepewa fursa kubwa,watu wengi hasa viongozi wetu wanafikiria maendeleo ni lazima waone vitu vinavyoonekana kama majengo n.k,lakini katika AZAKI ina asilimia 50 katika utoaji wa elimu na asilimia 50 katika utoaji wa vifaa tiba,”amesema Kipobota.

Kipobota amesema katika maeneo yote yaliyoainishwa katika mpango huo AZAKI inaweza kuingia katika maeneo hayo yote na kushiriki kwa kutoa huduma kwa maeneo tajwa pia kwa kufanya uchechemuzi pamoja na kuongeza kuelewa kwa jamii kuhusu masuala mbalimbali.

Lengo la kufanyika mkutano huo kati ya THRDC na wanachama wa mtandao huo ni Kuwapitisha na kuwaelewesha wanachama pamoja wadau wa mtandao katika maeneo yanayohusu AZAKI katika kuandaa mpango wa utekelezaji wa mpango wa tatu wa maendeleo wa taifa wa miaka mitano (FYNDP III) pamoja na Kupata utaratibu wa ushiriki wa wanachama na wadau wa Mtandao huo katika kuandaa mpango mkakati huo ambao unatarajiwa kukamilika mwezi Juni mwaka huu.