February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

THRDC KUADHIMISHA KWA MARA YA 7 SIKU YA WATETEZI WA HAKI ZA BINADAMU

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRD) umetangaza kufanya kwa mara ya saba maadhimisho ya siku ya “Watetezi wa Haki za Binadamu” maarufu defenders day.Kwa mujibu wa mratibu wa kitaifa wa mtandao huo Wakili Onesmo Olengurumwa alipozungumza na wandishi wa habari kwenye Ofisi kuu za mtandao huo jijini Dar es Salaam,maadhimisho hayo yamepangwa kufanyika katika ukumbi wa Mlimani City Julai 02 mwaka huu.

“Tangu mwaka 2013, tarehe 28 Aprili kila mwaka, THRDC huwa inaadhimisha Siku ya Watetezi wa Haki za Binadamu kitaifa kama njia ya kusherehekea kuanzishwa kwa mamlaka maalum ya Watetezi wa Haki za Binadamu, ya Umoja wa Mataifa ambayo ndio siku ya Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania”,amesema Lisa Kagaruki,Afisa ushawishi wa wanachama toka mtandao huo.

Katika Kuadhimisha siku hii ya Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania “Defenders Day” Mtandao umekuwa ukishirikiana na wanachama wake, wadau wa Maendeleo, Watetezi wa Haki za Binadamu, pamoja na Mamlaka za kiserikali. Uhusishwaji huu umelenga kuimarisha mahusiano kati ya Watetezi wa Haki za Binadamu na Serikali.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mtandao huo kwa kipindi cha miaka kadhaa iliyopita Maadhimisho ya Siku ya Watetezi wa Haki za Binadamu yamekuwa ya kihudhuriwa na Wageni mbali mbali wakiwemo viongozi wa serikali. Mwaka 2017 Mgeni Rasmi katika Maadhimisho ya 4 ya Watetezi wa Haki za binadamu Tanzania alikuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Ambaye sasa ni Rais) MH. Samia Suluhu Hassan ambaye aliwakilishwa na Mh. Prof. Palamagamba Kabudi (mb) Waziri wa Katiba na Sheria. Mwaka 2018 mgeni Rasmi katika maadhimisho ya 5 ya Watetezi wa Haki za binadamu Tanzania alikuwa ni Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Miko ana Serikali za Mitaa Mh. Suleimani Jaffo ambaye aliwakilishwa na Mh Joseph Kakunda (Mb) aliyekuwa Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Miko na Serikali za Mitaa. Na mwaka 2019 Mgeni Rasmia katika maadhimisho ya 6 ya Watetezi wa Haki za binadamu Tanzania alikuwa Mh. Isaac Kamwelwe Aliyekuwa Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi ambaye aliwakilishwa na Mlembwa Mnaku aliyekuwa kiongozi wa idara ya Tehama katika wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi. Mwaka 2020 hatukufanya maadhmisho kutokana na changamoto za korona.  Maadhimisho haya kwa miaka yote yamekuwa na tija kubwa katika kuboresha mahusiano na serikali na wadau wengine.

“Kutokana na Mlipuko wa ugonjwa wa Corona (COVID-19) nchini Tanzania Mwanzoni mwa mwezi Machi, 2020, Madhimisho ya Siku ya Watetezi wa Haki za Binadamu nchini Tanzania ambayo yalipangwa kufanyika Tarehe 28 April 2020 lakini hayakufanyika kabisa kutokana na sababu kwa sababu ya changangamoto za COVID-19”,amesema mratibu wa Mtandao huo,Wakili Onesmo Olengurumwa.

Kwa sasa Mtandao huo umepanga kufanya Maadhimisho hayo kwa matarajio ya kuwaleta pamoja Watetezi wa Haki za binadamu wapatao 300, Wawakilishi wa Asasi za Kiraia, Viongozi wa Kiserikali na Mahakama, Wadau wa Maendeleo, Mashirika ya Umoja wa Mataifa, Vyombo vya Habari pamoja na wadau mbali mbali wa haki za Binadamu ambao wote watakutana katika ukumbi wa mikutano wa Mlimani City ili kujadili maswala mbali mbali kuhusiana na Mchango wa Asasi za Kiraia katika Maendeleo ya Taifa.

Kauli mbiu ya Mwaka huu ni Kujadili mchango wa Asasi za Kiraia katika Utekelezaji wa Mpango wa tatu wa Maendeleo ya taifa wa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/26) ambapo asasi za kiraia zikiwa kama moja ya sekta muhimu katika maendeleo ya taifa, zimeonyesha nia katika kuchangia maendeleo.

Zaidi ya mashirika 300 wengi wao wakiwa ni Wanachama wa THRDC yametengeneza Mpango wa Asasi za Kiraia wa Utekelezaji wa Mpango wa Taifa Maendeleo wa Taifa (2021 / 22-2025 / 26).  Mpango huu wa utekelezaji utakabidhiwa kwa Waziri Mkuu wakati wa maadhimisho ya 7 Siku ya Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania, kuashiria mwendelezo wa kazi zinazofanywa na watetezi wa haki za binadamu/AZAKI katika kukuza maendeleo ya taifa.

Kulingana na Mpango mkakati wa Maendeleo wa taifa, wanachama wa THRDC wameangazia maeneo kadhaa ambayo wanaweza kufanya kazi pamoja na serikali kama sehemu ya utekelezaji wa mpango huu wa maendeleo. Maeneo haya ni pamoja na Elimu, Sekta ya Afya, Maliasili, Mazingira, Haki za binadamu, Upatikanaji wa haki, Usawa wa kijinsia, Ufuatiliaji na Tathmini, Mabadiliko ya hali ya hewa, Haki za wanawake na Ukatili wa Kijinsia, Maji / Usafi wa mazingira, Msaada wa kisheria, Usalama wa chakula, Ajira, Kilimo, Ufugaji, TEHAMA, Ushawishi wa sera, Utawala wa sheria na Utawala bora.

Maadhimisho ya 7 ya siku ya Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania, yamelenga katika kugusia maeneo muhimu ambayo wanachama wa THRDC, AZAKI, Mashirika ya Haki za Binadamu pamoja na Serikali watafanya kazi kwa pamoja katika kutelekeza Mpango mkakati wa miaka mitano wa maendeleo ya Taifa.

Kabla ya maadhimisho hayo,mtandao huo umeandaa baadhi ya warsha ili kubadilishana uzoefu na kukuza mahusiano, mafunzo ambayo yatatolewa ni pamoja na Mafunzo juu ya namna ya kuzingatia na kuendana na sheria za Ulipaji kodi. THRDC kwa kushirikiana na AcT2 na Shirika la WAJIBU (WAJIBU Institute of Public Accountability), Asasi nyingine za kiraia pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wameandaa mwongozo utakaoziwezesha Asasi za Kiraia kutekeleza sheria, kanuni na Sera zinazosimamia ulipaji kodi nchini Tanzania.

Katika kunogesha maadhimisho ya mwaka huu, Mtandao huo utawatambua na kuwapatia Tuzo Watetezi mbali mbali wa Haki za Binadamu pamoja na Asasi za Kiraia ambazo zina mchango katika maendeleo ya Taifa. waliochangia katika maendeleo ya taifa katika Nyanja ya Ajira, Sekta ya Elimu, Sekta ya Afya, Haki za Binadamu kwa ujumla, Maji na Usafi wa Mazingira.

Watetezi wa Haki za Binadamu/Asasi za Kiraia zitapata fursa ya kuonyesha kazi zao kama mchango wao katika maendeleo ya Taifa, pamoja na majadiliano yatakayolenga kukuza mahusiano kati ya Asasi za Kiraia, Wadau wa Maendeleo, pamoja na Viongozi wa Serikali.