March 23, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

TCRA YAFAFANUA KUHUSU KANUNI ZA UTOAJI MAUDHUI MTANDAONI

Leonard Mapuli/Hilda Ngatunga

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA imebainisha sababu zinazopelekea ulazima wa kutunga kanuni mara kwa mara na pia kutoza fedha za ada na leseni kwa watoaji wa maudhui mtandaoni.

Akizungumza katika mafunzo ya wandishi wa habari mitandaoni toka sehemu mbalimbali za Tanzania yaliyoandaliwa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) na ICNL, Mkuu wa Kitengo cha ufuatiliaji kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania Dkt. Philip Filikunjombe ametaja sababu hizo kuwa ni pamoja na kujenga uwajikaji,kuifanya jamii kuaminika pamoja na kuleta ushindani.

Hata hivyo Filikunjombe amekiri kuwepo kwa nguvu kubwa ya mitandao ya kijamii na hata Uandishi habari “Watu” unaozidi kushika kasi kote duniani na kwamba mabadiliko na kutazamwa upya kwa baadhi ya kanuni ni muhimu ili kulinda uhuru na haki ya utoaji na upokeaji Habari.

“Mabadiliko ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ina uwezo mkubwa wa kubomoa ama kujenga misingi ya utu pamoja masuala ya haki za binadamu”,amesema Filikunjombe.

Kwa muda mrefu wadau wa habari mitandaoni nchini Tanzania wamelalama kuhusu kanuni mbalimbali zenye kila dalili ya kuuminya uhuru wa habari na kutaka kanuni hizo kufanywa rafiki na si adui ambapo mamlaka hiyo imekiri kuanza kuzifanyia kazi.
“Tunafanya mapitio ya kanuni hizi ninyi kama wadau napendekeza leteni maoni yenu ikiwezekana andika andiko kuwa unapendekeza hili na hili halafu tutumie sisi tutakupa mrejesho wa mapendekezo yako,” amesema Filikunjombe

Mafunzo haya ya siku tatu yanayofanyika mkoani Morogogo yanahusisha wandishi wa habari 65 kutoka vyombo mbalimbali vya habari vya Tanzania vinavyochapisha maudhui yake kwa njia ya mtandao.