February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

TAASISI ZA KUTETEA HAKI ZA BINADAMU ZAUGANA KUISHAURI SERIKALI NAMNA YA KUTATUA MGOGORO NGORONGORO

Na: Anthony Rwekaza

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu,(THRDC), Mtandao wa Mashirika ya Wafugaji Tanzania (PINGOs Forum), Jukwaa la Ardhi Tanzania, Umoja wa Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) pamoja na wadau wengine kwa pamoja wameishauri Serikali kupitia Waziri Mkuu kuwashirikisha wadau wengine ikiwemo watetezi wa haki za binadamu katika mpago utakaondaliwa na Wizara ya Maliasili juu ya kuwaelimisha Wabunge juu ya sakata la mgogoro unaoendelea Ngorongoro.

Taasisi hizo zimetoa kauli hiyo leo Februari 12, 2022 mbele ya vyombo vya habari kwenye ofisi za THRDC, akizungumza Mratibu wa THRDC, Wakili Onesmo Olengurumwa amesema wanamuomba Waziri Mkuu kutoa nafasi kwa wadau huri ikiwemo wananchi wa Ngorongoro, Watetezi wa Haki za Binadamu pamoja na wadau wengine katika hatua ya kushiriki kutoa elimu kwa Wabunge kuhusu uhalisia wa hali ilivyo Ngorongoro

“Tunamwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu kuwapa nafasi wadau huru kama vile wananchi wa Ngorongoro, Watetezi wa Haki za Binadamu na wadau wengine kushiriki katika kutoa elimu kwa wabunge kuhusu hali halisi ya Wilaya ya Ngorongoro.” amesema Mratibu wa THRDC, Onesmo Olengurumwa

Olengurumwa amesema hali hiyo ni kutokana na ukweli kwamba Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, TAWA na Wizara ya Maliasili na Utalii ni miongoni mwa wanaodaiwa kutuhumiwa na Wananchi wa Wilayani Ngorongoro kuwa wapo sehemu ya mpango unaoendelea bila maafikiano.

Ameongeza kuwa wanaisihi serikali kutambua kwamba umaskini uliopo Wilaya ya Ngorongoro na ukosefu wa
huduma za jamii limesababishwa na mamlaka kushindwa kusimamia malengo ya uanzishwaji wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCA).

Mratibu huyo ambaye kwa mara kadhaa amekuwa akiishauri Serikali namna ya kushughulika mgogoro huo kuunda tume huru itakayowahusisha wafugaji wenyeji wa Ngorongoro, wataalamu
wa uhifadhi, watetezi wa haki za binadamu, wadau wa utalii, wataalamu wa mifugo ili kufanya utafiti jumuishi kuhusu hoja zinazobishaniwa, ambapo amedai kamati hiyo inaweza kutoa mapendekezo yatakayozingatia ulinzi wa hifadhi pamoja na haki za jamii ya Ngorongoro.

Pia Mkurugenzi wa Mtandao wa Mashirika ya Wafugaji Tanzania (PINGOs Forum), Edward Porokwa amesema yameibuka malalamiko kutoka kwa Wananchi wa Ngorongoro kuhusu baadhi ya vyombo vya habari na kupotosha umma kwa taarifa za uongo na zenye kutweza utu wa Wananchi hao

“Siku za hivi karibuni yameibuka malalamiko kutoka kwa wananchi wa Ngorongoro kuhusu baadhi ya vyombo vya habari na watu mbalimbali wanaopotosha na kutoa taarifa za uongo na zenye kutweza utu wa wananchi washio eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.” amesema Mkurugenzi wa PINGOs Forum, Edward Porokwa

Hata hivyo amesema madai hayo ambao ameyaita potofu yameendelea kutolewa kwenye baadhi ya vyombo mbalimbali vya habari, ambapo amedai taarifa hizo zimeleta taharuki kubwa kwa jamii za kifugaji
na hali ambayo amedai imepunguza ushiriki wao katika kazi zao za kawaida za kujipatia vipato kutokana na kile alichodai kuwa jamii hiyo inajihisi kutengwa na kunyanyapaliwa kutokana na wao kuamua kuishi katika utamaduni wa mazingira asilia.

Porokwa ambaye nae amekuwa akitoa maoni juu ya mgogoro kufuatia wananchi wengi kuwa wafugaji, amedai Wananchi wamelalamikia vyombo hivi vya Habari kwa kuendelea kuwadhalilisha katika
taarifa zao pengine kwa lengo la kutaka kushawishi taasisi za umma kuwa wale wananchi ni wakosaji na wanapaswa kuondolewa katika makazi yao. Amedai pia kusikitishwa madai ya taarifa za wandishi wengine ambao wamekuwa wakitafuta nafasi ya kuwasikiliza na wananchi kusumbuliwa wakati wanafanya kazi zao huko kwenye maeneo ya Ngorongoro.

Aidha Wakili Joseph Chiombola kutoka HAKI ARDHI, amesema hoja ya ” Maslahi ya Taifa” inayodaiwa kutumika imekuwa ikitumiwa vibaya kama sababu ya kuhalalisha mchakato wa kuwaondoa Wananchi wanaoishi ndani ya hifadhi hiyo ya Ngorongoro, amedai Wananchi hao wa jamii ya kimasai licha ya mchango wao katika kulinda hifadhi hiyo pamoja na rasiliamali lakini bado wameendelea kuonekana mchango wao hautambuliki

“Hoja ya ‘maslahi ya Taifa’ imekua ikitumika vibaya kwa nia ya kuhalalisha kuhamisha
wafugaji. Licha ya Wananchi
wa jamii hii ya kimasai katika kulinda hifadhi hii kwa miaka mingi pia imeshindwa
kudhaminiwa na kufanya waonekane hawana mchango wowote katika kulinda rasilimali
asili za Taifa.” amesema Wakili wa HAKI ARDHI, Joseph Chiombola

Lakini ameongeza kuwa hata hoja nyingine zinazotolewa kama wingi wa mifugo katika hifadhi hiyo pamoja madai ya jamii nyuma yao kuwepo na mashinikizo ya watu kuwa sio madai ya kweli kwa kuwa hakuna tafiti zozote za kuthibitisha ukweli wowote, hisipokuwa amedai wanaosema hivyo hawajui uhalisia uliopo kwenye jamii ya Ngorongoro.

Kufuatia uwepo wa mjadala Bungeni juu ya sakata la Ngorongoro ikiwemo kauli baadhi ya Wabunge kutaka Serikali iwaondoe Wananchi kwa nguvu endapo watashindwa kuama kwa hiari licha ya Wabunge wengine akiwemo Mbunge wa Jimbo la Ngorongoro kutaka mamlaka kujadiliana na wananchi juu ya mgogoro huo, lakini kufuatia hali hiyo Mratibu wa THRDC, Onesmo Olengurumwa amelitaka Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kusimamia mijadala hiyo pindi Wabunge wanapojadili kuhusu hali unayoendelea Ngorongoro, hususani kukemea kauli zinazotweza utu wa Wananchi wa Ngorongoro ambao wamekuwa wakilinda rasiliamali zinazopatikana Wilayani Ngorongoro.

“Tunaliomba Bunge letu lisimamia mijadala ya wabunge kuhusu Ngorongoro kwa usawa
na kukemea lugha zinazotweza utu wananchi wa Ngorongoro waliojitoa sadaka kwa
miaka mingi kulinda rasilimali zile Wilayani Ngorongoro.” amesema Mratibu wa THRDC, Onesmo Olengurumwa

Olengurumwa amesisitiza kuwa itambulike kuwa wananchi wa Ngorongoro hawana kosa lolote kwani kuongezeka kwa idadi ya binadamu na mifugo sio kosa kisheria. Ambapo ameshauri Sheria inayounda Mamlaka ya Uhifadhi ya Ngorongoro kupitiwa upya na kuboresha usisimamizi na ulinzi wa haki za wananchi pamoja na kuhakikisha hifadhi inalindwa na kuendelezwa.

Ameshauri pia mamlaka kuthibiti shughuli zingine za kibinadamu zinazosababishwa na uongezeko la shughuli za kitalii katika Hifadhi ya Ngorongoro, akitolea mfano mamlaka kuthibiti ujenzi wa hoteli na wingi wa magari, huku ameongeza kuwa ni muhimu kusitisha nia ya kutaka kuchukua ardhi ya vijini 14 vya Loliondo zenye kilomita za mraba 1500 na badala yake kuwe na makubaliano baina ya serikali na wananchi juu ya kuyalinda
maeneo hayo kwa shuguli za mifugo na wanyama pori.

Taasisi ambazo zimeshiriki kwa pamoja kutoa ushauri huo ni, TANZANIA HUMAN RIGHT DEFENDERS COALITION (THRDC), ALPHA AND OMEGA RECONCILIATION AND PEACE BUILDING (AREPEB), CIVIC AND LEGAL AID ORGANIZATION (CILAO), FOUNDATION FOR COMMUNITY INVOLVEMENT (FCI-TANZANIA), GREEN COMMUNITY INITIATIVES, HAKI ARDHI HAKIMADINI, LEGAL AND HUMAN RIGHTS CENTRE, MEDIA AID FOR INDIGENOUS PASTORALIST COMMUNITY, NGURUKA DEVELOPMENT AGENCY (NDA).

Taasisi nyingine ni PASTORALIST WOMEN COUNCIL (PWC), PINGOs Forum, RESOURCES ADVOCACY INITIATIVE, RUJEWA INTEGRATED EFFORTS TO FIGHT POVERTY (RIEFP),SAKALE DEVELOPMENT FOUNDATION (SADEF), TALA, TANZANIA MEDIA WOMEN ASSOCIATION (TAMWA), UCRT, WOMEN AND CHILDREN WELFARE SUPPORT (WOCWELS), WOMEN AND CHILDREN’S LEGAL AID ORGANISATION.

Itakumbukuwa kumekuwepo na hali ya sintofahamu kufuatia Serikali kutaka kuondoa baadhi ya kaya zilizopo ndani ya hifadhi ya Ngorongoro ili kupunguza idadi ya watu kama inavyodaiwa na mamlaka zinaratibu mchakato huo. Baada ya viongozi mbalimbali wa Serikali kutoa kauli za kuhusu mchakato huo jamii hiyo imekuwa ikitoa baadhi ya malalamiko juu ya kudai kutoshirikishwa juu ya hatua zinazotakiwa kuchukuliwa.

Kufuatia hali hiyo jambo ilo limemuibua Waziri Mkuu ambapo ameelezea mbaele ya Bunge juu ya mgogoro huo kuwa tayari ameshapokea maagizo kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan akimtaka kufuatilia mgogoro huo ambapo alieleza wazi kuwa ameshaanza kuyafanyia kazi maagizo hayo na tayari watendaji mbalimbali wameshaanza mazungumzo na wananchi wa Ngorongoro na alidai kuwa amemuelekeza Waziri wa Maliasili na Utalii kufanya semina maalumu na Wabunge ili kuwaelimisha zaidi juu ya uhalisia unaoendelea Ngorongoro.