February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

SIMBACHAWENE: SERIKALI INAENDELEA KUBORESHA MIFUMO YA UTOAJI HAKI

Waziri wa Katiba na Sheria, George Simbachawene, amesema Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, imefanikiwa kuboresha mfumo wa utoaji haki, katika kipindi cha mwaka mmoja.

Simbachawene amesema hayo leo Ijumaa, jijini Dar es Salaam, akizungumzia mafanikio ya uongozi wa Rais Samia, kuanzia Machi 2021 hadi Februari mwaka huu.

Waziri huyo wa Katiba na Sheria, amesema Serikali hiyo imeboresha mfumo wa utoaji haki kwa kutekeleza shughuli mbalimbali, ikiwemo kufanya marekebisho ya Sheria za Mahakama za Mahakimu, sura ya 11, yanayowezesha mawakili kufanya kazi kwenye mahakama za mwanzo.

Pia, amesema Serikali ya Awamu ya Sita imerekebisha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, ambapo kwa sasa unatoa sharti la upelelezi kukamilika kabla mtuhumiwa kufikishwa mahakamani na au mtuhumiwa akiachwa huru asikamatwe endapo upelelezi wa tuhuma zinazomkabili haujakamilika.

“Aidha, jitihada zimeendelea kuchukuliwa ili kurahisishia upatikanaji haki na utoaji huduma. Jitiahda hizo ni pamoja na kupunguza mrundikano wa mahabusu gerezani kwa kubadilisha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai iliyotoa masharti ya kukamilisha upelelezi kwanza kabla ya mtuhumiwa kufikishwa mahakamani,” amesema Simbachawene.

Simbachawene amesema, ndani ya kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wa Rais Samia, uwezo wa usikilizwaji mashauri mahakamani umeongezeka kwa asilimia saba, kutoka asilimia 92 iliyokuwepo Machi 2021 hadi kufikia asilimia 99.

Amesema, kuanzia Machi 2021 hadi Februari 2022, mashauri yalifunguliwa 181,768, ambapo 180,162 yalisikilizwa.

Pia, amesema Serikali hiyo imeendelea kuimarisha mfumo wa utatuzi wa migogoro nje ya mahakama kwa kutumia njia ya upatanishi, usuluhishi na maridhiano, kwa kusajili wasuluhishi 192, wapatanishi 106, waendesha majadiliano 37 na waendesha maridhiano 23.