March 23, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

SHAMBULIO UWANJA WA NDEGE WA KABUL RAIS WA MAREKANI JOE BIDEN ATANGAZA KULIPIZA KISASI

Na Loveness Muhagazi

Makao makuu ya Jeshi la Marekani Pentagon yameripoti kutokea kwa Milipuko miwili siku Alhamisi, Agosti 26 katika shambulio “tata” karibu na uwanja wa ndege wa Kabul. Tukio hilo limesababisha vifo vya watu sita, wakiwemo Wamarekani na watoto, na zaidi ya kumi na tano wamejeruhiwa taarifa za awali zimeripoti kuwa Afisa wa Marekani ameliambia Shirika la habari la Reuters kuwa mlipuko huo ulisababishwa na mtu aliyejitoa muhanga.

Kufuatia mlipuko huo Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaani vikali mashambulio ya kigaidi yaliyotokea nje ya uwanja wa ndege wa Kabul nchini Afghanistan. Ameeleza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesikitishwa sana na kuuliwa bila ya hatia raia wa kawaida katika mashambulio hayo ya Kabul, wakiwemo wanawake, watoto na vijana.

“Tunatumai serikali jumuisha itaundwa huko Kabul haraka iwezekanavyo, ili mamlaka husika zichukue jukumu la kulinda maisha na mali za Waafghani”. Msemaji wa wizara  

Wakati huohuo, kundi la kigaidi la ISIS limetangaza kuhusika na hujuma hiyo ambayo ni ya kwanza kutokea mjini Kabul tangu rais Ashraf Ghani aitoroke nchi; na mji mkuu huo wa Afghanistan kudhibitiwa na kundi la Taliban mnamo tarehe 15 Agosti.

Taarifa ya ISIS imeeleza kuwa Mwanachama wa Daesh aliyekuwa amejifunga mabomu alifanikiwa kupenya na kuufikia ummati mkubwa wa wakalimani na washiriki wa jeshi la Marekani katika kambi ya Baran karibu na Uwanja wa Ndege wa Kabul na kujiripua. Kufuatia tukio hilo  Rais wa Marekani Joe Biden amesema kamwe Marekani haitosahau wala kusamehe mashambulio hayo, na kwamba italipiza kisasi.

Hata hivyo Rais wa Marekani Joe Biden katika hotuba yake kwa taifa, amesema kuwa zoezi la kuondoa raia wakigeni kutoka Afghanistan itaendelea licha ya shambulio lililogharimu maisha ya watu kadhaa, hususan wanajeshi 13 wa Marekani karibu na uwanja wa ndege wa Kabul, nchini Afghanistan.

“Hatutazuiliwa na magaidi. Hatutawaacha wazuie operesheni yetu. Tutaendelea na zoezi hilo”, Rais Joe Biden