Na Antony Benedicto
Shahidi wa 10 wa Jamhuri ambaye ni Afsa wa Jeshi la Polisi, Ispecta Innocent Ndow anayefanya kazi kwenye kitengo cha uhalifu wa makosa ya kimtandao (Cyber Crime) akishughulika uchunguzi na uchambuzi wa taarifa, ameanza kutoa ushahidi wake leo Januari 17, 2022 kwenye Mahakama Kuu divisheni ya makosa ya Rushwa na Uhujumu katika Kesi namba 16/2021 inayomkabili Freeman Mbowe na wenzake watatu.
Amesema alipokea barua kutoka Ofisi ya DCI ikiwa na viambatanisho nane(nyaraka zenye namba za Mawasiliano na taarifa za miamala) ambavyo alitakiwa kuvifanyia uchunguzi na uchambuzi kupita mahabala ya uchunguzi wa kisayansi ‘software’, lakini ameiambia Mahakama kuwa kati ya viambatanisho hivyo alibaini nyaraka nne ndizo zilionekana kuwa na jinai.
Lakini katika hali ya sintofahamu wakati shahidi huyo akiendelea kutoa ushahidi Mahakamani, katika hatua ya kutambua vielelezo ambavyo ni nyaraka ya miamala kutoka kampuni ya Mawasiliano ya Tigo ghafla ameieleza Mahakama kuwa amepata changamoto ya kiafya (kwamba kichwa kinauma hawezi kutoa sauti), ameeleza kuwa kufuatia hali hiyo hawezi kuwa kwenye nafasi nzuri ya kuendelea kutoa ushahidi wake mbele ya Mahakama, baada ya kushauriana kwa pamoja Mawakili wa Jamhuri wameomba kesi hiyo kuahirishwa ili shahidi apatiwe matibabu.
Mahakama kupitia Jaji Joachim Tiganga ameridhia ombi hilo, ambapo ameahirisha kesi hiyo mpaka kesho Januari 18, 2022 saa 3:00 asubuhi.
Habari Zaidi
KIKOSI KAZI KITASAIDIA KULETA MARIDHIANO – JK
NI MIAKA MITANO SASA TOKEA LISSU ASHAMBULIWE
SHAHIDI JAMHURI AELEZA KINA MBOWE WALIVYOSUKA MPANGO WA KUTENDA UGAIDI