February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

SHAHIDI JAMHURI AELEZA KINA MBOWE WALIVYOSUKA MPANGO WA KUTENDA UGAIDI

Freeman Mbowe (Wa kwanza Kulia)akiwa Mahakama Kuu Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi-21/01/2022

Na: Anthony Rwekaza

Washtakiwa wanaokabiliwa na mashtaka ya ugaidi kwenye Kesi namba 16/2021 akiwemo Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe leo Januari 21, 2022 wamefikishwa kwenye Mahakama Kuu divisheni ya makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi ikiwa kesi hiyo inaendelea kusikilizwa mfululizo.

Shahidi wa 11 wa Jamhuri H4347 Sajenti Goodluck ambaye ni askari Polisi ameanza kutoa ushahidi wake akiongozwa na Wakili wa Jamhuri, ameiambia Mahakama kuwa Agosti 2020 akiwa kwenye maeneo yake ya kazi pamoja na askari wengine waliitwa ofisni na na aliyekuwa RCO wa Arusha (kwa sasa ni RPC Mkoa wa Kipolisi Kinondoni), ACP Ramadhani Kingai na kuwa aliwaeleza juu ya uwepo wa kikundi kinachopanga kutekeleza ugaidi.

Ameiambia Mahakama kuwa RCO Kingai aliwaeleza kuwa alipata taarifa kuwa mpango huo ulilenga kuwadhuru viongozi wa Serikali akiwemo aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai Leng’ai Ole Sabaya, kulipua vituo vya mafuta Nchini, kukata miti ili kuzuia barabara zisipitike, kuhamasisha maandamano yasiyo na kikomo Nchi nzima kwa lengo la kuleta taharuki kwa wananchi ili Nchi isitawalike.

Askofu Emmaus Mwamakula (Katikati) na Profesa Azaveli Lwaitama (Kulia) wakiwa Mahakamani kufuatilia kesi ya Mbowe-21/01/2022.

Shahidi huyo ameiambia Mahakama kuwa kwa taarifa walizopewa na RCO Kingai ni kuwa kiongozi wa kundi hilo alikuwa ni Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe, ameendelea kusema kuwa baada ya kupewa maelekezo walianza safari ya kuelekea Moshi ambapo amedai kuwa siku hiyo walifika na kuanza kuzunguka maeneo mbalimbali kuwatafuta watuhumiwa lakini mpaka kufika saa tano tano usiku walikuwa hawajafanikiwa na hivyo Kingai aliwaambia wakapumzike ili kuendelea na jukumu hile siku inayofuata.

Amesema siku iliyofuata Agosti 5, 2020 walifanikiwa kuwakamata watuhumiwa wawili ambao ni Adam Kasekwa, Muhammad Ling’wenya kwenye eneo la Rau madukani Moshi, ameiambia Mahakama kuwa baada ya kuwakamata walianza mchakato wa kuwapekua , ambapo amesema walianza kumpekua Adam Kasekwa ambaye walimkuta na bastola-K5340 pamoja na risasi tatu pia kipande cha karatasi kilichokuwa na kete zilizodhaniwa kuwa ni dawa za kulevya.

Katika kesi hiyo viongozi mbalimbali wa Chadema wakiwemo wajumbe wa halmashauri Kuu, Wanachama pamoja na wafuasi wameendelea kuwa sehemu kubwa ya watu wanaofuatilia mwenendo wa kesi hiyo mara kwa mara inapotajwa kusikilizwa.