March 23, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

SERIKALI YAZIANGUKIA NGO’S UHABA MAAFISA USTAWI WA JAMII

Serikali ya Tanzania, imetoa wito kwa wadau wa maendeleo, ikiwemo Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGO’s), kutoa ajira za muda kwa maafisa ustawi wa jamii, ili kupunguza changamoto ya upungufu wao katika ngazi ya kata.
Wito huo umetolewa leo Jumatatu na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima, akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha wa 2022/23.
“Nitoe rai kwa wadau wa maendeleo yakiwemo mashirika yasiyo ya kiserikali, kutoa ajira za muda kwa maafisa maendeleo ya jamii hususan katika ngazi ya kata, ambapo kuna upungufu mkubwa ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa afua za kutatua changamoto zinazoikabili jamii yetu,” amesema Dk. Gwajima.
Aidha, Dk. Gwajima amewaomba maafisa ustawi wa jamii waliostaafu, watoe mchango wao katika jamii.
Dk. Gwajima amesema wizara yake ina uhaba wa maafisa maendeleo ya jamii zaidi ya 2,000 ikiwa ni sawa na upungufu wa asilimia 43 kati ya 5,296 wanaohitajika.
“Pamoja na juhudi zote za ushirikishaji jamii zinazofanywa na maafisa maendeleo ya jamii nchini, bado tunakabiliana na changamoto ya uhaba wa maafisa hao. Jumla ya maafisa 5,296 wanahitajika nchini, hadi Aprili 2022, maaafisa waliopo katika ngazi ya mkoa, halmashauri na kata ni 3,014 ambapo upungufu ni 2,282,” amesema Dk. Gwajima.
Dk. Gwajima amesema wizara yake itaendelea kuwasiliana na Wizara ya Ofisi ya Rais-TAMISEMI, pamoja na Wizara ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, ili kutafuta namna ya kutatua changamoto hiyo.
Kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa 2022/23 , Dk. Gwajima ameliomba Bunge lipitishe bajeti ya Sh. 43.40, ambapo Sh. 14.14 bilioni, kwa ajili ya mishahara ya watumishi, Sh. 18.16 Bil, kwa ajili ya matumizi mengine na Sh. 11.92 kwa ajili ya miradi ya maendeleo.