February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

SERIKALI YATAKA MIGOGORO KANISANI, MISIKITINI IKOMESHWE

SERIKALI ya Tanzania, imewataka viongozi wa dini, wakomeshe migogoro ya matumizi mabaya ya madaraka na kugombania mali za nyumba za ibada, kwani hazileti afya kwa amani ya nchi.

Wito huo ulitolewa jana Jumatano na Makamu wa Rais, Dk. Phillip Mpango, kwenye hafla ya futari iliyoandaliwa na Kamati ya Amani ya Mkoa wa Dar es Salaam.

Dk. Mpango amesema migogoro hiyo inakwenda kinyume na katiba za madehebu yao na maandiko matakatifu.

“Viongozi wangu wa dini mtafute kwa bidii na kuomba amani itawale katika nyumba za ibada, Serikali na bila shaka wengi wenu tunakerwa na kuumizwa sana na migogoro ndani ya makanisa na misiti, ikiwemo kugombea uongozi na matumizi mabaya ya madaraka na mali za kanisa au msikiti,” amesema Dk. Mpango.

Aidha, Dk. Mpango ameshauri kamati za amani ziundwe kwa ajili ya kutatua migogoro inayoibuka katika nyumba za ibada.

“Natamani sana kila sehemu tuwe na kamati ya amani ya viongozi wa dini, lakini natamani kila dehebu liwe na kamati ya amani ambayo itafanya kazi usiku na mchana, kulea na kutafuta amani ndani ya madehebu yetu mbalimbali ya dini,” amesema Dk. Mpango.