March 23, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

SERIKALI YATAJA MATOKEO TATHIMINI MWENENDO BEI ZA BIDHAA 

SERIKALI ya Tanzania, imesema tathimini ya mwenendo wa bei za bidhaa nchini, imeonesha gharama za  bidhaa zinazozalishwa nchini ni himilivu, wakati zinazotoka nje ya nchi zikiwa za viwango visivyohimilika.

Matokeo ya tathimini hiyo yametajwa leo Jumatatu, jijini Dar es Salaam na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Ashatu Kijaji.

Dk. Kijaji amesema, bei ya bidhaa zinazoingizwa nchini kutoka nje ya nchi, hasa mafuta ya kula, petroli na dizeli, hazihimiliki kutokana na kupanda kufuatia athari za vita kati ya Urusi na Ukraine.

“Matokeo ya tathimini ya mwenendo wa bei za bidhaa mbalimbali ambazo tumepitia, imeonesha bei ya bidhaa zinazozalishwa nchini zina uhimilivu mkubwa, japo zipo bidhaa chache sana kama saruji na nondo, bei zake zimepanda kwa viwango visivyohimilika,” amesema Dk. Kijaji.

Kufuatia changamoto hiyo, Dk. Kijaji amesema Serikali inaendelea kufanya mazungumzo na wadau wanaojihusisha na biashara ya bidhaa hizo, ili kuangalia namna ya kudhibiti mfumuko wake wa bei.

“Kuhusu bei ya saruji na sukari tunaendelea na mazungumzo kati yetu Serikali na wadau, katika sekta hii na tathimini inaendelea kufanyika kwani kuna haja,” amesema Dk. Kijaji.

Pia, Dk. Kijaji amesema Serikali imeanzisha mfumo wa ufuatiliaji bei za bidhaa, ambao utawawezesha wananchi kutoa taarifa pindi watakapoona mabadiliko ya bei ya bidhaa sokoni, kwa ajili ya kuchukua hatua.

“Serikali imeanzisha mfumo wa ufuatiliaji bei za bidhaa mbalimbali, kila siku kutakuwa na call center itakayotumika  na wananchi, watapiga simu wanapoona mabadiliko ya bei ya bidhaa sokoni, ili tuweze kuchukua hatua haraka kabla ya taarifa za maafisa biashara wetu,” amesema Dk. Kijaji.

Aidha, Dk. Kijaji amewaagiza maafisa biashara wa mikoa yote nchini, kufuatilia mwenendo wa bei za bidhaa katika maeneo yao, kisha kutoa taarifa kwa makatibu wao, ili hatua za haraka zichukuliwe itakapobainika kuna mfumuko wa bei.

Katika hatua nyingine, Dk.Kijaji amesema Serikali imeziagiza taasisi zake zilizopewa dhamana ya kusimamia mwenendo wa bei za bidhaa, ziendelee kutekeleza majukumu yake bila kuathiri pande zote mbili.

“Mamlaka na taasisi za Serikali zilizopewa dhamana ya kusimamia mwenendo wa bei ya bidhaa, ziendelee kutekeleza majukumu yao bila kuathiri pande zote mbili, ili kudhibiti upandaji bei holela, hasa zinazozalishwa ndani ya Taifa letu. Hatuna sababu bidhaa hizo kuona zinapanda bei,” amesema Dk. Kijaji.

Akitaja mikakati ya Serikali katika kukabiliana na mfumo wa bei, Dk. Kijaji amesema wafanyabiashara wanaoingiza bidhaa zinazotoka nje ya nchi, ikiwemo mafuta, watapewa motisha hususani kwa  kuwapunguza kodi.