December 4, 2022

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

SERIKALI YASHAURIWA KUUNDA TUME KUDHIBITI MAGONJWA YASIYO YA KUAMBUKIZA

Mbunge  wa Mtambwe, Khalifa Mohamed Issa, ameishauri Serikali ianzishe tume maalumu ya kushughulikia magonjwa yasiyoambukiza, ili kuyadhibiti yasiendelee kuongezeka.

Issa ametoa ushauri huo leo Jumatatu, katika kipindi cha maswali na majibu, bungeni jijini Dodoma.

“Magonjwa haya yasiyokuwa ya kuambukiza yanaongezeka kila uchao, mfano kuanzia 2016 tulikuwa na wagonjwa 4,000,000, kufika 2020 wagonjwa wamekuwa 4,800,000 na inagharimu asilimia 20 ya bajeti ya Wizara ya Afya na kusababisha vifo, Serikali hamuoni ni wakati umefika magonjwa haya kuyaundia tume maalumu ya kuyashughulikia ikiwemo saratani,” amesema Issa.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel amesema Serikali itafanyia kazi ushauri wake.

Hata hivyo, Mollel amesema ni bora Serikali ikatumia fedha katika kuyakinga moja kwa moja magonjwa hayo badala ya kuanzisha tume maana fedha zitaishia kwenye masuala ya utawala.

“Tutafanyia upembuzi yakinifu wazo lake, lakini kikubwa ni kuongeza nguvu zaidi kwenye kuelimisha hasa magonjwa yasiyoambukiza, namna mtindo wa maisha na mambo mengine, ili kupunguza watu wanaopata matatizo hayo, lakini kuongeza bajeti kwenye utoaji elimu ili iwafikie wengi,” amesema Dk. Mollel na kuongeza:

“Maana yake ukianzisha taasisi wakati mwingine tunarudi kulekule, fedha nyingi zinaishia kwenye masuala ya utawala badala ya kumfikia mgonjwa mhusika, nafikiri muhimu kuongeza nguvu kwenye eneo hilo.”