February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

SERIKALI KUTOA RUZUKU YA PEMBEJEO KWA WAKULIMA

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amekubali ombi la Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, la kutoa fedha kwa ajili ya ruzuku ya pembejeo kwa wakulima, ili waweze kukabiliana na changamoto ya mfumuko wa bei ya bidhaa hiyo.

Akizungumza katika uzinduzi wa ugawaji vitendea kazi kwa maafisa ugani kilimo, leo Jumatatu, jijini Dodoma, Rais Samia amesema atazungumza na uongozi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ili kuangalia namna ya kupata fedha hizo.

“Tutakaa na Gavana wa BoT tuangalie mgawo wa kwenye ile fedha Sh. 1 trilioni, aliyotoa kukuza uchumi, kwa kuanzia sekta ya kilimo.  Nikuahidi fedha kwa ajili ya kuanzisha mifuko inapatikana,” amesema Rais Samia.

Wakati huo huo, Rais Samia ameiagiza wizara hiyo ianzishe mfuko wa pembejeo na  wa maendeleo ya kilimo, kwa ajili ya kukabiliana na changamoto ya mfumuko wa bei za pembejeo kwa wakulima.

“Nitoe agizo muanzishe mifuko ya mzunguko, ambao mmoja utakuwa wa pembejeo na wa pili wa maendeleo ya kilimo. Madhumuni tunapoenda kupata shida ya pembejeo zinapopanda bei, mfuko ushushe presha ya bei kwa wakulima. Wakulima wetu wasiende kupata kadhia ya kulipa pesa nyingi kulipa pembejeo,” amesema Rais Samia.

Mbali na kuahidi kutoa fedha hizo, Rais Samia ametoa wito kwa wabunge, kupaza sauti zao bungeni kuhusu sekta ya kilimo, ili ifanye vizuri kama zinavyofanya sekta nyingine.

“Wabunge mko hapa, mmesikia mipango ya Serikali imeongeza bajeti. Nawaombeni sana tubebeni sekta ya kilimo, sekta nyingine zinakwenda vizuri. Kwenyw kilimo pitisheni kwa kauli moja tuweze kutekeleza,” amesema Rais Samia.

Rais Samia amewaagiza wataalamu wa masuala ya kilimo, watoke katika ofisi zao kwenda kwa wakulima.

“Naagiza tafiti zote zitoke maabara ziende kwa wakulima. Tumefanya tafiti nyingi sana tunaziona kwenye maonesho sasa zitoke ziende kwa wakulima,” amesema Rais Samia.