February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

SERIKALI KULINDA HAKI ZA BINADAMU KWA WANANGORONGORO, YASISITIZA KUWA HAIALAZIMISHI MTU KUHAMA

Na: Anthony Rwekaza

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro amesema Serikali itahakikisha inalinda haki za Binadamu kwa Wananchi wa Ngorongoro wakati inaporatibu mpango wa kuhama kwa hiari licha ya kusisitiza kuwa hakuna anayelazimishwa kuhama.

Akizungumzia Sakata hilo Waziri wa Maliasili na Utalii, amesema amesema Serikali ipo ili kuhakikisha haki za binadamu zinalindwa  na kutaka watu wengine kuzingatia haki hizo kwa  kutowalazimisha wananchi hao kubakia.

“Sisi kama Serikali tupo hapo kuhakikisha haki za Binadamu hazikiukwi, Serikali haitakiuka haki za Binadamu na mtu mwingine yeyote asikiuke haki za Binadamu, wakae au waondoke kwa hiari.” Amesema Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbalo

Pia Waziri huyo amesema Serikali haimlazimishi mtu yoyote kuhama eneo la ndani ya hifadhi ya Ngorongoro, ametaka pia asitokee mtu yeyote kuwafanya wananchi wanaotaka kuhama kutokuhama, amesisitiza kuwa pia kufanya hivyo ni ukiukwaji wa haki za binadamu, amesema kuwa watu hao watahama kwa kuzingatia matakwa ya kikatiba na kisheria.

“Hawalazimishwi kuama na pia wasilazimishwe kubaki kwa sababu ni uamuzi wao anayetaka kuhama ahame, asitokee mtu yeyote anasema kwamba hakuna mtu kutoka hapo, na hiyo kumlazimisha mtu asiame nayo ni ukiukwaji wa haki za binadamu, watahama kwa hiari kwa mujibu wa Katiba yetu kwa mujibu wa sheria zilizopo na kwa kuheshimu haki za Binadamu, kwa sababu hao ni binadamu kama binadamu wengine.”- Waziri wa Maliasili na Utalii,Dkt. Damas Ndumbalo

Aidha Dkt. Ndumbaro amesema kinachoendelea kwa sasa kwenye hifadhi hiyo ni utaratibu wa watu kujiandikisha kwa hiari ili waweze kuhama na kwenda kuishi maeneo mbalimbali ikiwemo Wilayani Handeni, ambapo amesema Serikali imeshaanza kujenga nyumba kwa ajili ya wananchi watakojitokeza kwa hiari ili waweze kuwa wanaishi kwenye nyumba hizo.

“Kinachoendelea kwa sasa(Ngorogoro) ni watu hao kujiandikisha kwa hiari kabisa ili waweze kuhama na kwenda kuishi maeneo mbalimbali ikiwemo Handeni, ambapo Serikali inyoongozwa na Rais Mama Samia imeamua kujenga nyumba ili wale wote watakaoamua kuhama kwa hiari yao pasipo shuruti yoyote waweze kwenda kukaa pale”- Waziri wa Maliasili na Utalii,Dkt. Dismas Ndumbalo

Hata hivyo amesema sasa changamoto iliyopo ni kuwa eneo hilo ardhi yake haiogezeki lakini amedai kuwa idadi ya watu na mifugo inaongezeka, ameongeza kuwa kumekuwepo na mijadala kwenye vyombo vya habari kuhusu sakata zima la Ngorongoro na kuwa Serikali imekuwa ikifuatilia mijadala hiyo, ambapo amesema kuwa hali hiyo ni kuashiria cha uwepo demokrasia.

“Kumekuwepo na mjadala (Sakata la Ngorongoro) kwenye vyombo vya habari na wananchi, sisi kama Serikali tunaufatilia kwa sababu mjadala huu ndiyo demokrasia yenyewe, yaani pumzi ya demokrasia ni mjadala usipokuwepo mjadala ujue demokrasia imeminywa”- Waziri wa Maliasili na Utalii,Dkt. Damas Ndumbaro

Itakumbukuwa hivi karibuni Serikali imesema kuwa imeanza kupokea majina ya wananchi wa Ngorongoro wanaotaka kuhama kwa hiari, lakini jambo hilo limekuwa likihusiswa na propaganda licha ya Serikali kusema kuwa kama kuna mtu mwenye ushahidi au uhakika kuwa kwenye orodha hiyo yenye majina zaidi ya 400 sio mkazi wa Ngorongoro apeleke ushahidi ili hatua zichuliwe.

Vilevile kwa mara kadhaa sakata hilo limekuwa likiibua hoja mbalimbali juu ya ukiukwaji wa haki za binadamu, hasa kwa Mamlaka zinazosimamia hifadhi hiyo ambapo wadau mbalimbali ikiwemo watetezi wa haki za binadamu pamoja na wadau wa siasa wakishauri kuvunjwa kwa mamlaka hiyo ambayo imekuwa ikikana madai mbalimbali ambayo utolewa na baadhi Wananchi wa Ngorongoro ikiwemo kunyimwa haki za msingi ambazo udaiwa kuwa zipo kisheria.