Serikali imesema inatoa elimu bila ada na sio elimu bure na katika Waraka wa Elimu namba 3 wa mwaka 2016 unaainisha kuwa wazazi wana wajibu wa kushiriki kutoa michango kwa ajili ya maendeleo ya kiserikali ikiwemo kujenga miundombinu ya madarasa,vyoo na vinginevyo.
Kauli hiyo imetolewa hii leo Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI,Davis Silinde wakati akijibu swali la Mbunge wa Nkasi Aida Kenani.
Silnde amesema kuwa uchangiaji wa elimu unaoruhusiwa ni wa hiyari usiohusisha wanafunzi kutohudhuria masomo kwa kushindwa kutoa mchango.
“Majukumu ya jamii na wananchi kuhusu michango yamebainishwa katika waraka wa elimu namba 3 wa mwaka 2016 unaeleza kamati au bodi za shule zitashirikisha jamii katika maamuzi ya masuala mbalimbali yanayohusu maslahi ya maendeleo ya shule hususan uchangiaji wa hiyari na kuwasilisha maamuzi hayo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ili kupata kibali” ameongeza Silinde.
Silinde ameongeza kuwa serikali iliamua kutoa elimu msingi kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha nne bila malipo ili kuwezesha watoto wote wa kitanzania wenye rika la elimu msingi kupata elimu bila kikwazo chochote.
Habari Zaidi
DCI KINGAI ASISITIZA WAZAZI KUZINGATIA MALEZI BORA KWA WATOTO WAO ILI KUPUNGUZA UKATILI
THRDC,C-SEMA YAENDESHA MAFUNZO KWA POLISI NA WAENDESHA MASHITAKA