February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

SAKATA LA UJAMBAZI LATUA BUNGENI

Kassim Majaliwa-Waziri Mkuu wa Tanzania

Na Leonard Mapuli.

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amelithibitishia bunge kuwa serikali inafanya kila iwezalo kudhibiti kabisa vitendo vyote vya uhalifu vilivyoanza kujitokeza katika baadhi ya maeneo nchini Tanzania.

Waziri mkuu ameyasema hayo bungeni katika kipindi cha maswali na majibu kwa waziri mkuu baada ya mbunge wa Makete, Festo Sanga kutaka kauli ya serikali juu wimbi la uhalifu na hasa ujambazi katika majiji ya Dar es Salaam,Arusha,Mbeya na Mwanza ulioanza kuibuka hivi karibuni.

“Serikali inao wajibu wa kulinda raia wake,usalama wao,mali zao,lakini pia kuhakikisha wanaendesha shughuli zao za kila siku kwa amani na utulivu” amesema Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na kuongeza kuwa licha ya jukumu la ulinzi wa nchi kuwa mikononi mwa vyombo vya ulinzi na usalama ni wajibu wa kila mtanzania kushirikiana na vyombo hivyo kwa kutoa taarifa pindi anapoona viashiria vya uvunjifu wa amani.

Ni jukumu letu sote kuhakikisha kuwa tunashiriki kikamilifu kwenye ulinzi na usalama nchini,na kila mtanzania pale anapoona ama anapohisi kuna dalili za upotevu wa amani,ni vyema kutoa taarifa”,amesema Waziri Mkuu Majaliwa na kulipongeza jeshi la polisi kwa jinsi linavyofanya kazi kudhibiti vitendo vyote vya uhalifu vilivyoanza kujitokeza.

Siku za hivi karibuni, Rais Samia Suluhu alionya juu ya wimbi la ujambazi katika jiji la Dar es Salaam na kumtaka Mkuu wa Jeshi la polisi kulishughulikia haraka iwezekanavyo,hatua ambayo kwa mujibu wa Waziri Mkuu, inaendelea vizuri.

“Rais anapoagiza maana yake anaagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuchukua hatua kali dhidi ya hawa wote wanaosababisha madhara ya usalama, niwasihi Watanzania kutoa taarifa pale tunapoona kuna tatizo ili majeshi yetu yafanye kazi inayokusudiwa “ ,amehitimisha Waziri mkuu katika majibu yake juu ya suala la uhalifu na hasa ujambazi, aliloulizwa bungeni jijini Dodoma.

Bunge limetenga utaratibu wa maswali ya papo kwa papo kati ya wabunge na Waziri mkuu kila siku ya Alhamisi ambapo maswali mbalimbali huulizwa na kujibiwa kwa muda wa dakika thelathini.