February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

SAKATA LA SAMAKI KUFA MTO MARA LAMUIBUA OLENGURUMWA; ATAKA UCHUNGUZI UFANYIKE

Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), umeiomba Serikali kuwafanyia ukaguzi wananchi wanaotumia maji na rasimali kutoka Mto Mara, ili kubaini kama hawajapata madhara kufuatia madai ya mto huo kuwa na kemikali.

Wito huo umetolewaleo Ijumaa na Mratibu wa THRDC, Onesmo Olengurumwa wakati akihojiwa na Watetezi TV,siku moja baada ya Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Juma Chikoka, kupiga marufuku shughuli za kibinadamu ikiwemo uvuvi wa samaki kwenye mto huo.

Chikoka alipiga marufuku shughuli hizo kwa muda hadi Serikali itakapotoa maelekezo mengine, baada ya samaki wengi katika mto huo kufariki dunia, huku sababu ikitajwa kuwa kemikali iliyoingia ndani ya maji.

“Ni vyema sasa viongozi wakalichukua hili suala kwa uzito na kuanza kufuatilia kama kuna watu wameshatumia hao samaki wenye kemikali ili waweze kupatiwa matibabu haraka. Sababu madhara yatakuja kuonekana baadae,” amesema Olengurumwa.

Aidha, Olengurumwa ameshauri wananchi watakaopata madhara kufuatia changamoto hizo walipwe fidia na kampuni au watu waliosababisha kemikali kuingia katika mto huo.Pia ameshauri wale wanaotegemea shughuli za uvuvi na wanaotambulika sheria kulipwa fidia katika kipindi hiki ambacho wamesitisha shuguli zao katika mto Mara.

“Serikali iangalie hilo, lakini gharama zote za madhara haya yaliyosababishwa na kemikali hizi wabebe mgodi wenyewe, kugharamia gharama zote zitakazojitokeza kwa wananchi , Serikali na wengine,” amesema Olengurumwa.

Wakati huo huo, Olengurumwa ameishauri Serikali iweke sheria kali kudhibiti kampuni, watu au mtu kuachia kemikali ziingie kwenye vyanzo vya maji vinavyotumika kwa wananchi, wanyama na viumbe hai.

“Migodi kwa miaka mingi imekuwa ikilalamikiwa na imekuwa ikichafua mazingira na maji. Historia imeonesha na tulikuwa tunafuatilia miaka hiyo maji yamekuwa yakichafuliwa na watu wamedhurika wengi maeneo ya migodi na suala linaendelea,” amesema Olengurumwa.