February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

SAKATA LA NGORONGORO:IDARA NANE ZA UN ZATOA TAMKO,ZANUSA HARUFU YA UVUNJIFU WA HAKI ZA BINADAMU

Idara nane za Ushauri kuhusu Haki za Binadamu za Umoja wa Matifa (UN) zimeonyesha wasiwasi wao kwa serikali ya  Tanzania na mashirika ya kimataifa kufuatia kuwepo kwa mpango wa kutaka kuwahamisha wamasai wa Ngorongoro kutoka katika ardhi yao ya asili.

Katika taarifa yao iliyowasilishwa kwa serikali ya Tanzania mnamo February 9,mwaka huu  Idara hizo za UN wamesema kuiondoa jamii hiyo katika eneo lao la asili kwa jina la “kuendeleza uhifadhi” bila jamii hiyo kushirikishwa kikamilifu ni uvunjifu wa misingi ya haki za binadamu.

“Serikali imeshindwa kuwa na mbinu ya uhifadhi itakayojumuisha uhifadhi wa asili pamoja na kufanya kazi kwa pamoja na jamii hiyo ya kimasai iliyoishi na kuitunza ardhi hiyo vizazi hata vizazi,”imesema taarifa hiyo ikieleza mipango hiyo imeshindwa kujumuisha mzizi wa tishio la uchafuzi wa mazingira unaosababishwa na shuguli za kitalii katika hifadhi hiyo.

Aidha taarifa hiyo imeongeza kuwa kundi hilo la jamii ya kimasai ambao maisha yao ya kiutamaduni yanategemea Ngorongoro hawakushirikishwa,kukubaliana wala kutoa idhini yao ya awali juu ya mipango hiyo ya kutaka kuhamishwa kutoka hifadhini.

“Jamii hiyo ya kimasai wamekuwa wakitengwa katika nafasi za uongozi katika Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro na mara kwa mara wamekuwa wakikabiliwa na mlolongo wa matukio ya kutaka kuondolewa kwa nguvu  hifadhini,”imesema taarifa hiyo.

Idara hizo za UN zilizotia saini barua hiyo ni  Idara ya masuala ya chakula, Makazi,Haki za Kiutamaduni,Mazingira,Chakula,Jamii za watu wa asili,Wakimbizi wa ndani,Umasikini pamoja na Idara ya masuala ya maji, wamesema serikali ya Tanzania imeshindwa kuzingatia mbinu ya uhifadhi ambayo inajumuisha uhifadhi wa asili na kushirikiana na jamii katika utunzaji na kuendeleza uhifadhi Ngorongoro.

“Tuna wasiwasi kwamba kuhamishwa kwa wamasai kutoka katika ardhi yao ya asili kutatenganisha uhusiano wao wa kiroho na kimwili na mazingira yao wanayoyaona ni “nyumbani”,hali hiyo itasababisha ukosefu wa makazi pamoja na athari za kiakili na itakuwa ni kizuizi katika kutimiza haki za msingi za upatikanaji wa maji salama na usalama wa chakula,”imeongeza taarifa hiyo.

Wamesema ushiriki kikamilifu wa wananchi katika ngazi na michakato ya kutoa maamuzi ni wa muhimu kwani unahitajika na Kamati ya Urithi wa Dunia ya UNESCO lakini licha ya umuhimu huo jamii hiyo imekuwa haishirikishwi katika mipango na maamuzi ya uendeshaji wa mbuga hiyo.Hata hivyo UNESCO iliwahi kutoa taarifa yake na kusema kuwa haijawahi kuagiza wamasai wa Ngorongoro waondolewe hifadhini

Aidha Idara hizo za UN , wameiomba Kamati hiyo ya urithi wa dunia kuzingatia kwa makini kuwa kuunga mkono mipango hiyo wakati kumekuwepo na shutuma kadhaa zilizoibuliwa kuwa utekelezaji wa mipango hiyo unaweza kukiuka haki za jamii hiyo ya asili,hivyo waeiomba Kamati hiyo kutokana na ukaribu wake na serikali ya Tanzania kuhakikisha kwamba mipango hiyo kuhusu Ngorongoro inaendana na haki za binadamu.

“tuna wasiwasi kwamba mipango hii imeendeshwa bila ushirikishwaji wa wananchi ambacho ni kinyume na sharia za kimataifa za haki za binadamu hususan haki za kuwa na makazi bora ya kuishi,chakula,maji safi na salama,na haki ya kushiriki katika uundaji na utekelezaji wa sera na maamuzi ambayo yanaweza kuathiri haki ya mtu ya kiutamaduni,”imeongeza.