February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

SAKATA LA NGORONGORO, ‘MASLAHI MAPANA YA TAIFA’ MSAMIATI AMBAO HAUTAKIWI KUTUMIWA KISIASA

Kati ya msamiati ambao umekuwa ukitoka kwenye vinywa vya wanasiasa wengi pamoja na baadhi ya wanaharakati wanapokuwa  wanataka kuhalalisha hoja zao ambazo mara kwa mara huziwasilisha kwa umma ni ngumu kuacha msamiati huu ‘maslahi mapana ya Taifa’.

Tokea sakata la Ngorongoro liibuke msamiati huo umekuwa ukitumiwa sana hususani na baadhi ya viongozi ambao wapo kwenye mamlaka za Serikali, Wanaharakati, Wanahabari pamoja na taasisi zisizo za kiserikali, lakini kwa jicho la tatu msamiati huu umekuwa ukitumiwa zaidi na wale ambao wamekuwa wakishawishi au kutaka jamii hiyo ya kimasai kuhamishwa ndani ya hifadhi ya  Ngorongoro.

Pia endapo msamiati huo hautatumika vizuri huenda maslahi binafsi ya makampuni ya kitalii, kiwindaji na wawekezaji wa mahoteli wanaweza jificha katima kivuli hicho  cha maslahi mapana ya Taifa.

Kati ya hoja ambayo imekuwa ikipigiliwa msumari ni ile ya kuwataka wakazi katika eneo la Ngorongoro kuhamishwa kwa madai ya maslahi mapana ya Taifa huku watu mbalimbali wakiibua hoja zao kuwa endapo wakazi hao wataendelea kubaki basi Ngorongoro ipo hatarini kupotea.

Wakazi wa eneo la Ngorongoro hawapo katika hifadhi hiyo kwa bahati mbaya ama kwa bahati nasibu wapo kwa uwezo wa Mungu takribani miaka 1000 sasa wilayani Ngorongoro na badaye kuingia makubaliano ya kudumu ya uwepo wao hapo, hata baada ya hifadhi ya Ngorongoro kuanishwa mwaka 1959.

Lakini kuibuka kwa mgogoro huu kwa mara nyingine huku wengi wakitumia propaganda hasi za kuaminisha umma kuhusu kile wananchokiamini kuhusu Ngorongoro na hata baadhi ya vyombo vya habari kufanya mahojiano na watu ambao sio wakazi halisi wa Ngorongoro ili kuhalalisha hoja yao ya ‘maslahi mapana ya Taifa’ ni kuikosea jamii ya wamasai wanaoishi Ngorongoro.

Ikumbukwe kuwa Mojawapo ya misingi ya kuanzishwa kwa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ni kuendeleza maisha ya jamii ya asili iishiyo Ngorongoro,Je kama uhifadhi na maisha ya binadamu haviwezekani nani anapaswa kutumiwa lawama? Mamlaka ya Hifadhi au wana Ngorongoro? Ni vyema kujadili kwa kina na kudadavua ili kuwa na majibu sahihi na utatuzi wa kudumu, maana ili utibu ugonjwa ni lazima ukifahamu chanzo.

Kwa mtazamo wangu kuwahamisha wananchi wa Ngorongoro kunaweza kupoteza uhalisia wa hifadhi hiyo iliyojizolea umaarufu na upekee kwa binadamu kuishi na wanyama wa porini pamoja na aghalabu sana kudhuriana.

Hoja ya ‘Maslahi mapana ya Taifa’  umekuwa ukitumika sana , lakini ieleweke zaidi msamiati huo umekuwa ukitumiwa zaidi na upande unaotetea kuwa jamii hiyo inatakiwa kuondoka eneo hilo, wengi wao wanao simamia msimamo huo wamekuwa mstari wa mbele kutumia hata propaganda hasi za kuichafua jamii hiyo.

NINI MAANA YA MSAMIATI HUO KIUHALISIA? (MASLAHI MAPANA YA TAIFA)

Kwa mtazamo wa jicho la tatu msamiati huo ni masamiati wa kisiasa amabao umekuwa kama mtindo wa lugha utumikao katika mazingira maalumu (wataalamu wa kiswahili wanaita ‘Rejesta’). Kimtazamo kila mmoja kuna anavyoweza kuuleza msamiti huo, ikiwa na maana pia kila mtu kuna anavyoweza kuutafsiri kulingana na mazingira unapotumiwa.

Licha ya msamiti huo tafsiri yake kutegemea mtazamo binafsi katika kutafsiri, lakini hakuna namna yoyote ya mantiki ya kitafsiri inayoweza kutenganisha msamiti huo, kabla ya kufikia neno Taifa bila kujumuisha wananchi, hakuna Taifa bila Wananchi! neno maslahi mapana ya Taifa hayawezi kutenganishwa na Wananchi. Kwenye Nchi zinazoongozwa kidemokrasia mamlaka upata nafasi kutoka kwa Wananchi ( inaweza hisiwe hivyo lakini inatakiwa kuwa hivyo), kwa kutambua umuhimu wa Wananchi uamuzi wa namna yoyote utakiwa kuzingatia kuwapa nafasi wananchi hao kutoa maoni kupitia milija mbalimbali kuwa wanaitaji nini au hawataki nini.

Kuipa hoja uzito wa ‘Maslahi ya Taifa’ bila ushirikishwaji wa  wananchi au kuwapa nafasi rafiki ya kutoa maoni yanayoweza kuongeza wigo wa kimtazamo kabla ya kufikia uamuzi, huo ni usiasa usiyo na tija kwa Taifa endelevu.

Hoja ya maslahi mapana ya Taifa kwenye sakata la Ngorongoro inatakiwa kwenda sambamba na tafiti na kuwapa fursa rafiki wananchi kuwasilisha mitazamo yao,maoni, tafiti huru za kitaalamu zisizofungamana na maslahi ya upande wowote, kuacha wazi zaidi dirisha la majadiliano baina ya pande hizo mbili zinazosigana.

Inapotokea hayo yakashidwa kuzingatiwa ni rahisi maslahi binafsi yakavalishwa joho la maslahi mapana ya Taifa kwa kujua au kutokujua, lakini jambo ambalo ubeba maslahi binafsi badala ya maslahi mapana ya Taifa hujulikana kwa muda mfupi, Taifa linaweza kuingia hasara kubwa au uamuzi wa awali kuibua sintofahamu zaidi hata kuwa na viongozi wasioaminika kwenye nyoyo za wananchi wengi kutokana na kuamini matokeo hasi kuwa chanzo chake ni viongozi ambao ndio upuliza kipyenga cha mwisho.

MAKALA HII NI MAONI BINAFSI YA MWANDISHI