March 23, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

SAKATA LA NGORONGORO: ACT WAZALENDO WATAKA MHIFADHI MKUU,BODI KUONDOLEWA


Warning: file_get_contents(https://www.youtube.com/get_video_info?video_id=): failed to open stream: HTTP request failed! HTTP/1.0 410 Gone in /home1/watetezi/public_html/wp-content/themes/watetezi/inc/template-functions.php on line 834

MHIFADHI NGORONGORO AONDOLEWE

MHIFADHI NGORONGORO AONDOLEWE

 

Na: Anthony Rwekaza

Chama cha ACT Wazalendo kimeshauri mamlaka za uteuzi, kumtengua Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Ngorongoro, Dkt. Freddy Manongi, kutengua bodi ya mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro pamoja na kuvunjwa kwa mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro kutokana na kushindwa kutekeleza majukumu yao.

Akizungumza leo Februari 15, 2022 kwa niaba ya Chama chake Msemaji wa Sekta ya Aridhi na Maendeleo ya Makazi (Waziri kivuri), Wakili Bonifasia Mapunda amesema ACT Wazalendo inapendekeza kwa mamlaka ya uteuzi ambayo yapo kwa Rais wa Nchi kutengua uteuzi wa muhifadhi Mkuu wa Ngorongoro Dkt. Freddy Manongi kutokana na kushindwa kutekeleza majukumu yake ndani ya hifadhi ya Ngorongoro, hali ambayo amedai inapelekea wananchi kukosa huduma muhimu, kama huduma ya maji safi na salama, chakula, huduma za afya pamoja na barabara.

“Tunapendekeza Mamlaka ya Uteuzi itengue uteuzi wa Mhifadhi Mkuu wa
Mamlaka ya Ngorongoro Daktari Freddy Manongi kwa kushindwa
kutekeleza majukumu yake ipasavyo hadi kupelekea Wakaazi wa Hifadhi ya
Ngorongoro kukosa huduma muhimu kama maji safi na salama, chakula,
barabara na huduma za afya.” amesema Bonifasia Mapunda

Pia amesema kumekuwa na malalamiko ya kutoka kwenye jamii ya kimasai inayoishi ndani ya hifadhi juu ya madai ya kufanyiwa vitendo vya unyanyasaji kwa amri ya
Mhifadhi, lakini alipoulizwa juu Dkt. Manongi alipoulizwa kuhusu madai hayo amesema jambo hilo hawezi kulisemea kwa wakati huo (alipoulizwa). Hata hivyo Msemaji huyo amedai Manongi ameshatimiza miaka 60 ya
kustaafu toka mwaka 2021 hvyo ameshauri kuwa umri huo alionao kwa sasa ni muafaka kupumzishwa”

Ameongeza kuwa wanapendekeza kwa mamlaka ya uteuzi kutengua mamlaka ya Bodi ya hifadhi ya Ngorongoro kutokana na kushindwa kutekeleza majukumu yake ya kushauri Serikali ipasavyo juu ya kuendesha hifadhi hiyo, huku pia ACT inashauri Serikali kuachana na mpendekezo yaliyopo kwenye ripoti inayoishauri Serikali juu ya wananchi wa Ngorongoro kuondolewa hifadhini wamedai ripoti iliandaliwa bila wananchi pamoja na wadau kushirikishwa.

“Tunapendekeza kwa Mamlaka ya Uteuzi kuwa Bodi ya Mamlaka ya Hifadhi
ya Ngorongoro ivunjwe kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake na
kuishauri serikali ipasavyo juu ya Hifadhi hii.Tunapendekeza Serikali iachane na Mapendekezo yote yaliyotolewa katika
Ripoti ya Matumizi Mseto ya Ardhi ya Ngorongoro yaani The Report on
Multiple Land Use Management Plan ikiwa ni pamoja na pendekezo la kuondoa watu katika hifadhi ya Ngorongoro. Ripoti hiyo iliandaliwa bila ushirikishwaji wa Jamii ya Wamaasai waishio Hifadhini na wadau wa
uhifadhi.”amesema Bonifasia Mapunda

Licha ya mapendekezo hayo pia wameshauri kuvunjwa kwa mamlaka ya Ngorongoro (NCAA) ivunjwe na badala yake iundwe kampuni yenye yenye itakayomilikiwa kwa ubia baina ya wananchi na Serikali huku wananchi wakipewa asilimia kubwa ya ubia huo, lakini wamedai uendeshaji wa kampuni uratiwe na Seriali.

“Tunapendekeza Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) ivunjwe na
badala yake iundwe Kampuni yenye kumilikiwa kwa Ubia kati ya Wananchi
Waishio Ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro na Serikali. Wananchi wamiliki
51% na Serikali 49%. Uendeshaji wa kampuni hii uwe mikononi mwa
Serikali. “amesema Bonifasia Mapunda

Vilevile wamependekeza kuwepo na majadiliano (Dialogue) baina ya pande mbili kati ya Serikali (Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro) kwa upande mmoja na Jamii jamii ya wawakilishi wa wenyeji wanaoishi ndani ya Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro kwa upande wa pili, huku pia wakishauri kuundwa kwa timu kwa ajili ya kufanya uchambuzi yakinifu kwa kuzingatia misingi ya demokrasia na kisheria ili kuandaa hadidu rejea kwa ajili ya kukabiliana na changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikioelekea migogoro.

Emmanuel Lazarus Mvula ambaye ni msemaji wa ACT Wazalendo katika Sekta ya Fedha na Uchumi ambaye amedai amekuwa akifuatilia kwa karibu sakata la Ngorongoro kwa muda murefu nae amepata fursa ya kufafanua baadhi ya mambo.

Amesema tofauti na mambo mengi ambayo yanasikika yakisemwa lakini wananchi wa Ngorongoro wameendelea kuwa watu muhimu kwenye hifadhi hiyo, amedai kuwa umuhimu huo unathibitishwa kwa idadi ya faru weusi wanaopatikana kwenye hifadhi hiyo pekee licha ya awali kuwepo kwenye hifadhi nyingine.

“Tofauti na mengi mliyoyasikia katika majuma haya mawili, wananchi wa Ngorongoro wameendelea kuwa ni wahifadhi namba moja na hili linathibitishwa kwa idadi ya wanyama katika hifadhi hasa Faru weusi ambao wamebaki katika Hifadhi hii pekee wakati walikuwepo katika hifadhi zote.” amesema Emmanuel Lazarus Mvula

Pia Msemaji huyo amedai kuwa madai yanayotolewa na Mamlaka, Wabunge, watu na pamoja na kikundi cha baadhi ya waandishi wa habari kuwa wananchi hao wanaishi katika mazingira magumu na hatarishi ni kichekesho, amesema hatakiwi kulaumiwa kwa sababu wanaotakiwa kutoa huduma hizo ni Mamlaka ya Ngorongoro kwa mujibu wa Sheria.

Amedai Mamlaka imeshindwa kutekeleza majukumu yake na badala ya kulaumiwa na kulazimishwa kutoa huduma hizo inawatupia lawama wananchi wanaoishi kwenye hifadhi ya Ngorongoro, amedai licha ya jamii hiyo wananyimwa huduma za muhimu ambazo ni haki zao lakini wanaendelea kusimamia msimamo wao.

Ameeleza kuwa mgongano wa kimtazamo umekuwa chanzo cha sintofahamu ya muda mrefu baina ya jamii inayoishi kwenye hifadhi hiyo na mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro, amedai kwa kipindi kirefu jamii hiyo imekuwa ikilalamikia kutoshirikishwa ipasavyo katika usimamizi wa eneo hilo kwenye michakato ya tafiti mbalimbali ambazo ufanyika pamoja kushiriki katika utengenezwaji wa mipango kama vile GMP.

“Mgongano huu wa kimatazamo umekuwa chanzo cha sintofahamu ya muda mrefu kati ya jamii na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro. Jamii imelalamika kutengwa katika usimamizi wa eneo hili. Jamii ya wafugaji wakazi wa eneo hili kwa muda mrefu sana, wameomba kushirikishwa katika mapendekezo ya mabadiliko ya sheria ya usimamizi wa eneo, kushirikishwa katika tafiti mbalimbali na utengenezwaji wa mpango wa kusimamia eneo zima maarufu kama GMP (General Management Plan). Juhudi za jamii kuomba kushiriki katika kutambua na kutatua changamoto zinazoikabili Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro zilionekana kugonga mwamba kwa muda mrefu.” amesema Emmanuel Lazarus

Lakini Msemaji huo wa kisekta Emmanuel Lazarus ameeleza mbele ya vyombo vya habari kuwa eneo la Hifadhi ya Mamlaka ya Ngorongoro ni ardhi inayomilikiwa kimila na wafugaji amesema kuna vijiji 25 ndani ya eneo hilo ambavyo hadhi zao siyo tofauti na vijiji vyote Tanzania.

Ameongeza kuwa Mwaka 1958- 1959 Serikali ya kikoloni ya Tanganyika iliwahamisha kimabavu jamii ya kimasai kupisha kuanzishwa kwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti yenye ukubwa wa kilometa za mraba 15,000 ambapo amedai jamii hiyo ilibakiwa na eneo dogo (8,100 km2), la iliyokuwa ardhi yao, yaani NCA. Amesema pamoja na hayo wafugaji hao wanatumia ardhi hiyo na wanyamapori na watalii.

Amedai kuwa Serikali ya kikoloni iliahidi mwaka 1958 kuwa haitawahamisha tena wa jamii hiyo ya kimasai kutoka Ngorongoro. Ambapo amesema Mwaka 1975 sheria ya Ngorongoro iliunda Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) – Game Parks Miscilleneous Amendment Act 1975 na kuipa hadhi ya mtu kisheria aneyeweza kushtaki na kushtakiwa kwa jina lake.

Itakumbukuwa kumekuwepo na mkindhano wa hoja juu ya sakata la Serikali kutaka kuwaamisha baadhi ya wananchi wanaoishi Ngorongoro kwa madai kuwa wao wameongezeka pamoja na mifugo, baadhi ya wadau mbalimbali wakiwemo watetezi wa haki za binadamu na wanaharakati wamekuwa wakipinga hoja hizo na kuishari Serikali kuzingatia sheria na taratibu ikiwemo masuala ya haki za binadamu katika kushughulikia mgogoro huo, wakitaka jamii ya kimasai inayoishi kwenye hifadhi hiyo kushirikishwa ili kupata muafaka wa pamoja namna ya kulinda na kuendeleza hifadhi hiyo.

Hata hvyo Waziri Kassim Majaliwa akiambatana na watendaji wengine wa Serikali wameanza kufanya ziara kwenye jamii hiyo ili kutafuta suluhu ya mgogoro ambao umekuwa ukigonga vichwa vya habari pamoja na kuibua gumzo na mjadala katika vyombo vya habari pamoja na kwenye mitandao ya kijamii.