February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

SAKATA LA MTO MARA; HECHE AITAKA SERIKALI IFANYE UCHUNGUZI HURU

Serikali ya Tanzania, imeombwa kuunda tume huru kwa ajili ya kuchunguza chanzo cha mabadiliko ya maji ya Mto Mara, yaliyosababisha athari ikiwemo vifo vya samaki kadhaa.

Witu huo ulitolewa jana Jumatatu na aliyekuwa Mbunge wa Tarime Vijijini John Heche, akitoa maoni yake kuhusu matokeo ya kamati maalumu iliyoundwa na Serikali, kuchunguza sakata hilo, ambayo yalidai mabadiliko ya maji ya mto huo yamechangiwa na ongezeko la kinyesi cha wanyama.

“Tunaitaka Serikali itafute au iunde timu nyingine huru, yenye watu huru hata wakiwa wachunguzi wa kimataifa wachunguze sababu hili jambo linahusu  maisha ya watu. Tutafute maabara huru hata za nje ya nchi, ichunguze kisha iwaambie Watanzania ukweli ili kuondoa hofu,” alisema Heche.

Katika hatua nyingine, Heche alimuomba Rais Samia Suluhu Hassan, amfukuze kazi Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Selemani Jafo, kwa kushindwa kuwajibika katika suala hilo.

Heche ameiomba Serikali ichukue hatua za dharura kuwanusuru wananchi wanaotumia maji ya mto huo, kwa kuwapelekea maji safi na salama ya kutumia wakati ufumbuzi wa sakata hilo ukitafutwa.

Wito hup umekuja ikiwa zimepita siku kadhaa tangu kamati maalumu ya kitaifa iliyoundwa na Serikali kuchunguza mabadiliko ya maji ndani ya Mto Mara, kusema chanzo cha tatizo hilo ni shughuli za binadamu pamoja na nguvu za asili.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Prof. Samuel Manyele alisema changamoto hiyo ilipelekea kuwepo kiwango kikubwa cha kinyesi cha mifugo mtoni, pamoja na uozo wa mimea ndani ya mto, hasa mimea vamizi kama vile maji na matete.

Hata hivyo prof. Manyele amesema mgodi wa dhahabu wa Barrick North Mara,  hauhusiki na uchafuzi huo.