February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

RIPOTI CAG IFANYIWE KAZI ,MIFUMO YA KIFEDHA IBADILISHWE

Na Evarist Mapesa

Mjadala mzito unazidi kufukuta nchini Tanzania tangu kutolewa kwa Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Charles Kichere, iliyoibua ‘uozo’ katika Taasisi na Sekta mbalimbali za kiserikali kutokana na kutumia vibaya fedha bila kufuata utaratibu,sera,kanuni na sharia zinazoiongoza taifa hilo la Afrika Mashariki.

Wachambuzi wa masuala ya uchumi nchini Tanzania wanaamini kuwa ‘upigaji’ huo ambao umekuwa ukijitokeza mara kwa mara katika ripoti mbalimbali za CAG ni kutokana na uratibiwaji wa kimfumo wakiamini iwapo hakutakuwa na mabadiliko ya kikatiba na kimfumo, matokeo haya yataendelea kuwepo kwa sasa na miaka mingine ijayo kwani watu wamekuwa wakiangalia mianya iliyopo na kuitumia ipasavyo.

Ripoti hii inajaribu kuonesha kuwa uchumi wa Tanzania unavuja kwa kiwango kikubwa katika eneo la matumizi ya fedha za umma, eneo hilo ndicho kitovu muhimu kwa uchumi wa nchi yeyote ile duniani, na kiunganishi muhimu wa masuala ya uendeshaji ya masuala ya uwajibikaji.

Kwa mujibu wa mchambuzi wa masuala ya uchimi nchini Tanzania Bravious Kahyaza anaamini kuwa kiwango cha upotevu wa fedha ni makubwa sawa na zaidi ya asilimia 6.7 ya ukuaji wa kile kinachochangia ukuaji wa uchumi kila mwaka katika nchi ya Tanzania (total factor productivity)

“Ukienda kwenye takwimu za pato ghafi la nchi, ukichukua kiwango cha ukuaji ule (total factor productivity), ukachukua fedha kwenye taasisi zote kubwa za umma, utakuta inachukua asilimia 6.7 ya total factor productivity, sasa kama unapoteza asilimia hizo maana yake ni kwamba ukuaji wa uchumi wenu ambao ni halisia, hauwezi kuleta matokeo kwa umma”, alisema Kahyaza.

Kwa mujibu wa wataalam wa uchumi ulimwenguni wamekuwa wakishauri kuwa ni sharti  kutokupoteza zaidi ya asilimia 3.5 ya kile kinachochangia katika ukuaji wa tija, kisipotee kwa kiwango hicho, lakini hali hiyo ni tofauti kwa Tanzania ambayo imepoteza zaidi ya mara mbili ya pato hilo.

Kwa sasa nchini Tanzania kumekuwa na mijadala ambayo inazidi kufukuta hasa kwenye mitandao ya kijamii, baadhi ya watu wamekuwa wakielezea hisia zao kutokana na ripoti hiyo iliyotolewa siku chache zilizopita na kubaini kuwa mashine 89 za ambazo zimekuwa zikitumika katika makusanyo ya faini za makosa ya usalama barabarani zinazotumiwa na trafiki hazijawahi kurekodi muamala hata mmoja kwenye mfumo wa malipo wa Serikali.

Suala hilo bado linaendelea kuwashangaza walio wengi kwani kila siku barabarani madereva na wamiliki wa vyombo vya moto wamekuwa wakitozwa faini za makosa mbalimbali na cha kushangaza ni kwamba hutoa pesa za faini hizo na kupewa lisiti inayoonesha kuwa mtuhumiwa kalipia kiasi fulani kutokana na kosa husika.

Swali la kujiuliza ni je, lisiti hizo ambazo zimekuwa zikitolewa huwa zinatoka wapi? kuna mtambo usio rasmi ambao umekuwa ukitumiwa kutoa risiti hizo? kama ni ndiyo nani anauendesha? na kwanini pesa hizo hazijawahi kurekodiwa na serikali? zimeenda wapi? na akina nani wanaohusika katika mkondo huo?.

Kahyaza, anasema kuwa ukosefu wa makusanyo hayo katika eneo hilo la barabarani unaathiri ukuaji wa uchimi, uwezo wa serikali kukusanya mapato,unaathiri moja kwa moja vipato vya watu.

“Ili uchumi wa nchi uweze kukua, unahitaji serikali inayokusanya mapato, na ungaangalia kiwango cha mapato kwa mtu mmoja mmoja, kwa hiyo ukiwa na kiwango cha fedha nyingi ambazo hazipiti katika mfumo, lazima uwezo wa serikali kupata mapato lazima utapungua”,alisema Kahyaza.

“Kupungua kwa makusanyo yatokanayo na kodi maana yake uwezo wa serikali kupeleka huduma kwa mtu mmoja unakuwa unapungua na ikipungua inaenda moja kwa moja tena kuathiri uwezo wa serikali kutumia mambo muhimu, hivyo uchumi kusinyaa au haukui kwa kiwango ambacho kinaweza kutokea, maana yake utapata kipato kidogo”,aliongeza Kahyaza.

Mbali na kasoro zilizojitokeza katika mashine 89 za makusanyo ya faini za makosa ya usalama barabarani lakini pia ripoti hiyo ilimulika suala la mishahara hewa kwa watumishi wasiostahili na kusababisha upotevu wa fedha za umma.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo Mamlaka ya Serikali za mitaa 25 zililipa Sh556.84 milioni kwa watumishi waliostaafu, waliofariki, waliotoroka, walioachishwa kazi na watumishi waliokuwa likizo bila malipo.

Ikumbukwe mwanzoni mwa mwezi April 2016, katika ripoti mpya iliyotolewa baada ya ukaguzi wa wafanyakazi hewa nchini Tanzania, ilibaini kuwa serikali ilikuwa ikiwalipa wafanyakazi hewa takribani 2000 kutoka mikoa mbalimbali nchini.

Suala hili Kahyaza amesema mazingira na mifumo ya nchi inaruhusu watu kutumia mianya hiyo  kujinufahisha wao wenyewe lakini pia siasa imekuwa ikipelekea watu kufanya hivyo pasipo hatua zozote kuchukuiwa.

“Mfumo wetu unahitaji kubadilishwa kama ambavyo watu wameanza kuchukua hatua katika mataifa mengine, jambo lingine ni kupeleka mamlaka kwenye kitovu jinsi watu wanavyolipwa huku taasisi zinazoundwa za utumishi ziwajibike zaidi kwenye hayo mazingira,” alisema Kahyaza.

Ripoti hiyo pia imeonyesha deni la taifa hadi kufikia Juni 30, 2021 deni la Serikali lilifikia trilioni 64.52 kutoka trilioni 56.76 mwaka 2019/2020 ikiwa ni ongezeko la trilioni 7.76 sawa na asilimia 13.7 ikilinganishwa na ongezeko la trilioni 3.65, sawa na asilimia saba kwa mwaka uliopita.

Ongezeko hilo limekuwa likiibua maswali mengi kwa wananchi na viongozi juu ya ukopaji na matumizi ya fedha hizo huku wengine wakienda mbali kwa kutabili kile kitakachokuja kuja kutokea siku za usoni.

Hata hivyo serikali mara zote imekuwa ikisema kipimo cha deni la Serikali kinachotumia pato la Taifa kinaonyesha kuwa deni ni himilivu.

Kahyaza amesema taifa linakuwa na deni himilivu pale deni linakuwa chini ya asilimia 50 la pato lako ghafi, taifa bado inaweza kuendelea kukopa, ukusanyaji wa mapato kama hauathiri malipo ya deni la taifa na rasiliamali zikiwa sawa.

“Ni makosa makubwa sana kufananisha Tanzania na mataifa makubwa namna ambavyo yanakopa kwa sababu ili kujua njia hiyo siyo sahihi kuna vitu vitatu vya kuangalia ambavyo ni deni lako unalikopa kwenye thamani ya fedha ipi? mfano sisi sarafu yetu ikishuka kwa asilimia moja dhidi ya dora ya kimarekani deni letu linaongezeka kwa zaidi ya bilioni 316”.

“kigezo kingine ni ikiwa unakuwa na deni kubwa harafu deni hilo linaingizwa kwenye uchumi  lakini maisha ya watu hayakui huku umaskini wa raia haupungui kwa kiwango ambacho unakopa pia kuangalia uhusiano uliopo kati ya hoja za kihasibu na kiuchumi,” alisema Kahyoza.

Kwa miaka ya hivi karibuni Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa Serikali imekuwa ikibainisha utumiaji mbaya wa fedha na rasilimali za umma hali ambayo hupelekea kuiletea nchi hasara na kushindwa kupiga hatua za kimaendeleo.