February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

RAIS SAMIA:AGOSTI 23 NI TAREHE YA SENSA

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amesema Sensa ya Watu na Makazi ya 2022, itafanyika Jumatatu, ya tarehe 23 Agosti 2022.

Rais Samia ametangaza tarehe hiyo leo Ijumaa, akizindua nembo na tarehe ya sensa, visiwani Zanzibar.

“Napenda kutamka rasmi kuwa, tarehe 23 Agosti mwaka huu, ni tarehe ya sense ya watu na makazi kwa hapa nchini kwetu Tanzania,” amesema Rais Samia.

Mkuu huyo wa nchi amehimiza Watanzania wote washiriki zoezi hilo, ili kuiwezesha Serikali kupata idadi yao kamili kwa ajili ya kupanga shughuli za maendeleo.

“Naomba kila Mtanzania aliye hai ahesabiwe tujue idadi, ili tukijipanga tujue tunajipanga kwa namna gani. Mkawasomeshe wananchi kila mmoja aelewe kwamba, tunahesabiwa ili kwenda sawa na hesabu zetu za maendeleo ya kiuchumi, hakuna sababu nyingine iliyofichwa,” amesema Rais Samia.

Aidha, Rais Samia ameagiza nembo ya sensa itumike katika shughuli mbalimbali za kiserikali na sekta binafsi, ili kulitangaza zoezi hilo kwa wananchi.

“Wito wangu nembo hii itumike kuanzia itakapozinduliwa kwa shughuli ya sense, hadi itakapokamilika. Shughuli zote za Serikali na sekta binafsi tumieni nembo hii kuitangaza sense, kwa kuiweka katika tovuti zenu na taasisi zitakazokuwa na vipindi katika Tv zenu nembohizi zitumike,” amesema Rais Samia na kuongeza:

“Sekta binafsi nembo zinaweza kuwekwa kwenye bidhaa mbalimbali zinazozalishwa nchini, ikiwemo kwenye maji, risiti. Kila kinachotumika basi nembo ya sensa ionekane.”