February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

RAIS SAMIA, MWINYI WASHIRIKI KUMBUKIZI MIAKA 50 YA KIFO CHA KARUME

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, pamoja na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi, wameongoza dua ya kumuombea muasisi wa Serikali ya Mapinduzi visiwani humo, Hayati Abeid Aman Karume, aliyeuawa tarehe 7 Aprili 1972.

Dua hiyo imefanyika leo Alhamisi, katika kumbukizi ya miaka 50 ya kifo cha Hayati Karume, iliyofanyika katika ofisi ndogo za CCM Zanzibar.

Kumbukizi hiyo ilihudhuriwa na viongozi wa kitaifa wa Tanzania na Zanzibar, ambao ni Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk. Phillip Mpango, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Wengine ni Makamu wa Rais wa visiwa hivyo, Othman Masoud Othman (wa kwanza) na Hemed Suleiman Abdullah (wa pili), Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Saleh Omari Kabi, pamoja na Kaimu Kadhi Mkuu Zanzibar, Sheikh Hassan Othman Ngwali.

Pia, wanafamilia ya Hayati Karume, walishiriki kumbukizi hiyo, akiwemo Rais Mstaafu wa Zazibar na, Amani Abeid Karume, pamoja na mama yake, Fatma Karume.

Mawaidha katika kumbukizi hiyo yalisomwa na Mjumbe wa Baraza la Ulamaa, Sheikh Hamis Abdulhamid, aliyesema Hayati Karume aliwawekea Wazanzibar msingi wa taaluma kwa kufungua Chuo cha Kiislamu 1972,ambacho kimetoa maulamaa, akiwemo yeye.

“Ametuwekea misingi hii sababu ije imfae kesho akhera na itamfaa sababu Mtume anatuhadithia kwamba, mwanadamu anaacha mambo matatu ambayo ni muhimu sana, akasema ukifanya sadaka ambayo itaendelea na itawafaa wa baadaye, basi na yeye huko aliko atakuwa anapata fungu lake,” amesema Sheikh Hamis.