February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

RAIS SAMIA KUWAPIMA MA-RC KUPITIA MFUMO WA M-MAMA

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amesema atatumia mfumo wa usafirishaji wa dharura wa wajawazito na watoto wachanga (M-MAMA), kupima utendaji wa halmashauri na wakuu wa mikoa.

Akizungumza katika uzinduzi wa mfumo huo, leo Jumatano, jijini Dodoma, Rais Samia amesema ataingia makubaliano na wakuu wa mikoa, kuona kama watetenga fedha za utekelezaji wa mfumo huo utakaofanya kazi katika mikoa 14.

“Niagize halmashauri zote zitakazopitiwa na mpango huu, kama nilivyoagiza mwanzo kuangalia suala la lishe bora kwa wajawazito na nikawataka watenge fedha tukawa tunasainishana kwenye kadi, nitawasainisha hapa wakuu wa mikoa kuona mnatenga fedha zinazokwenda kutia nguvu kwenye mpango huu. Lengo kuokoa maisha ya mama na mtoto,” amesema Rais Samia.

Amesema mfumo wa M-MAMA utasaidia kupunguza vifo vya wajawazito na watoto wachanga wakati wa kujifungua, kwani utawasaidia kupata usafiri wa hakika na haraka kwenda hospitali kujifungua.

Katika hatua nyingine, Rais Samia amesema, Serikali inatarajia kutoa ajira 32,000, ambapo baadhi yake zitahusu sekta ya afya na elimu, ili kuboresha utoaji huduma za afya na elimu kwa wananchi.

Mbali na Serikali yake kupanga kutoa ajira hizo, Rais Samia amesema Serikali yake imeagiza magari ya kubebea wagonjwa ya kawaida 233 na mengine 25 ambayo yanafanana na vituo vya afya. Magari hayo yatasambazwa nchi nzima.