February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

RAIS SAMIA AWEKA WAZI KINACHOSABABISHA MGAO WA MAJI

Na: Anthony Rwekaza

Kufuatia uwepo wa mgao wa maji unaondelea kwenye kwenye maeneo mbalimbali Nchini hususani katika Jiji la Dar es salaam, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amebainisha vyanzo mbalimbali vinavyopelekea uwepo wa changamoto hiyo.

Akizungumza leo Alhamasi Novemba 18, 2021 katika maadhimisho ya miaka 50 tokea kuanzishwa kwa Hospitili ya Bugando iliyoko Mkoani Mwanza, ameeleza umati wa wananchi waliojitokeza pamoja na Umma wa Watanzania kuhusiana na changamoto ya upatikanaji wa maji.

Rais Samia Suluhu Hassan amesama wananchi wa Jiji la Dar es salaam utegemea maji kutoka Mto Ruvu, ambao amedai maji kwenye mto huo yamepungua kwa kiasi kikubwa, hali ambayo imepelekea mgao wa maji safi na salama kwenye baadhi ya maeneo ya Jiji la Dar es salaam.

“Mtiririko katika maeneo ambayo maji yanachukuliwa yanasafirishwa na kupelekwa kwa matumizi ya watu yakiwa maji safi na salama unapungua kwa kiasi kikubwa, kwa mfano Jiji Dar es salaam linatumia Mto Ruvu , Ruvu juu na Ruvu chini, kina cha maji kinachochukuliwa kwa kawaida kwa siku katika mto wa Ruvu chini kimepungua kwa nusu nzima, nakufanya ule mchakato wa kupeleka maji kwa wananchi na wenyewe kupungua kwa kiasi kikubwa, na ndiyo maana Dar es salaam kumekuwepo na mgao mkubwa wa maji.” amesema Rais Samia Suluhu Hassan

Pia Rais Samia amesema baada ya Serikali kugundua upunfu wa maji kwenye mto huo, wamekuta baadhi ya watu wamefunga mitambo inayochepusha maji na kufanya maji yashindwe kwenda kwa wingi kwenye mto kama ilivyozoeleka badala yake wanayapeleka kwenye shughuli za kilimo, amesema hali hiyo ni uhujumu wa makusudi unaokwamisha ili kwenda kutengenezwa kufanya yaweze kuwa safi na salama ili kupelekwa kwa Wananchi kwa ajili ya matumizi ya wananchi.

“Tumekuta watu wamejenga ‘brooks’ za kuchepusha maji, yamekwenda kwenye kilimo na matumizi mengine, tumekuta magogo na madude mengine yamewekwa kuzuia maji yasiende kwenye mto, hii kuna maana mbili, moja kutumia maji kwa kilimo lakini la pili ni uhujumu wa makusudi kuzuia maji kwenda kutengenezwa na kufanya yawe maji safi na salama kwenda kwa Wananchi.” Amesema Rais Samia Suluhu Hassan

Aidha Rais Samia amesema baada ya Serikali kuendesha opareisheni kwa siku mbili kuanzia Novemba 17, 2021 kwenye maeneo yanayouzunguka mto Ruvu, wanaendelea pamoja na zoezi la kutoa mchanga kwenye mto huo ili kufanya kina cha maji kuwa kirefu kiweze kuifadhi maji ya mengi.

Vilevile Rais Samia Suluhu Hassan amesema changamoto ya upungufu wa maji inachangiwa pia na Wafugaji wanaopeleka mifugo yao mingi kwa wakati mmoja kwenye vyanzo vya maji ambavyo vinategemewa na wananchi, huku akiitaja uharibifu wa vyanzo vya maji mfano ukataji wa miti na kuendesha shughuli za kibinadamu kandokando na maeneo tegemezi ambayo wananchi utegemea kupata maji.

Ikumbukwe kwa zaidi ya wiki mbili baadhi ya wananchi wa Dar es salaam wamekuwa wakilalamilikia changamoto ya upatikanaji wa maji kwenye maeneo yao, kama ilivyozoeleka, lakini mamlaka ya maji kwenye Mkoa huo DAWASA imekuwa ikitoa sababu za zinazopelekea mgao huo akidai ni kutokana na maji kupungua kwenye mto Ruvu hali ambayo inasababishwa na upungufu wa mvua.

Hali ya uhitaji wa maji kwenye Jiji Dar es salaam ni mkubwa kutokana na uwepo wa shughuli nyingi muhimu, pia Jiji hilo ndiyo kitovu kikuu cha uchumi kwenye Nchi ya Tanzania kutokana na kuwa na idadi kubwa ya wakazi.