December 4, 2022

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

RAIS SAMIA AWATAKA WATETEZI WA HAKI BINADAMU NCHINI KUTOA ELIMU YA KATIBA KWA UMMA

Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa kufuatia tamko la Umoja wa Mataifa la Watetezi wa Haki za Binadamu la mwaka 1998 na Ibara ya 8 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali ndiye mtetezi mkuu wa haki za binadamu, lakini amewataka Watetezi wa Haki za Binadamu kulibeba jukumu la kuelumisha Umma juu ya mambo mbalimbali yanavyoelekezwa.
Akizungumza wadau wa haki za binadamu kwenye maadhimisho ya miaka 10 tokea ulipoanzishwa mtandao wa watetezi wa haki za binadamu Nchini Tanzania (THRDC), Rais Samia amesema kuwa tamko hilo pamoja na kifungu hicho cha Katiba vinaonesha kuwa Serikali ndiye mlinzi mkuu wa haki za binadamu
“Kutokana na matakwa ya tamko la Umoja wa Mataifa la Watetezi wa Haki za Binadamu la mwaka 1998 na Ibara ya 8 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, serikali ina jukumu na kwa kweli ni mtetezi mkuu wa kulinda haki za kijamii, haki za binadamu na haki za watu.” amesema Rais Samia
“Mlichosema nimefanya kazi kubwa ndani ya mwaka mmoja ilikuwa ni kazi ya kutimiza matakwa haya. Kulinda haki za watu katika nyanja mbalimbali, kuhakikisha wanapata huduma za Afya zilizo nzuri, kuhakikisha wanapata elimu njema, kuhakikisha wanapata maji ya kunywa, haki zote zile za matakwa ya msingi na haki nyingine, jinsi tunavyo kwenda kwenye ngazi za maendeleo. “- Rais Samia Suluhu Hassan
“Mtetezi mkubwa wa haki za binadamu ndani ya Tanzania ni katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo serikali ndio inayoitekeleza, ndio sheria mama ambayo ina haki zote za wanadamu wanaoishi Tanzania.”- Rais Samia Suluhu Hassan
“Swala langu kwenu, je hawa Wanadamu tunaowatetea wanaijua hiyo katiba? Nataka niache kazi kwenu, katika eneo la elimu kwa Umma muifanye kazi hiyo kuwaelewesha watu waijue katiba yao.” Rais Samia Suluhu Hassan
“Kwa sababu wanapodai haki lazima wajue na wajibu wao. Kwa hiyo haki zipo kwenye katiba na wajibu, wakieleweshwa vizuri, watajua wajibu wao ni nini kikatiba. Naomba niache jukumu hilo kwenu.” -Rais Samia Suluhu Hassan