March 23, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

RAIS SAMIA AWATAKA MAJAJI KUWA NA UTU.

Na Leonard Mapuli,Dar es Salaam

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewaapisha majaji wapya 28, saba miongoni mwao wakiwa wa mahakama ya rufani na wote amewataka kutenda haki lakini waongozwe na “Utu” katika kutimiza majukumu yao.

“Mkaongozwe na utu,Haki na nafsi zenu pia,sasa kama nafsi yako ikukutuma kwenda kuchukua fedha kwa mtu,na ukaminya haki haki ,ujue umeshateteleka” amesema Rais Samia wakati akihutubia hadhara baada ya hafla ya kuwaapisha majaji hao wapya katika Ikulu ya Rais ya jijini Dar es Salaam.

Rais Samia pia amezitaka Mamlaka zingine zinazofanya kazi na mahakama zikiwemo Polisi ,Ofisi ya taifa ya Mashtaka na Taasisi ya  kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) kuongeza kasi ya upelelezi ili kuipa mahakama ahueni ya mlundikano wa kesi unaosababishwa na ucheleweshwaji wa hukumu ya kesi mbali mbali.

Katika hotuba yake fupi,rais Samia ameeleza umuhimu wa haki katika kuleta maendeleo na hivyo kuwataka majaji wote kwenda kusimamia na kuhakikisha Haki inatamalaki.

“Kwenye Haki ndio kwenye amani na uelewano,na hapa ndipo Shughuli za Kisiasa hunawili”,ameongeza rais samia.

Majaji hao ambao uteuzi wao ulitangazwa Mei 12 ni miongoni mwa majina 232 yaliyopita katika hatua mbalimbali za mchujo kwa mujibu wa sheria na taratibu za kuwapata majaji zinavyoelekeza.

“Vigezo vilivyotumika na Kamati ndogo ya Tume ya Utumishi wa Mahakama kupata majina ilikuwa ni Pamoja na uadilifu”, amesema Profesa Ibrahim Juma,Jaji Mkuu wa Tanzania alipozungumza katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete,Ikulu ya Dar es Salaam mara baada ya kiapo kwa majaji hao.

Kuapishwa kwa majaji wapya 28 kunatajwa kwenda kupunguza mzigo katika mahakama za Tanzania ambapo kabla ya kuapishwa kwa majaji wapya 21 wa Makama kuu,Mahakama hiyo katika Masjala zake 16 zenye divisheni 4 ilikuwa na uwezo wa kusikiliza mashauri 21,861,na jaji mmoja alikuwa akihudumia mashauri 342 lakini sasa kila jaji atashughulikia mashauri 257.

Katika upande wa Mahakama ya Rufaa kabla ya kuapishwa kwa majaji 7 wapya,Mahakama hiyo ilikuwa ikisikiliza kesi kwa kuunda majopo matano ya majaji watatu na kila jopo lilisikiliza na kuamua mashauri 28-36 katika kikao kimoja,na sasa majopo yataongezeka na kufikia 7.

Kati ya majaji 28 waliokula kiapo,13 miongoni mwao ni wanawake,ambapo watatu watakwenda kuhudumu Mahakama ya Rufaa na wengine 10 Mahakama Kuu.Hii ni mara ya kwanzana kwa Rais Samia Suluhu Hassan kuapisha majaji tangu aingie madarakani,na inafanya idadi ya majaji wa Mahakama kuu ya Tanzania kufikia 91,huku wale wa Mahakama ya rufani wakifikia 24