Rais wa Serikali ya Awamu ya Sita, Samia Suluhu Hassan, amewaomba viongozi wa dini wa madhehebu mbalimbali, kuliombea Taifa kwani linawategemea.
Akizungumza katika kongamano la viongozi hao kwa ajili ya kuiombea Serikali yake, lililofanyika leo Jumanne, jijini Mbeya, Rais Samia amewaomba waendelee kuwaombea viongozi, ili waongoze kwa haki na uadilifu.
“Nawashukuru sana kwa kongamano mnalofanya, nashukuru sana kwa kweli Taifa linawategemea sana viongozi wa dini kwa maombi, sala na dua zenu. Ndiyo maana tunaweza kufanya tunayofanya,” amesema Rais Samia na kuongeza:
“Kwa hiyo mimi niwashukuru viongozi wa dini na kamati zote za amani, niwatie moyo muendelee kunifanyia hivyo. Mliombee Taifa, mtuombee na viongozi tuweze kuongoza kwa uadilifu, tuongoze kwa haki, tuongoze kama matamanio ya Watanzania. Nategemea ushirikiano wenu.”
Mwenyekiti wa Kongamano la Viongozi wa Dini la Kumuombea Rais Samia, Askofu Donald Mwanjoka, amesema wamechukua hatua hiyo baada ya kuguswa na uongozi wake.
““Nasi tunafanya hivyo tumeguswa na uongozi wako unavyoongoza tangu umeingia madarakani. Tumekusanyika hapa tuendelee kuubeba mpaka tunafika mahali tunasema kwamba ingekuwa kuna rais wa dunia, tungekuchagua uwe rais wa dunia,” amesema Askofu Mwanjoka.
Naye Askofu Antony Lusekelo, amesema Rais Samia amekuwa anatoa uongozi unaotatua changamoto za wananchi moja kwa moja.
“Nawaambia Watanzania wote, tazameni ambavyo Rais Samia anafanya kazi, sijawahi kuona Rais anatoa fedha ya Serikali kwenda kusaidia mfumuko wa bei ya sukari, lakini amefanya kitu cha ajabu sana, amesema wananchi hawataweza kubeba peke yao, serikali itabeba mzigo huo,” amesema Mchungaji Lusekelo.
Habari Zaidi
DCI KINGAI ASISITIZA WAZAZI KUZINGATIA MALEZI BORA KWA WATOTO WAO ILI KUPUNGUZA UKATILI
THRDC,C-SEMA YAENDESHA MAFUNZO KWA POLISI NA WAENDESHA MASHITAKA