December 4, 2022

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

RAIS SAMIA ATOA MUELEKEO UPATIKANAJI WA KATIBA,TUME HURU YA UCHAGUZI

Rais Samia Suluhu Hassan, amekiagiza kikosi kazi cha kuratibu maoni ya wadau wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa, kimpe mapendekezo juu ya upatikanaji wa katiba mpya na tume huru ya uchaguzi.

Agizo hilo limetolewa na Rais Samia, leo Jumatatu, Ikulu jijini Dar es Salaam, akipokea taarifa ya awali ya utendaji wa kikosi kazi hicho, iliyowasilishwa na Mwenyekiti wake, Profesa Rwekaza Mukandara.

“Hili la katiba mpya mtakwenda kulifanyia kazi, mtaleta mapendekezo. Yawe mapendekezo yatakayotangazwa Watanzania wote waelewe. Mimi nakubaliana kwamba ni jambo la muda mrefu, lakini Watanzania wote waelewe hivyo,”

“Lakini kwanza tukafanyie kazi maboresho yote tuliyosema, tufanyie kazi katika kipindi hiki cha muda wa kati. Halafu uko mbele tuone kuna haja ya kurekebisha katiba yetu? Pengine kutakuwa kuna haja sio kuandika katiba mpya,” amesema Rais Samia.

Akizungumzia kuhusu upatikanaji wa tume huru ya uchaguzi, Rais Samia ameomba apatiwe mapendekezo ili ayafanyie kazi.

“Tume huru mtatuletea mapendekezo, maana yake ni nini? Iweje? Lakini angalieni na mifano ya waliokuwa na tume huru hawana migogoro ya kisiasa? Mfano majirani zetu wanazo zinazoitwa tume huru, lakini zinaendeshwaje? Hawana migogoro,” amesema Rais Samia.

Maelekezo hayo ya Rais Samia, yametolewa baada ya Prof. Mukandara, kutaja sababu nne zitakazopelekea mchakato wa katiba mpya, usikamilike hadi kufikia 2025, ikiwemo kukosekana muda wa kutosha wa kuanza kutumia katiba hiyo ndani ya kalenda ya uchaguzi.

Rais huyo wa Tanzania, amekitaka kikosi hicho,kimpe mapendekezo juu ya utatuzi wa changamoto za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, ili zifanyiwe kazi kabla ya 2024.

“Mkae muone namna gani tunaweza tukafanya huu uchaguzi, tutoe taarifa vizuri. Kabla ya 2024 tuwe tumefanya uchambuzi na tujue tunaelekea wapi. Kwa nini huyu, kwa nini asiwe huyu, mpaka kieleweke tuelewe vizuri. Tuone njia ya kupita, kama tunaweza pita katikati ya TAMISEMI na kama sio TAMISEMI nani mwingine wasimame pamoja,” amesema Rais Samia.

Rais Samia ameagiza sheria na kanuni za uchaguzi pamoja na kanuni za maadili za vyama vya siasa, zinazosimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, zifanyiwe maboresho ili kuondoa dosari zake.

Rais Samia amesema atazungumza na vyama vya siasa ambavyo havitoi ushirikiano katika masuala mbalimbali ya kisiasa yanayoendelea nchini, ili kujua malalamiko yao kwa ajili ya kuyatatutia ufumbuzi.

“Najua kwamba kwenye vyama vya siasa hamjakaa vizuri sana, bado kuna vyama vya siasa ushiriki wao. Lakini nitaendelea ku-engage nao, kukaa na kuzungumza nao niwasikilize na nione wanataka maboresho yepi,” amesema Rais Samia na kuongeza:

“Tuwafanyie nini? Lengo ni wote twende kwenye treni moja, sio wengine wako kwenye treni, wengine wako nje, hapana. Wote tuingie kwenye treni tuendeshe siasa zenye tija kwenye Taifa letu.”