Rais Samia Suluhu Hassan, amewaagiza mawaziri wasimamie matumizi ya fedha za mkopo zilizotolewa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), ili zimalizike ndani ya muda uliopangwa.
Mkuu huyo wa Tanzania, ametoa maagizo akizindua Barabara ya Nyahua-Chaya, wilayani Uyui, mkoani Tabora.
“Matumizi ya fedha hizi mwisho mwezi ujao, tusipozitumia kuna fedha ziko njiani zinakuja lakini wanaangalia hizi tunazimalizaje. Tusipovuka asilimia 90 hatutapata fedha nyingine ina maana uwezo wetu wa matumizi ni mdogo kuliko tunazoomba, hatutapata fedha nyingine na tukipata zitapunguzwa,” amesema Rais Samia.
Rais Samia amesema “nawaagiza mawaziri mwende mkasimamie matumizi ya hizi zilizoko kwenye bomba kutemwa, zikatemwe kwa muda tuliokubaliana.”
Rais Samia amesema, kuna baadhi ya watumishi wa halmashauri wamekuwa wanachelewesha matumizi ya fedha hizo kwa sababu mbalimbali, ikiwemo utoaji tenda za ununuzi wa vifaa kwa lengo la kupata rushwa.
“Kuna fedha za UVIKO-19, mwisho wa matumizi ya fedha zile ni mwezi ujao wa Juni, 2022, hadi leo bado nasoma kuna vijitenda tenda vinacheleweshwa huko TAMISEMI, vile vitu vya kuagizwa bado tenda hazijaamuliwa, Waziri wa TAMISEMI, Innocent Bashungwa naomba ukasimamie hili,” amesema Rais Samia.
Katika hatua nyingine, Rais Samia ameziagiza Halmashauri kutumia fedha za miradi vizuri ili kuziba mianya ya matumizi mabaya ya fedha za umma.
Habari Zaidi
DCI KINGAI ASISITIZA WAZAZI KUZINGATIA MALEZI BORA KWA WATOTO WAO ILI KUPUNGUZA UKATILI
THRDC,C-SEMA YAENDESHA MAFUNZO KWA POLISI NA WAENDESHA MASHITAKA