February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

RAIS SAMIA ATOA MAAGIZO KUHUSU ATCL, TICS, MSD

Rais  wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ameagiza utendaji wa mashirika ya umma uboreshwe, ili yajiendeshe kwa ufanisi na kuleta tija kwa Taifa.

Rais Samia ametoa maagizo hayo leo Jumanne, baada ya Ripoti ya Ukaguzi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere, kwa mwaka wa fedha 2020/21, kubaini dosari kwenye uendeshaji wa mashirika na taasisi za umma.

Kiongozi huyo wa Tanzania, ameagiza utendaji wa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL), ukaboreshwe kwa kupunguza mzigo wa madeni.

Huku akiagiza baadhi ya ndege zilizonunuliwa na Serikali zikabidhiwe kwa shirika hilo, badala ya kukodishwa kama ilivyo sasa.

“Kingine kilichojitokeza ni ATCL, ambalo kwa mwaka huu wamejitahidi kupunguza kiwango cha hasara. Tumepokea pendekezo baadhi ya ndege zikabidhiwe kwa ATC ili vitabu vyao vya mali vikae vizuri, pia kuna suala la madeni iliyorithi lazima tukae tuangalie jinsi ya kuyatoa, ili thamani ya shirika ipande,” amesema Rais Samia.

Rais Samia amesema “ sababu inashushwa na madeni iliyorithi. Lakini ndege wanazoendesha ni za kukodi, ni kweli tukiwapa baadhi ya ndege vitabu vyao vya mali vitapanda bei kidogo, naagiza vikafanyiwe kazi.”

Katika hatua nyingine, Rais Samia amemuagiza Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Hussein Katanga, akafumue upya uongozi wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD), ili kuboresha utendaji wake utakaowezesha kupata tena tenda za usambazaji dawa, zinazotolewa na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

“Suala la MSD kwa kweli inataka general over rolling, kwa hiyo nakuagiza kalitizame kwa haraka kuanzia uongozi wa juu, manunuzi na vitengo vyote ili twende vizuri. Kwa sababu MSD ilifika hatua ya kupata tenda ya kuuza madawa ndani ya SADC, lakini hatua tuliyofika leo hata ndani watu wanalalamika,” amesema Rais Samia.

Wakati huo huo, Rais Samia amemuagiza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akaisimamie Kampuni ya Ushushaji Mizigo Bandarini (TICS), ili kutafuta muarobaini wa malalamiko ya kampuni hiyo kuchelewa kushusha mizigo ya meli zinayowasili nchini.

“Upande wa Mamlaka ya Bandari (TPA), meli zinakaa siku mbili hadi tatu lakini kwa upande wa TICS, zinakaa hadi siku 28. Kwa hiyo hapa sekta mkaangalie kuna nini, sababu wale ni kampuni binafsi wanafanya kazi yao, lakini waendane na mashartyi na taratibu ilizowekewa na bandari,” amesema Rais Samia.

Aidha, Rais Samia ameagiza Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC), litizamwe upya kwa kuwa mwenendo wake hauridhishi, kutokana na miradi yake kuongoza kusuasua na kutoleta tija kwa Taifa.

Pia, Rais Samia ameagiza mashirika ya umma yasiyokuwa na bodi za wakurugenzi, yapatiwe bodi hizo haraka iwezekanavyo, ili yafanye kazi kwa ufanisi.