RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ameviomba vyama vya siasa vya upinzani, viunge mkono jitihada zake za kuijenga Tanzania, akisema jukumu hilo siyo la Chama Cha Mapinduzi (CCM), pekee.
Akizungumza katika kongamano la haki, amani na maridhiano, lililofanyika leo Jumanne, jijini Dodoma, Rais Samia amesema yeye amekuwa mkarimu kwa vyama vya siasa, hivyo na wao wanatakiwa kumrudishia ukarimu, kwa kumuunga mkono kwani lengo ni kuijenga Tanzania.
Kongamano hilo limeandaliwa na Kituo cha Dwmokrasia Tanzania (TCD).
“Twendeni tukajadiliane maendeleo yanayoendelea, Tanzania yetu ilikuwa imefika uchumi wa kati wa chini, sasa hivi kazi yetu kupambana turudi na kwa mipango na jinsi ninavyoendesha Serikali, nina imani itakapofika 2025 kama hatujafika, tutakaribia.”
“Natarajia mwaka ujao tutakuwa kwa asilimia tano, miaka miwili ijayo tutakuwa kwa asilimia 6.8, hii siyo nguvu yetu Serikali, ni nguvu yetu kwa pamoja,” amesema Rais Samia.
Rais Samia amewataka wajumbe wa kongamano hilo, wampe mapendekezo ambayo yako ndani ya uwezo wake, katika utekelezaji.
“Narudia tena, tuzungumze tukiangalia hali ya uchumi wetu, lakini hali ya Tanzania yetu na mazingira. Msije mkaja na jambo ambalo mna hakika hili Rais hataweza tekeleza, naomba tuwe kama mimi, nimekuwa mrahimu kwenu,mnirudishie urahimu ili tufanye kazi pamoja tunajenga nyumba moja,” amesema Rais Samia.
Katika hatua nyingine, Rais Samia amekubali ombi la Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), anayemaliza muda wake, Zitto Kabwe, la kurekebisha Sheria ya Vyama vya Siasa, akitaka apewe mapendekezo juu ya suala hilo.
“Niingie kwenye maombi ya mwenyekiti, amesema ifikapo Julai 30 tutasherehekea miaka 30 ya mfumo wa vyama vungi, ameomba mabadiliko ya sheria ya vyama, mabadiliko yatategemea mtakavyotuletea mapendekezo na sisi tutachuja katika mazingira yetu kama itakuwa na mkanganyiko lazima tukutane,” amesema Rais Samia.
Pia, Rais Samia amekubali ombi la Serikali kuipa ruzuku TCD.
“Kulikuwa na suala la ruzuku kutoka serikalini kwa TCD, kwa bajeti ijayo mmechelewa sababu tumeshagaqa bajeti, ila linazungumzika,” amesema Rais Samia.
Habari Zaidi
DCI KINGAI ASISITIZA WAZAZI KUZINGATIA MALEZI BORA KWA WATOTO WAO ILI KUPUNGUZA UKATILI
THRDC,C-SEMA YAENDESHA MAFUNZO KWA POLISI NA WAENDESHA MASHITAKA