March 23, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

RAIS SAMIA AIPONGEZA THRDC

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ameyapongeza Mashirika Yasiyo ya Kiserikali , yanayoshughulika na masuala ya utetezi wa haki za binadamu hususan watu wenye ulemavu, ikiwemo Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC).

Pongezi hizo zimetolewa na Rais Samia, leo Jumatano, katika mkutano wake na watu wenye ulemavu, uliofanyika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.

Rais Samia amezishukuru Asasi hizo za Kiraia ikiwemo THRDC, kutokana na misaada inayotoa kwa Serikali katika kuendeleza sekta za watu wenye ulemavu, pamoja na kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo inayowagusa.

“Nitumie fursa hii kutoa shukrani zangu za dhati kwa washirika wote wa maendeleo, wanaotuunga mkono na wengine tuko nao hapa, UNICEF, USAID, UNFPA, WHO, UN WOMEN na Mtandao wa Kutetea Haki za Binadamu,” amesema Rais Samia na kuongeza:

“Tunashukuru kwa msaada mnaotupa kuendeleza sekta hii ya ndugu zetu wenye ulemavu kusukuma mipango yao na kuiweka nguvu kifedha na kusaidia kwenye mipango na kuiunga mkono Serikali kutekelea miradi mbalimbali ya kuhudumiwa walemavu.”

Mkutano huo umehudhuriwa na viongozi wa Mashirika ya watu wenye ulemavu takribani 150 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, THRDC imeshiriki kikamilifu kwa kupeleka katika mkutano huo mashirika ya watu wenye ulemavu 30 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.

Mtandao wa THRDC, kwa sasa unawanachama zaidi ya 200 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar , ambao wanafanya shughuli za utetezi wa haki za binadamu za makundi mbalimbali, ikiwemo watu wenye ulemavu,na katika kukuza kazi zake Mtandao umefungua tawi visiwani Zanzibar.