December 4, 2022

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

RAIS SAMIA AIPONGEZA THRDC

Rais Samia Suluhu Hassan, ameupongeza Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), kwa kazi kubwa iliyofanya nchini katika kipindi cha miaka 10 tangu kuasisiwa kwake mnamo mwaka 2012.
Rais Samia ametoa pongezi hizo hapo jana wakati akihutubia katika sherehe za maadhimisho ya miaka 10 ya THRDC, zilizofanyika kwenye Ukumbi wa PSSSF Tower, jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wageni mbalimbali mashuhuri kutoka taasisi za kitaifa na kimataifa,ikiwemo wanachama zaidi ya 200 wa Mtandao huo kutoka Tanzania Bara na Visiwani.
“Nitoe pongezi kwa taasisi yenu ambayo leo inaadhimisha miaka 10 toka kuundwa kwake, safari ya miaka 10 ilikuwa ndefu ina mabonde na milima. Mmepita mabonde mmevuka, mmepanda milima mmevuka na sasa mmefikia hapa mlipofika nab ado safari yenu ni ndefu mno sababu masuala ya haki za binadamu lina Nyanja kubwa ambazo linatakiwa mzifanyie kazi,” amesema rais Samia.
Katika hatua nyingine, Rais Samia alizindua ripoti ya shughuli zilizofanywa na THRDC ndani ya miaka 10 tangu kuanzishwa kwake.
Licha ya pongezi hizo, Rais Samia ametoa maagizo kwa taasisi zinazoshughulika na masuala ya haki za binadamu kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, katiba, mila na desturi za kitanzania.
Aidha, Rais Samia amewataka watetezi wa haki za binadamu waache harakati zenye lengo la kupambana na Serikali bali wafanye harakati zinazoibua masuala chanya yenye kuwasaidia wananchi.
Rais Samia amesema katika serikali yake hakuna mapambano bali kuna sera za upatanisho, maridhiano na kuwaunganisha Watanzania pamoja.
“Uanaharakati unaweza kuwa vyote, siwakatazi kuwa wanaharakati mnaweza kuwa chanya na au hasi lakini uanaharakati chanya unajenga Zaidi. Fanyeni uanaharakati ibueni maovu yanayofanyika. Njooni tukae tuzungumze,” amesema rais Samia.
Mkuu huyo wa nchi, amewataka wanaharakati hao kupeleka malalamiko yao serikalini ili yafanyiwe kazi.
“Hapa wote ni Watanzania hakuna wa kwenda kupambana na Serikali. Unapambana na Serikali kwa jambo gani? Niliwaambia wenzetu wa vyama tunapambana kwa kitu gani wote tunaendesha siasa za Tanzania, lengo letu kuijenga Tanzania,” amesema Rais Samia.
Rais Samia amesema “mnajigawa mafungu mnakwenda mnapambana, mnapambana kwa jambo gani? Ndiyo maana tukasema fanyeni harakati za haki za binadamu kulingana na mazingira ya kitanzania, kama mliokuwa wanaharakati wa aluta continua badilikeni wanangu.”
Katika hatua nyingine, Rais Samia ameshangazwa na kitendo cha watetezi wa haki za binadamu, kujikita Zaidi katika utetezi wa haki za wanasiasa, badala ya masuala yanayowagusa wananchi ikiwemo wanaopteza maisha ajalini na wanaojeruhiwa kwa mapanga na vijana wanaofanya uhalifu wa kutumia silaha maarufu kama Panya Road.
Wakati huo huo, Rais Samia alizitaka asasi za kiraia na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali, kutoa elimu ya uraia kwa wananchi hususan katiba ya nchi Ibara ya 29 na 30, ili wajue haki zao pamoja na wajibu wao.
“Ndugu zangu mtetezi mkubwa wa haki za binadamu ni katiba yetu ambayo Serikali ndiyo inaitekelza, ndiyo sheria mama ambayo ina haki zote za wananchi. Sswali langu kwenu hawa wanadamu tunaowatetea wanaijua katiba na nataka niache kazi kwenu katika eneo la elimu kwa umma,” amesema Rais Samia.
Rais Samia amesema “Muifanye kazi hiyo kuwaelewesha watu wajue katiba yao sababu wanapodai haki lazima wajue na wajibu wao.Niseme kwamba zile haki zilizobainishwa kwenye Ibara ya 29 na 30 ya katiba ziende zikajulikane kwa wananchi.”
Katika hatua nyingine, Rais Samia amewakosoa watetezi wa haki za binadamu kujikita Zaidi katika utetezi wa haki za kisiasa na kusahau haki za makundi mengine.
“Nilikuwa najiuliza utetezi wa haki kwa muda mrefu tulikuwa tumejielekeza kwenye kutetea haki lakini hata nyie wana mtandao mmejielekza Zaidi kwenye haki za kisiasa kuliko haki nyingine, nilikuwa nasema kuna tatizo kubwa la ubakaji si Zanzibar hata huku vitoto vinabakwa lakini sauti haijaja juu. Mmekuwa mkitetea haki za wanasiasda kuliko hakiza watoto,” amesema rais Samia.