February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

RAIS SAMIA AAHIDI KUMALIZA CHANGAMOTO ZA WANAFUNZI WENYE MAHITAJI MAALUM

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

RAIS Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali yake itaendelea kutenga fedha , kwa ajili ya kutatua changamoto zinazowakabili watoto wenye mahitaji maalumu shuleni.

Kiongozi huyo wa Tanzania, ametoa ahadi hiyo tarehe 7 Machi 2022, jijini Dar es Salaam, baada ya uongozi wa Shule ya Sekondari ya Benjamini William Mkapa, kumuomba atatue changamoto zinazowakabili wanafunzi wenye mahitaji maalumu.

“Niwahakikishie Serikali inajipanga kushughuliki changamoto hizi zote kadri bajeti itakavyoturuhusu, natambua baadhi ya changamoto zenu zinahitaji utatuzi wa haraka mawaziri husika wako hapa na wakiondoka wanaenda kuzishughulikia,” amesema Rais Samia.

Aidha, Rais Samia amesema Serikali inaendelea kutekeleza miongozo mbalimbali iliyowekwa kwa ajili ya kusimamia utendaji wa taasisi zinazotoa elimu maalumu na jumuishi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu.

“Serikali imeendelea na mkakati wa kitaifa wa elimu jumuishi wa 2021/22 hadi 2025/26, ambao utazingatia utoaji wa elimu jumuishi katika ngazi zote za elimu. Lengo kutoa elimu bora kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu,” amesema Rais Samia.

Rais Samia amesema Serikali yake haitakubali kuona mtoto wa Kitanzania anakosa elimu kwa sababu ya kuwa na changamoto za kimaumbilie.

“Hatutakubali mtoto wa Kitanzania akose fursa ya kielimu kwa sababu ya changamoto za kimaumbile. Tutafanya kila tunaloweza tumetoa fedha nyingi kwa ajili yenu, tutaendelea kujenga mazingira wezeshi ili watoto wote wenye mahitaji maalumu waweze kwenda shule,” amesema Rais Samia.

Kuhusu maombi ya Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Benjamini William Mkapa, Joseph Deo, ya kuboresha miundombinu ya shule hiyo ili kuwasaidia wanafunzi wenye mahitaji maalumu kupata elimu, Rais Samia ameagiza Wizara ya Ofisi ya Rais-TAMISEMI, kutoa fedha kwa ajili ya kuzitatua.

Rais Samia ameiagiza Wizara ya Elimu ijenge hosteli za wanafunzi wa kike na wa kiume katika shule hiyo, huku akiahidi kutuma mtu wa kujenga chumba maalum kwa ajili ya upimaji usikivu wa wanafunzi viziwi.