February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

RAIS DKT. MWINYI ASEMA UTOAJI HAKI KWA MISINGI YA SHERIA, USAWA HUEPUSHA MIGOGORO

Na: Anthony Rwekaza

Rais wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Dkt.Hussein Mwingi amewasisitiza watendaji wa mamlaka zinazohusika na shuguli za utoaji haki ikiwemo Mahakama kutekeleza vyema majukumu yao ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Ameyasema hayo Februari 7, 2022 wakati akifunnga kilele cha maadhimisho ya wiki ya sheria visiwani Zanzibar ambapo alikuwa mgeni rasmi, ameeleza kuwa katiba ya Zanzibar pamoja na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zimeweka msisitizo mkubwa juu ya umuhimu wa usimamizi wa haki.

“Katiba ya Zanzibar na katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweka msisitizo mkubwa katika usimamizi wa haki kwa kutambua kuwa utoaji na usimamizi wa haki ni muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii, kama inavyoelezwa kwenye kauli mbiu ya mwaka huu” Amesema Rais Dkt.Hussein Mwinyi

Pia Rais Hussein Mwinyi amesema ni muhimu viongozi katika sekta zote kuzingatia kuwa wanapotekeleza majukumu yao wanafanya Serikali pamoja na wao kukubalika katika jamii, lakini pia amedai utoaji haki kwa misingi ya sheria uiepusha jamii na migogoro hisoyo ya lazima vilevile upelekea wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za kimaendeleo.

” Ni muhimu sisi viongozi katika sekta zote tukazingatia kwamba tunaposimamia utoaji wa haki, imani ya wananchi kwa Serikali yao na sisi viongozi inaongezeka, vilevile utoaji haki kwa misingi ya sheria na usawa inaepusha jamii na migogoro hisiyo ya lazima na inawahamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo, kwa kutambua hali hiyo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendelea kuboresha taasisi na mifumo ya utoaji haki ili kuimarisha kasi ya maendeleo na ujenzi wa Nchi yetu” amesema Rais Hussein Mwinyi

Aidha Rais Mwinyi amesema ili kuwa na sheria bora amewahasa wataalamu wa sheria kuwa na ushirikiano na kuwa wepesi wa kutoa ushauri wa kisheria kwa kuzingatia taratibu, huku pia akiwataka wataalamu wa sheria kujiendeleza kitaaluma na kushiriki mafunzo mbalimbali yanayogusa maeneo mapya ya sheria kwa ajili ya kuisaidia Serikali kutekeleza mageuzi ya kiuchumi.

“Ili kuwa na sheria bora nakuhimizeni nyinyi wataalamu wa sheria mfanye kazi kwa ushirikiano na muwe wepesi kutoa ushauri wa kisheria kwa Serikali kwa kuzingatia taratibu zilizopo, aidha nakuhimizeni wataalamu wote wa sheria wa umma na binafsi kujiendeleza kitaaluma na kushiriki mafunzo mbalimbali hasa katika maeneo mapya ya sheria mpya tunayoyaitaji kwa ajili ya kutekeleza mageuzi ya kiuchumi tunayoyapanga” amesema Rais Dkt.Hussein Mwinyi

Lakini pia Rais Mwinyi amesisitiza matumizi ya lugha y kiswahili katika Mahakama na katika utungaji wa sheria mpya, amedai kuwa kwa kutumia lugha hiyo itasaidia wananchi ambao wanaweza kukosa haki zao kwa sababu ya kushindwa kuelewa vizuri lugha ya kingereza ambayo mara nyingi ilikuwa ikitumika.

Vilevile Kaimu Jaji Mkuu Zanzibar, Khamis Ramadhani awali kabla ya hotoba ya Rais Myinyi, amesema wameshirikiana na Mtandao wa Watetezi wa haki za binadamu (THRDC) ili kutengeneza ‘ Need Assessment’ ikiwa na maana kuwa ni ripoti ambayo inaonesha wananchi wanataka nini, ambapo ameeleza kuwa mchakato huo umeshaanza kwa kuwahusisha wataalamu katika kada hiyo, makubaliano hayo yanayotajwa kuwa yatachochea upatikanaji wa haki na kupunguza changamoto mtambuka zinazokwamisha upatikanaji wa haki yalisainiwa Januari 14, 2022 kwa kukutanisha pande mbili kati ya Mahakama na THRDC.

Itakumbukuwa THRDC ina siku chache tokea ilipofungia tawi lao visiwani Zanzibar, wakiwa na malengo wa kupanua wigo wa utetezi wa haki na kushirikiana na mamlaka mbalimbali kutatua changamoto zinazoweza kuwa zinakwamisha upatikanaji wa haki kwa wananchi visiwani Zanzibar.

Maadhimisho hayo ambayo ufanyika kila mwaka, yakihashiria kumalizika kwa likizo ya Mahakama na kufungua mwaka mpya, kwa mwaka huu yamebebwa na kauli mbiu isemayo “Usimamizi wa Haki ni msingi wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii”, ambapo Rais Dkt Mwinyi amewapongeza kuwa kauli hiyo inaenda sambamba ya malengo ya Serikali katika mageuzi ya kiuchumi ambayo utakiwa kuambatana na myororo mzuri wa utoaji haki kwa wananchi pamoja na wawekezaji.