February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

PROF. ASSAD AWASILISHA MAPENDEKEZO KIKOSI CHA RAIS “MTU AKIVUNJA KATIBA ANATAKIWA AONDOKE”

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), mstaafu, Profesa Mussa Assad, amewasilisha mapendekezo yake kuhusu uimarishwaji utawala bora, katika kikosi kazi cha Rais Samia Suluhu Hassan, akitaka viongozi wa umma wanaokiuka katiba waondolewe katika nyadhifa zao.
Akizungumza na wanahabari, muda mfupi baada ya kuwasilisha mapendekezo hayo, jana Alhamisi, jijini Dar es Salaam, Prof. Assad amesema, lazima nchi iongeze juhudi kwenye masuala ya utawala bora, hususan katika mihimili yake mitatu, Bunge, Mahakama na Serikali.
“Tumezungumza kuhusu namna gani tuongeze juhudi za utawala bora katika nchi, kwenye eneo lote la taasisi kama Bunge, Serikali na Mahakama, hivi vitu vitatu ni muhimu sana vikawa vinafanya kazi kama inavyotakiwa kuhakikisha katiba inatekelezwa,” alisema Prof. Assad.
CAG huyo mstaafu alisema “tulisema lazima lifanyiwe kazi kuhakikisha mtu akivunja katiba ziko namna za kumchukulia hatua, kama ambavyo akitokea mtu akavunja katiba ambayo aliiapia anatakiwa aondoke kwa hiyo hilo ndilo nililosema.”
Akizungumzia kuhusu madai ya katiba mpya na tume huru ya uchaguzi, alisema “ni vizuri kuwa na ktaiba mpya, lakini ni vizuri zaidi kuwa na watu ambao wanaweza kusimamia hiyo katiba na hilo tumesema ndiyo tatizo kubwa. Ndiyo maana miaka iliyopita tulifika mahala hatuwezi kusema chochote sababau kule juu ambaye alikuwa, hakuna mtu yeyote ambaye anaweza kumsikiliza.”