March 23, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

POLISI PUNGUZENI KESI ZA KUBAMBIKA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan hii leo amelitaka Jeshi la polisi kuharakisha chunguzi za kesi mbali mbali zilizopo ili kusaidia uharakishwaji wa usikilizwaji au ufutwaji wa kesi hizo Pamoja na kusaidia watuhumiwa kuhukumiwa ipasavyo.

Rais Samia ameeleza hayo wakati akizindua kiwanda cha ushonaji cha Jeshi la Polisi, ambacho mbali na ajira kinatarajiwa kuwa na uwezo wa kuzalisha jozi laki 125,200 za sare za Askari polisi Pamoja na Sare za makampuni ya ulinzi binafsi.

Wakati wa hotuba yake Rais Samia amelitaka jeshi la polisi kupunguza kesi za kubambikiza ambazo zimekuwa zikichelewesha uchunguzi na kusababisha wingi wa mahabusu katika magereza nchini.

Kuna mlolongo mkubwa wa makesi ya kubambikiza, sasa mlolongo huu ukipungua na mahabusu nao watapungua, kwa sababu wengi wapo wanasubiri kuhukumiwa, kesi haiendi, Ushahidi hakuna, mpelezi anashindwa kupeleka kesi kwa sababu hakuna Ushahidi

RAIS SAMIA

Mbali na hayo Rais Samia, amelitaka jeshi la polisi kutotumia sheria za kudhibiti makosa zilizowekwa kama kitega uchumi cha ukusanyaji wa tozo na faini kwa raia.

kwa hiyo niombe sana nilizungumza hili na TAKUKURU na wameweza kufuta kesi 147 ambazo waliwabambikiza watu mbali mbali huko kwa hiyo na nyie jeshi la polisi jikagueni, kama kuna za aina hiyo nazo zifutwe ili tupunguze wingi wa mahabusu kwenye majela yetu

RAIS SAMIA

Katika hatua nyingine Rais Samia ameeleza kusikitishwa na Ongezeko la vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia vilivyotajwa kuongezeka kutoka 398 mwezi Januari mwaka jana hadi kufikia 458 mwaka huu, huku  akitilia mkazo suala la malezi kwani vitendo hivi vinaanzia na wakati mwingine humalizwa na wanafamilia wenyewe.

Rais Samia amezitaka jamii kujitokeza hadharani na kutofumbia au kuficha vitendo vya unyanyasaji vinanyofanyika na kumalizika kifamilia jambo linalopelekea kuongezeka kwa vitendo hivyo.