February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

POLISI ARUSHA WATOLEA UFAFANUZI TUKIO LA KUKAMATWA KWA WANAHABARI

Na: Anthony Rwekaza

Kufuatia tukio la kukamatwa kwa Waandishi wawili wa habari Kolumba Victor (Global TV) na Alphonce Kusaga (Tripple A Radio na Kusaga Online tv) kudaiwa kushikiliwa na Jeshi la polisi katika Kituo Kikuu cha polisi Arusha (Central), ambao waliachiwa kwa dhamana.

Jeshi la Polisi kupitia Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, ACP Justine Masejo wametoa ufafanuzi juu ya taarifa ya kukamatwa kwa waandishi hao, ambapo taarifa yao imeeleza kuwa chanzo cha kukamatwa kwao ilikuwa ni baada ya watuhumiwa wawili Ester Jackson (38) na Isaya Mollel (20) ambao ni wakazi wa Ngaramtoni Mkoani Arusha kukamatwa na misokoto ya bangi 1755.

Taarifa hiyo imefafanua kuwa baada watuhumiwa hao kukamatwa na askari wa Jeshi la akiba (Mgambo) mashuhuda walifanya utaratibu wa kuwasiliana na waandishi wa habari ambapo walifika na kufanya mahojiano na mashuhuda hao kuhusu tukio la kukamatwa kwa watuhumiwa hao wawili.

Wameeleza kuwa waandishi hao walipokuwa wakihoji mashuhuda waliwasimamisha Askari hao kwa ajili ya kupata taarifa licha kudai kuwa waliwapiga picha, imeelezwa kuwa baada ya kudhania kupigwa picha mzozo ulianza baina ya askari hao na waandishi.

Baada ya kuibuka kwa mzozo huo taarifa hiyo imeeleza kuwa walifikishwa kwenye kituo cha Polisi kati (Kati) baada ya Askari hao kuomba msaada wa askari Polisi waliokuwa zamu, lakini kutokana na wananchi kukusanyika kituoni hapo, Mkuu wa kituo hicho cha Polisi aliwachukua waandishi pamoja na mgambo hao kwa ajili ya mahojiano zaidi.

Imeelezwa kuwa baada ya kuchukuliwa maelezo waliachiwa, pia taarifa hiyo inaeleza kuwa wameshachukua maelezo ya wananchi walioshuhudia mzozo mzima, huku wakiweka wazi kuwa watapeleka jarada kwenye ofsi ya mwendesha mashtaka wa Serikali DPP kwa ajili ya hatua nyingine za kisheria.

Itakumbukuwa baada ya kuenea kwa taarifa za kushikiriwa kwa waandishi hao, Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) ulitoa tamko la kulaani tukio la kukamatwa na Polisi, Waandishi wa Habari wawili Jijini Arusha ambao ni Victor Korumba Moshi wa Global TV Online na Alphonce Kusaga wa Triple A Radio wakidaiwa kuwa katika utekelezaji wa majukumu yao.

Pia THRDC kwenye tamko hilo iliwataka Jeshi la polisi kuheshimu haki za wanahabari wakiwa katika utekelezaji wa majukumu yao na walilitaka Jeshi la hilo kuachiwa kwa waandishi hao, ambapo baada ya kupokea na kuonekana kwa baadhi ya kipande cha (clip) kuonekana kinasambaa kwenye mitandao ya kijamii ikionyesha mzozo huo wakiwa kwenye kituo cha Polisi, THRDC ilifanya jitihada za kuhakikisha waandishi hao wanapata msaada wa kisheria wakiwa kituoni hapo.

Lakini nae Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa habari mkoani Arusha, alisema waandishi hao walikamatwa wakati wakitekeleza majukumu yao kufuatia tukio la Askari Polisi wa Kituo cha Sakina kudaiwa kuwapiga wananchi Feburuari 23,2022, lakini taarifa rasmi ya Polisi imeeleza tofauti na madai hayo.

Aidha AZAKI 14 kutoka Ngorongoro walitoa tamko ilo kueleza kadhia ambayo imekuwa ikiwakumba wadau mbalimbali wanaoenda Ngorongoro wakiwemo waandishi wa habari, ambopo waliishauri Serikali kupitia Waziri Mkuu kutoa maelekezo kwa wasaidizi wake kuwa pasiwepo na vitisho wala kuzuia wa habari hasa wa vyombo binafsi, waandishi wa kujitegemea pamoja na Mashirika yasiyo kiserikali kuingia kwenye mikutano ambayo imekuwa ikifanyika hasa kuhusu Ngorongoro.

“Waziri Mkuu atoe maelekezo kwa wasaidizi wake pasiwepo na vitisho,uzuiajiwa kuingia katika eneo la mkutano kwa makundi mbalimbali ikiwemo waandishi wa habari
hasa vyombo vya habari binafsi,waandishi wa kujitegemea na Mashirika yasiyo ya
kiserikali”Tamko la Azaki Ngorongoro

Hata hivyo kwenye taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi Mkoani Arusha inaeleza kuwa Jeshi hilo litaendelea kuhakikisha wananchi wakiwemo wanahabari wanaendelea kutekeleza majukumu yao kwa amani, lakini wakisisitiza kuwa hali hiyo itaenda sambamba na kuzingatia sheria na taratibu.