March 23, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

PINGAMIZI LA MBOWE NA WENZAKE KUHUSU ‘DIARY’ LAGONGA MWAMBA

Na: Anthony Rwekaza

Leo Jumatano Novemba 17, 2021 Mahakama ametupilia mbali pingamizi la utetezi la kuitaka Mahakama ifute ushahidi wa Shahidi wa pili Jamhuri H4323 DC Msemwa baada ya kukutwa na ‘diary’ kizimbani. Jaji Joachim Tiganga anayesikiliza kesi hiyo amedai kuwa hakuna sehemu imeelezwa kuwa shahidi hajui umuhimu wa kuzungumza ukweli.

Lakini kwenye uamuzi Jaji amekubali kuwa shahidi alikiuka taratibu alipofungua na kuandika katika ‘diary’ akiwa kizimbani, mawakili wa utetezi pamoja na Jamhuri wameikagua diary hiyo ambayo imekaa mahakamani kwa siku zisizopungua tatu.

Baada ya uamuzi huo Jaji Joachim Tiganga amesema kuna umuhimu wa mawakili wa utetezi pamoja na Jamhuri kwa pamoja kukagua kile kilichoandikwa kwenye diary hiyo iliyoibua utata na mvutano wa hoja baina ya pande zote mbili.

Ikumbukwe upande wa utetezi ulipokuwa ukiwasilisha hoja za kupinga tukio la shahidi kukutwa na diary na namna linavyoweza kuwaathiri wateja wao, waliiomba Mahakama kuona umuhimu kuridhia diary hiyo kukaguliwa ili kujua kilichoandikwa ndani.

Hilo linakuwa pingamizi la pili kutupiliwa mbali ndani ya siku tatu, ambapo siku ya Jumatatu Novemba 15, Mahakama ilitupilia mbali pingamizi la upande utetezi lililokuwa likiomba Mahakama hiyo kutopokea nyaraka ya barua iliyoletwa na shahidi kuwa kielelezo halali, Mahakama ilikubali kupokea kielelezo hicho na kutaka shahidi wa pili wa Jamhuri akisome Mahakamani.

Kwa sasa kesi hiyo namba 16/2021 inaendelea kusikilizwa kwa mfululizo kwenye Mahakama kuu Divisheni ya makosa ya Rushwa na Uhujumu uchumi, ikiwa inasikilizwa kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi kufuatia mawakili wa utetezi kupinga kupokelewa kwa maelezo ya mshtakiwa namba tatu Mohammed Ling’wenya, lakini washtakiwa wengine wanaotuhumiwa na makosa ya ugaidi ni Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe, Adam Kasekwa na Khalifan Bwire anayekamilisha idadi ya washtakiwa wanne.