February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

PINGAMIZI KESI YA MBOWE LATUPILIWA MBALI

Mahakama Kuu Kitengo cha Rushwa na Uhujumu Uchumi imetupilia mbali pingamizi lililowasilishwa na upende wa utetezi kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza mashitaka ya ugaidi yanayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA,Freeman Mbowe na wenzake watatu.

Akisoma uamuzi huo Jaji Luvanda amesema mahakama hiyo ina uwezo wa kusikiliza mashauri ya ugaidi kwa mujibu wa sheria ya Uhujumu Uchumi ya mwaka 2019 na sheria ya Kuzuia Ugaidi ya mwaka 2002 na kulingana na sheria hiyo makosa ya ugaidi ni miongoni mwa makosa ya uhujumu uchumi yanayoweza kusikilizwa na mahakama Kuu Divisheni ya Rushwa na Uhujumu uchumi.

Baada ya kutolewa kwa uamuzi huo Wakili wa Serikali Robert Kilanda aliiomba mahakama hiyo kubadili maelezo katika hati ya mashitaka yaliyoeleza kuwa Aishi Hotel ipo katika wilaya ya Moshi na badala yake iandikwe Hai ambapo Hoteli hiyo ipo, ombi ambalo lilikubaliwa na mahakama.

Aidha Wakili wa utetezi,Peter Kibatala ameiambia mahakama kuwa ana hoja za kisheria za mapingamizi kuhusu taarifa zilizowasilishwa katika hati ya mashitaka kuwa na kasoro, hoja ambayo imepingwa na wakili wa serikali ambaye ameiomba mahakama kuendelea na shauri hilo.

Kutokana na kuwepo kwa mgongano wa kisheria mahakama imetoa dakika 15 kwa upande wa utetezi kuwasilisha mapingamizi hayo kwa njia ya maandishi.