February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

PINGAMIZI KESI YA MBOWE DHIDI YA MWANASHERIA MKUU, IGP, NA DPP, HOJA KUWASILISHWA KWA MAADISHI, MAAMUZI KUTOLEWA SEPTEMBA 23, 2021

Na: Anthony Rwekaza

Kesi ya Kikatiba namba 21/2021 iliyofunguliwa na Freeman Mbowe dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP) na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), imesomwa leo Jumatatu Agosti 30, 2021 kuahirisha kufuatia Jaji wa Mahakama Kuu, John Mgetta kuridhia ombi la mawakili wa utetezi(Jamhuri) kuomba kuwasilisha hoja za mapingamizi manne kwa njia ya maadishi ambavyo pande zote zimeridhia.

Jaji John Mgetta baada kusikiliza maelezo kutoka kwa mawakili wa pande zote mbili, ambao kwa pande Jamhuri waliongozwa na Wakili Mkuu wa Serikali Hang’i Change na Deodatus Nyoni huku upande wa Freeman Mbowe akiwakilishwa na mawakili saba wakiongozwa na Wakili Peter Kibatala, Nashoni Nchunga, Sisty Aloyce na Marko Lugina, ametoa muda wa pande hizo kuwasilisha hoja zao.

Upande Jamhuri ambao umeweka pingamizi hilo utatakiwa kuwasilisha hoja hizo t September 9, 2021 huku upande uliofungua mashtaka utawasilisha hoja zake September 13, kabla ya kusomwa kwa maamuzi ya mapingamizi hayo September 23, 2021 saa tatu asubuhi.

Kati ya mapingamizi hayo manne moja ni kutaka kesi hiyo iondolewe Mahakamani kwa madai kuwa utaratibu uliotumika kufungua kesi ulikiuka sheria na taratibu huku wakiomba mapingamizi hayo yasikilizwe kwa maadishi mbele ya Jaji wa Mahakama kuu John Mgetta.

Freeman Mbowe ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, alifungua kesi ya kikatiba Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam akidai kuwa alivujiwa haki za kikatiba wakati wa alipokamatwa akiwa Jiji Mwanza Julai 21, 2021 na baada ya kukamatwa walikiuka katiba na sheria kuhusu utaratibu kumkamata, kumpekua na kumuweka kizuizini muda mrefu bila kupelekwa Mahakamani.

Pia Mbowe kwenye kesi hiyo anaiomba mahakama itamke kuwa DPP na IGP pamoja na Mahakama ya Kisutu, ikitenda kwa amri ya DPP na AG, walikiuka haki zake zinazolindwa na masharti kifungu cha 29 (2) na (3) cha Sheria ya uhujumu uchumi kwa kushindwa kumjulisha kwa maandishi kwamba atashtakiwa kwa mashtaka mazito chini ya Sheria ya Kuzuia Ugaidi na Sheria ya Uhujumu Uchumi.

Vilevile Mbowe anadai kwa makusudi walishindwa kumuwezesha kupata fursa na njia za mawasiliano ili kuwasiliana na wakili na au ndugu zake kuhusiana na kufikishwa mahakamani kabla na wakati wa kufikishwa kortini na kusomewa mashtaka bila huduma za mawakili ambapo anadai kwa kufanya hivyo walikiuka haki zake za msingi.

Ikumbukwe Mwanasiasa huyo alifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi kisutu Dar es Salaam na kusomewa mashtaka ya ugaidi yeye pamoja na wenzake akidaiwa kula njama ya kufanya ugaidi kwenye kesi namba 63/2021 ya uhujumu uchumi, ambapo kesi ilianza kusikilizwa kwenye Mahakama hiyo kabla ya Hakimu Thomas Simba Jumatatu Augosti 23, 2020 kuihamisha kwenye mahakama Kuu kitengo uhujumu Uchumi ambapo itasikilizwa Jumanne Agosti, 31 2021.

Freeman Mbowe akiwakilishwa na mawakili wake alifungua kesi hiyo Julai 30, 2021 na kwa mara ya kwanza ilianza kusikilizwa Agosti 9, 2021 ambapo Upande wa Jamhuri uliweka pingamizi.