February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

PASIPO MAONO WATU HULA NYASI!LAKINI MAONO NI NINI BASI?

Denis Mpagaze


 1. Maono ni kuona kesho ukiwa leo. Mzee aliyefoji vyeti aliamua kustaafu kwa hiari baada ya kusikia Magufuli ameshinda Urais wa Tanzania kwa sababu aliona giza mbele kwa wenye vyeti feki na kweli baada ya kustaafu zake panga la vyeti feki likapita, wakati wenzake wanafyekwa vichwa yeye anafyeka pensheni yake ya milioni 138! Waswahili wanasema machale yalimcheza. Wahenga tunasema aliona kesho akiwa leo! Alikuwa na maono! Maono ni kuona mambo yajayo kwa macho ya akilini.
 2. Maono ni kutekeleza jambo akilini kabla halijaonekana machoni. Kijana mmoja aliona tangazo la kazi ya ulinzi, akaanza kufanya kazi za ulinzi kichwani kwake ya kuongoza magari, akifungua geti, akishusha bendera, akiwapa kitabu cha kusaini wageni, kisha akaenda kwenye mbao ya matangazo, akabandua lile tangazo na kwenda nalo hadi kwa meneja wa ile kampuni. Meneja akashangaa, “mbona umeng’oa tangazo la kazi? Kijana akasema, “Tangazo halihitajiki tena, mlinzi nimeishapatikana, nimekuja.” Meneja alicheka kisha akampa kazi ya ulinzi kijana. Unapotaka jambo anza kulifanyia kazi ofisini ili ibaki kazi ya kuliprint tu.
 3. Maono ni uwezo wa kupanga kesho yako akilini kwako. Dubai ya leo ni matokeo ya kazi iliyofanyika akilini kwa kiongozi wao Sheikh Mohammed bin Rashid Al Maktoum. Baada ya kuona mafuta yatakwisha akajenga vivutio vya utalii kichwani, alipomaliza akaviprint dunia ikashangaa. Leo jengo refu kuliko yote duniani liko Dubai. Linaitwa Burj Khalifa! Lina urefu wa mita 830, ghorofa 163 kwenda juu; lina nyumba za kuishi, hoteli, supermarkets, maduka na ofisi kibao.
 4. Leo kisiwa cha kuvutia duniani kipo Dubai. Kinaitwa Palm Islands. Walijaza mawe na mchanga kwenye kina kirefu cha bahari kisha wakashusha mijengo ya kufa mtu. Hata David Bekham anamiliki mjengo pale. Aliununua kwa pesa za kufa mtu. Leo shopping Mall kubwa kuliko zote duniani iko Dubai. Inaitwa Dubai Mall. Ukubwa wake ni sawa na viwanja 50 vya mpira wa miguu. Ina hoteli za kifahali 250, pakingi za magari 14,000, maduka 1200 na dude la maonyesho ya viumbe wa majini. Linaitwa Dubai Aquarium and underwater zoo. Ndo kubwa kuliko yote duniani. Limenjengwa kwa vioo tupu. Lina ujazo wa lita millioni 10 za maji. Linazaidi ya aina 300 za viumbe wa baharini. Kwa mwaka wanatembelea wageni hadi 84 milioni na wote wanalipia.
 5. Leo hii Airport busy kuliko zote duniani iko Dubai. Kila baada ya dk 5 ndege inatua na nyingine inapaa. Kwa siku zinatua zaidi ya ndege 2,000. Yaani Dubai kila dakika wanamiminika maelfu ya watalii, wafanyabiashara na wala bata kutoka pande zote za Dunia. Hii inaitwa “you build it, they will come”. Leo Dubai ni kona ya Dunia kutoka kuwa janga. Sasa sikiliza maneno ya Mswahili baada ya kumsimulia maono ya Dubai. “Mpagaze, Dubai Sikanyagi, ng’oo! Hayo ni majanga tupu, huwezi kunipandisha ghorafa ya 163. Hata hicho kisiwa sikanyagi ng’oo! Hata huko kwenye masamaki siendi. Hivi akitokea mwehu mmoja akavunja hicho kioo si itakuwa balaa? Hakika pasipo maono watu wanakula nyasi.
 6. Mtu bila maono ni mtu bila wakati ujao. Mtu bila wakati ujao huishi kurudi nyuma. Anakuwa mtu wa kukumbuka miaka iliyopita kwa mabaya; utasikia mwaka jana ulikuwa mwaka wa shetani kwangu; mwaka juzi ndo nilipata ajali; mwaka uliopita muda kama huu ndo nilinusurika kufa! Huyu hawezi kuchungulia kesho. Kuna mtu kila dakika kwa mazungumzo yake utasikia tulipokuwa pale London, nilipokuwa sijaoa, enzi za ujana wangu! Huyu aliishapoteza dira. Mbele anaona giza kama wana wa Israel. Walivyotikiswa kidogo walitamani kurudi utumwani kama wale vijana waliomwambia Nyerere heri enzi za ukoloni.
 7. Ukiwa na maono ni rahisi kuvumilia nyakati ngumu unazopitia maana una picha nzuri akilini kuhusu kesho yako. Binti anakwenda kuolewa analia kuwaacha wazazi wake lakini harudi nyuma kwa sababu anapicha kubwa akilini kwake kuhusu maisha ya ndoa zaidi ya kuwaacha wazazi; mpishi anakata vitungu hadi machozi yanamtoka lakini haachi kukata vitunguu kwa sababu ana picha kubwa akilini kwake kuhusu utamu wa kitunguu kwenye chakula kuliko maumivu ya kitunguu machoni; mwanamke aliyebeba mimba na kuzaa kwa uchungu bado atabeba nyingine tena kwa sababu maono yake kuhusu uzazi ni makubwa kuliko karaha za mimba.
 8. Mkulima anabeba jembe lililomkata shambani na kurudi nalo nyumbani badala ya kuliacha huko kwa sababu maono yake ni makubwa kuliko jeraha la jembe; jamaa mmoja alipotoka jela na kukuta mke wake amezalishwa watoto wanne hakupoteza muda kutaka kujua nani alisababisha kwa sababu maono yake ya kutafuta pesa na kuanza maisha mapya yalikuwa makubwa kuliko aliyemzalisha mke wake! Ukibeba maono lazima kwanza ukubali kuonekana chizi machoni pa watu. Lugha yako itabadilika na maamuzi yako yatawashangaza wengi.
 9. Maisha yenye maoni yanatia hamasa, maono yatakufanya uinuke mara saba unapoanguka mara tatu. Wenye maono hawakasirishwi na kila mtu. Eti unakutana na mtu anakonda kwa sababu mchumba wake kamcheat, amekosa hamu ya kula; hivi kabla hujakutana naye ulikuwa huli? Unatoa wapi muda huo? Hii ni kwa sababu huna maono! Ungekuwa na maono usingepoteza muda wako na mtu asiyekujali! Mtu mwenye maono makubwa atakuwa busy kuyatimiza, hana muda wa kumrushia mawe kila mbwa anayebweka. Kubweka ni tabia ya mbwa! Kuna watu ni tabia yao kubweka. Ukipewa nafasi kuzungumza ukatumia muda mfupi wanasema hujajiandaa, ukitumia muda mrefu wanasema hutunzi muda!
 10. Maisha bila maono yanaboa! Maisha bila maono ni sawa na kupanga tofari. Mafundi wawili walikuwa wanajenga jengo moja; walipoulizwa wanafanya nini, wa kwanza alijibu napanga tofari, wa pili akajibu najenga shule. Wa kwanza hakuwa na maoni ndo maana aliona tofari mbele yake, wa pili aliona shule kwa sababu alikuwa na maono. Mtu asiyekuwa na maono anaishia kuona macho yanapoanzia, mwenye maono ananzia kuona pale macho yanapoishia. Maono ni kuona wasivyoviona wengine. Kuangalia ni kazi ya macho bali maono ni kazi ya moyo.
 11. Mwanafunzi alimjibu mwalimu aliyempa adhabu ya kupiga magoti kwa kosa la wengine hivi, “Mwalimu unaweza kudhani nimepiga magoti lakini kwa taarifa yako moyoni nimesimama.” Hata wale wanafunzi wakati wamemfuata Nyerere kupinga suala la JKT walimwambia unaweza kutulazimisha kwenda huko, tutakwenda lakini mioyo yetu haitakuwa huko! Mwenye maono anaona mbali, asiyekuwa nayo huona mbele! Mtu asiyekuwa na maono ukimwambia achague shilingi 50,000 leo au 200,000 kesho, atachagua 50,000 ya leo.
 12. Maisha bila maono yanaboa. Kazi bila maono inaboa. Watu wengi hatufurahii maisha kwa sababu tunafanya kazi tusizozipenda ndo maana malalamiko hayaishi! Unamka asubuhi, unakwenda kazini, unarudi, unapitia baa, unalewa, unafika nyumbani unafungua mlango kwa buti na wakati una mikono, yaani umekuwa kero hadi watoto wako wanaulizana baba yao utakufa lini. Uko bored kwa sababu unatekeleza ndoto za wengine ndo maana ukisikia holday unashangilia maana huna cha kupoteza, mashine ya ofisi ikiharibika unashangilia kwa sababu siku hiyo mtapumzika! Hujui mwekezaji anapata hasara kiasi gani! Hayakuhusu!
 13. Ukiwa na maono utajihisi mwenye deni. Maono humpa mtu msukumo wa kuamka usiku wakati wengine wamelala na kuchapa kazi. Maono humpa mtu nguvu za kuukomboa wakati. Maono humpa mtu ujasiri wa kusimamia kile anachokiamini kwa jasho na damu. Maono yatakusaidia kuwa mwekezaji badala ya mtumiaji, utakuwa mtendaji badala ya mlalamikaji; mtunza muda badala ya mtupa muda! Kwanza muda hautupwi, wewe ndo unatupika!
 14. Maisha bila maono ni sawa na bendera kufuata upepo. Utakuwa kama yule msindikizaji alipofika station, wakakuta treni ndo inaondoka, wakaanza kuikimbiza, mmoja akaishika na kupanda, akaondoka nayo, huyu mwingine akabaki anacheka hadi anaishiwa nguvu, watu wakamuuliza kulikoni? Akawaambia mie ndo nilikuwa nasafiri, sasa aliyepanda treni ni msindikizaji. Ndo maisha bila maono utasafiri bila kujua unakwenda wapi! Kama hauna maono hata chizi anaweza kuyaendesha maisha yako. Hapo jiandae kula nyasi.
 15. Kuishi katika kijiji kisichokuwa na zahanati na wakati mbunge wenu anashangaa mataa kwenye bunge la Ndugai ni kula nyasi; kushindwa kulipa kodi ya nyumba na wakati unapata mshahara kila mwezi ni kula nyasi; kukatikiwa mafuta kwenye gari lako njiani na wakati ni mtumishi wa serikali ni kula nyasi; kukurupushana kwenye ndoa kila siku na wakati hakuna aliyewalazimisha kuingiemo ni kula nyasi; wala nyasi ni wengi!
 16. Ukiwa na maono mabaya utapata matokeo mabaya, ukiwa na maono mazuri utapata matokeo mazuri. Mke na mume walikuwa wezi sana. Sasa siku mke amebeba mimba, mume alipiga picha akili jainsi mtoto wao atakavyokuwa mwizi kuliko wao. Na mke wake naye akapiga picha hiyohiyo. Siku mama amemaliza kujifungua alisikia mkunga akilalamika kupoteza pete yake ya ndoa. Walipokunjua vidole vya mtoto waliikuta hiyo pete. Unapowaza kitu akilini kinatokea machoni. Hii Hadithi alitusimulia Pd Kamugisha!
 17. Maono ni kuona ambacho hakionekani. Kwa mtu asiyekuwa na maono, jana na leo ni sawa. Huna maono utaishia kumtupia mawe kila mbwa anayekubwekea ukiwa safarini. Huwezi kufika kwa sababu hujui unakokwenda. Maono bila vitendo ni ndoto. Zinapatikana sana huko makanisani wanakopokea makontena kutoka akilini kutokea China na kushindwa kuyaprint! Sikiliza mpendwa ukiishalipokea Kontena akilini kutoka China anza mchakato wa kulileta mtaani kwenu sasa Mchungaji na Waumini wenzako walione, wakubariki!
 18. Kama una maono ya kuwa na kampuni yako, anza mazoezi ya kumiliki kampuni yako kichwani. Ingia ofisini, salimia wafanyakazi wako, endesha vikao vya kampuni, lipa mishahara, wape onyo wazembe, yaani fanya kila kitu wanachofanya wamiliki wa kampuni. Mshukuru Mungu kila siku dakika kumi kabla hujalala na dakika kumi unapoamka kwa ajili ya kampuni yako! Biblia inasema ukiwa na imani kidogo kama punje ya haradani unaweza kuhamisha milima. Nakwambia lazima utafungua kampuni tu! Kikubwa hakikisha hakuna kitu cha kukutoa kwenye reli.
 19. Mwenye maono hapoteza muda. Huwezi kumkuta na watu wasiojua wanakwenda wapi; kuna watu lazima waondoke kwako ndo ufanikiwe, Ibrahimu alizungumza na Mungu baada ya Ruthu kusepa. Kuna mahusiano lazima yavunjike ndo ufanikiwe; kuna ndoa lazima zivunjike kwanza ndo ufanikiwe, hasa kama ndoa hiyo haikuanza na Mungu. Ndoa imeanzia uzinzini, inafungiwa madhabahuni na kurudi uzinzini kwa sababu jasiri haachi asili halafu unaogopa kuivunja ati kilichounganishwa na Mungu hakiwezi kutenganishwa na mwanadamu. Acha utani bana! Mumezinzika kabla ya ndoa hadi shetani akaona gere halafu unasema Mungu ndo kawaunganisha! Uliona wapi!!!!
 20. Kama huna maono yako basi usiharibu maono ya mwenzako. Kumlazimisha mtoto kuwa kama wewe ni kuharibu maono ya mtoto wako! Eti kwa sababu ulikuwa Injinia unataka na mwanao awe Injinia na wakati Hesabu anapata namba za viatu! Tujifunze kwa wakulima. Hakuna mkulima anayetamani mwanaye awe mkulima kama yeye! Hayupo! Tuwasikilize watoto kujua maono yao tuyapalilie. Haijalishi ni wadogo kiasi gani. Waulize wanataka kufanya nini. Usiwapangie tu.
 21. Yese alimpangia mtoto wake Daudi kazi ya kuchunga mbuzi na wakati Mungu alimleta kuwa nabii. Ongea na wanao mambo makubwa, siyo kila siku habari za pilau na nguo za sikukuu! Ukienda safari watoto watakuagiza vyakula badala ya vitabu! Jenga utamaduni wa kuwapeleka watoto wako kwenye semina na makongamano ya maana, wakutanishe na watu wenye akili! Huko watapata ndoto kubwa!
 22. Orville na Wilbur watoto wa Mzee Milton Wright na Susan na Bi Catherine Koerner Wright WA Marekani maarufu kama The Wright brothers walivumbua ndege kutokana na vindege vya kuchezea waliyoletwa na baba yao. Walianza kujenga taswira akilini mwao kuwa ndege moja inawarusha hewani. Wote wakashikilia maono hayo, wakaunda ndege na kuvunja rekodi ya dunia. Unapopata maono ya jambo fulani, ukaanza utekelezaji wake akilini kuna nguvu hufungua kile unachohitaji kufanikisha maono yako. Kikubwa weka imani, bidii na akili!
 23. Lakini pia usiogope kuonekana mkaidi pale unaposimamia maono yako. Ukitaka kuonekana mweemaa kwa kutii kila mtu utashindwa kutimiza maono yako! Kumbuka mti ulionyoka ndo unaokatwa! Baba yake Arnold Swhwarzenegger alitaka mwanaye awe mwanajeshi lakini dogo akagoma, ndoto yake ilikuwa uigizaji. Alivyowaeleza hivyo wazazi wake hawakumuelewa na kumpeleka jeshini kwa lazima lakini mwishi wa siku alitoroka jeshini na kwenda kutimiza ndoto yake! Leo Arnold Swhwarzenegger anajulikana dunia nzima. Sikiliza roho yako maana roho yako ndo inajua uachotakiwa kupata, baba yako, mke wako na jamaa zako.
 24. Katika maisha tafuta watu wanaomini katika maono yako, wakimbie watu wanasioamini ndoto yako; tafuta mke anayeamini katika maono yako maana huyo hatasumbuliwa na leo yako ilivyo maana anaiona kesho yako yenye mafanikio; achana na akina filisika tujue tabia ya mkeo! Kichwa kimebebwa na shingo imara shingo ikiyumba mwanaume umekwisha. Mke mwenye maono atajua mwisho wa safari yako kabla hujaianza. Wakati wengine wanalalamika kuhusu leo iliyojaa shida yeye anamsifu Mungu kwa kuwa ameishaiona kesho yako ya furaha.
 25. Je unaishi ili kutimiza siku au unatimiza siku ili uishi? Unakaa na watu wenye story za kula kitimoto iliyokaushwa vizuri na pilipili kwa mbali unategemea kutoka salama? Sikiliza kama unampango wa kuchomoka kimaisha kaa na watu wanaoongelea mabilioni hata kama huna kitu mfukoni! Lazima utatengeneza pesa hizo akilini na baadaye utaziprint. Lakini wakati mwingine unanishangaza sana. Rafiki zako wakiondoka unasema ni wajinga, halafu bado kesho nakuona uko nao. Ni kwa sababu huoni kesho! Unaishi na mke anayekupa changamoto za kula bata halafu unasema unampango wa kutoboa. Nani alisema! Umetulia kabisaaa na mume mla bata kwenye nyumba ya kupanga! Acha kupoteza muda.
 26. Mwenye maono anavalue muda. Hapotezi muda kwa sababu ukipoteza muda muda utakupoteza. Utakufa ni lofa na kufanya historia ya marehemu kuwa fupi sana siku ya mazishi yako. Marehemu alizaliwa, akazurula akafa! Unashinda na wafanyabiashara wadogowadogo lazima ubaki huko.
 27. Huna maono utaishi maisha bendera fuata upepo. Ukisikia oya tugome; unagoma bila hatakuelewa maana ya kugoma. Sikiliza kugoma ni kuweka presha kwa mtu mwenye akili kuliko wewe afikiri kwa niaba yako alisema Mwakasege. Yaani atatute matatizo uliyoshindwa kutatua.
 28. Maisha bila maono ni sawa na kufungua saluni kwenye mtaa wa watu wenye vipara tu. Jamaa alikwenda kijijini akakuta watu wote wanatembea peku, wakapeleka kontena la viatu wakidhani ni fursa; kufika wakaambiwa kutembea peku ni jadi ya wale watu. Wakivaa viatu wanachekwa. Ni sawa na kumuona Mrisho Mpoto peku barabarani unataka kumnunulia viatu. Huna maono utaishi kama mpiga ramli!
 29. Kuna familia ilihamia mtaa mpya na kila asubuhi waliona jirani yao kaanika nguo hazijatakata vizuri, basi mama akawa anajiuliza hivi hawa hawajui kufua? Siunajua majungu tena. Siku moja wameamka asubuhi wakaona jirani kaanika nguo zimetakata. Mama akauliza mume uliwatonya nini? Maana naona leo nguo zimetakata. Baba akasema hapana kuna kitu nimefanya. Leo nimeamka asubuhi sana nikasafisha madirisha yetu ndo maana umeona vizuri. Safisha dirisha la macho yako uone vizuri!
 30. Ndugu zake Yusufu walishindwa kusafisha madirisha wakamuona mdogo wao mkuda, wakamuuza; mke wa mfalme akamuona Yusufu sukari akamtamani; mafalme akamuona Yusufu mfungwa akamfunga; Mungu akamuona Yusufu kiongozi akampa uongozi! Unahitaji macho ya rohoni kuona uzuri wa kitu kilichopo mbele yako.